Wanaharakati wanaojaribu kwenda Palestina wamezuwiliwa kupanda ndege katika nchi kadha za Ulaya, baada ya Israil kuyaonya mashirika ya ndege kwamba hawatawaruhusu abiria wao kuingia nchini.
Watu kama 1,500 wanatarajiwa katika uwanja wa ndege wa Ben Gurion, Tel Aviv, wakielekea Ufukwe wa Magharibi, kwenda kuonesha upinzani wao dhidi ya ujenzi wa makaazi ya Waisraili katika eneo hilo.
Wanaharakati wanataka kuingia kwa wingi kuwaunga mkono Wapalestina wanaoishi Ufukwe wa Magharibi.
Wanasema wakiwapo huko wataonesha mshikamano na wale wanaopinga ujenzi zaidi wa makaazi ya wa-Israili kwenye ardhi ambayo ina utatanishi kuhusu nani anaimiliki.
Hii ni mara ya tatu kwa wanaharakati wanaowaunga mkono WaPalestina kujaribu kufanya ile wanayoiita kampeni ya "karibuni Palestina".
Kujibu hayo, Israil imeweka polisi zaidi katika uwanja wa ndege wa Ben Gurion, mjini Tel Aviv.
Piya inaonesha imeyaonya mashirika ya ndege kwamba yatabidi yabebe gharama ya kuwarejesha nyumbani wanaharakati wataokataliwa kuingia Israil.
Mashirika ya ndege nayo yameamua kutowaruhusu wanaharakati kupanda ndege.
Mashirika mengine ya ndege yamevunja kabisa safari za kwenda Tel Aviv.
No comments:
Post a Comment