Nchini Mali wapiganaji wa kabila la Tuareg, ambao wameteka maeneo kadha hivi karibuni, wanasema sasa wameuzingira mji muhimu kwenye jangwa, Timbuktu.
Taarifa zinasema risasi zinasikika katika mitaa inayozunguka mji.
Jumamosi wapiganaji hao walidhibiti mji muhimu mwengine wa Gao, ambao una ngome kubwa kabisa ya jeshi kaskazini mwa nchi.
Kiongozi wa wanajeshi walioasi na kunyakua madaraka nchini Mali juma lilopita, Amadou Sanogo, alisema wanajeshi waliacha Gao itekwe, ili kuepusha maafa katika maeneo ya makaazi.
Baada ya mapigano ya siku nzima kwenye eneo la mji wa Gao, wanajeshi wa Mali waliondoka kwenye makambi mawili, ikiwemo ngome kubwa kabisa kaskazini mwa nchi.
Kiongozi wa mapinduzi ya Mali, Kepteni Amadou Sanogo alisema kwenye televisheni ya taifa, kwamba jeshi liliamua lisipigane kwa sababu kambi ziko karibu na maeneo ya makaazi.
Kwa hivo wapiganaji wanasema wanaudhibiti mji huo wenye ngome.
Ripoti zimesema kumetokea hasara lakini idadi haikutajwa.
Hilo ni fanikio kubwa kwa wapiganaji wa kabila la Tuareg katika vita vyao vya kuania uhuru wa eneo la kaskazini.
Timbuktu, mji wa kale, ndio mji mkuu pekee wa kaskazini uliobaki mikononi mwa jeshi.
Lakini wapiganaji wanasema tayari wanaizingira Timbuktu, na wakaazi wanasubiri mapigano ambayo yanaweza kuzuka wakati wowote.
Jumuia ya Afrika Magharibi, Ecowas, imeweka tayari wanajeshi 2,000, iwapo itahitajika kuingilia kati nchini Mali.
No comments:
Post a Comment