![]() |
Sheikh Majid Saleh |
Na Joyce Ngowi
UONGOZI wa Msikiti wa Sunni Muslim Jamatin umesema unatarajia kumfikisha Mahakamani Waziri wa Mambo ya Ndani, Shamsi Vuai Naohodha kwa kuuengua uongozi wa Kamati ya muda iliochaguliwa kihalali na waumini wa Msikiti huo kwa madai kuwa hautambuliki.
Hali hiyo imekuja baada ya mgogoro wa kugombea madaraka katika msikiti huo kudumu kwa muda mrefu sasa kitendo kilichosababishwa kuundwa kamati ya Muda kuelekea mchakato wa Katiba mpya ambayo ingefanya uandaliwe uchaguzi wa kuwapata viongozi wapya.
Akizungumza na wandishi wa habari, kiongozi wa kundi la viongozi walionguliwa madarakani, Sheikh Maggid Saleh Mohammed alisema wanatarajia kwenda Mahakamani Mei 2 mwaka huu kupinga kitendo cha waziri huyo kwani kimekiuka sheria na kuingilia imani ya dini hiyo.
Alisema kuwa lengo lao ni kuitaka mahakama kuusimamisha uongozi huo mpya ulioingizwa kimahaba na waziri huyo hadi hapo pande hizo mbili zitakapofikia muafaka na kuandaliwa uchaguzi mpya kama ilivyo agizwa na mahaka hapo awali.
"Kitendo alichofanya Waziri, Nahodha siyo cha kiungwana kwani kwanza amepingana na amri ya mahakama lakini pia hakiendani na imani ya dini yetu na tatu analeta siasa kwenye dini na kuingiza tabaka la kizanzibari na kibara,"alisema
Alisema kitendo hicho ni cha ubaguzi kutokana na viongozi ambao, Nahodha aliowaweka madarakani wote ni wazanzibari wenzake hivyo amekiuka madaraka yake kwa kuonesha upendeleo wa wazi kwa kuwabagua watu wa Tanzania Bara.
Mohammed alisema Waziri alionyesha udhaifu katika maamuzi yake kwani katika muda wa siku mbili aliweza kuwapa haki Kamati ya muda kisha kubadilika na kuwapa Wazanzibari wenzake uongozi.
Alimtaka Waziri, Nahodha kutii sheria za nchi kwani mahakama iliagiza usifanyike uchaguzi wala mkutano wowote hadi pande hizo zitakapokaa kwa pamoja kisha kupanga jinsi zitakavyoendesha uchaguzi.
Alisema haipendezi migogoro ya kidini kutatuliwa mahakamani lakini hali hiyo imesababishwa na chombo ambacho kingesimamia migogoro hiyo Baraza la Kuu la Waislam Nchini (Bakwata) kushindwa kabisa kutekeleza majukumu yake kutokana viongozi wake wengi kujiingiza zaidi katika maswala ya kidunia.
Pamoja na mpango wao wa kumshtaki waziri huyo na uongozi uliopo madarakani kinyume cha taratibu za imani ya dini hiyo, Shekh Saleh alisema upo muda wa kiongozi huyo kutengua uamuzi wake na kuuomba radhi uongozi wa imani ya dini hiyo kwa kuwatendea mambo yasiyostahili.
No comments:
Post a Comment