TANGAZO


Sunday, April 1, 2012

Newcastle yaisasambua Liverpool 2-0

Mabao mawili yaliyofungwa na Papiss Cisse yamezidi kuiongezea Newcastle hamu ya kucheza mashindano ya Ulaya msimu ujao baada ya kuongeza machungu kwa Liverpool iliyocheza na wachezaji 10 tu katika pambano la Ligi Kuu ya Kandanda ya England.
Papiss Demba Cisse aliyewalaza Liverpool
Papiss Demba Cisse aliyewalaza Liverpool

Cisse alitumbukiza mpira kwa kichwa baada ya kulishwa mpira wa juu na Hatem Ben Arfa katika kipindi cha kwanza kabla ya kufunga bao la pili alipopokea pasi ya Demba Ba katika nusu ya pili ya mchezo.
Kiwango cha chini ya kandanda kilichooneshwa na Liverpool, ambapo mshambuliaji wao wa kati Andy Carroll alioneshwa kadi ya manjano baada ya kujiangusha kwa makusudi katika eneo la Newcastle, pia ilishuhudia mlinda mlango wao Pepe Reina kutolewa nje kwa kuoneshwa kadi ya nyekundu.
Na kwa sasa Liverpool wamekwishapoteza michezo sita kati ya saba ya ligi.
Reina alioneshwa kadi nyekundu baada ya kuchezewa rafu na James Perch alipokuwa akijiandaa kufunga mpira uliopigwa na Mike Williamson.
Lakini baada ya kugongana na mlinzi huyo wa Newcastle, Reina alimtwanga kichwa Perch na mwamuzi Martin Atkinson hakuwa na njia nyingine ya kufanya ila kumtoa nje kwa kadi nyekundu.
Kilikuwa kipindi kingine cha kushuhudia vijana wa Kenny Dalglish wakinyanyaswa, ambao katika msimamo wa ligi wanashikilia nafasi ya nane, pointi 11 nyuma ya Chelsea wanaoshikilia nafasi ya tano.
Na kwa wenyeji Newcastle, matokeo hayo yamewainua na kufikisha pointi sawa na Chelsea wakiwa wanatafuta nafasi muhimu ya kumaliza msimu kwa kucheza Ligi ya Ulaya.

No comments:

Post a Comment