TANGAZO


Sunday, April 15, 2012

Manchester United yajichimbia kileleni

Manchester United imeongeza wigo wa pointi hadi tano dhidi ya Manchester City kileleni mwa Ligi Kuu ya Kandanda ya England lakin i ushindi wao dhidi ya Aston Villa uligubikwa kwa mara nyingine na penalti iliyoonekana ni ya utata.

Manchester United wazidi kujiimarisha kileleni
Manchester United wazidi kujiimarisha kileleni

Ashley Young, ambaye alifanikiwa kupata penalti wakati Manchester United walipocheza na QPR, kwa mara nyingine alifanikiwa kupata penalti baada ya kutegewa na Ciaran Clark.
Kuguswa huko kwa Young kulikuwa kudogo sana lakini Wayne Rooney alifanikiwa kufunga mkwaju huo wa penalti kabla Danny Welbeck kuipatia Manchester United bao la pili.
Villa iliimarika kidogo baada ya kipindi cha pili lakini walikuwa Rooney na Nani walioandika mabao mengine mawili yaliyohitimisha karamu ya mabao 4-0.
Manchester United walionekana kikosi bora zaidi katika kipindi cha kwanza na ushindi huo umepunguza pia deni la mabao ya kufunga na Manchester City na sasa kuwa manne.
Lakini bado swali litaendelea kubakia kwa wapenzi wa kandanda juu ya Young anavyojiangusha na aliposhutumiwa alipofanya hivyo dhidi ya QPR, ambapo Shaun Derry aliadhibiwa kwa kumsukuma mshambuliaji huyo wa pembeni na alioneshwa kadi nyekundu.
Rufaa iliyokatwa na Rangers ilitupiliwa mbali na Chama cha Kandanda cha England na shutuma zitaendelea kumuandama Young kutokana na alivyofanya kwa mara nyingine.
Na kubwa zaidi Young alifanya hivyo kwa timu aliyowahi kuichezea na itaongeza zaidi chumvi kwenye jeraha kwa timu ya Aston Villa.
Villa walishindwa kuivunja rekodi dhidi yao wanapopambana na Manchester United, ambapo wamewahi kushinda mara moja tu katika mechi 31.
Jambo muhimu ni kwamba wapo pointi sita juu ya msatari wa kuteremka daraja na sasa wanajiandaa kwa pambano dhidi ya Sunderland, Bolton na West Brom ambapo lazima watafute pointi kujihakikishia hawateremki daraja.

No comments:

Post a Comment