TANGAZO


Saturday, April 14, 2012

Dk. Shein azindua Baraza, Kamati za Uhakika wa Chakula, Taifa, Wilaya na Shehia, mjini Zanzibar

Baadhi ya wajumbe wa Kamati mbalimbali, wakiwa katika mkutano wa uzinduzi wa Baraza na Kamati za Uhakika wa chakula na Lishe katika ngazi ya Taifa, ukumbi wa Salama Bwawani Hotel, mjini Zanzibar leo. Uzinduzi huo ulifanywa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein. (Picha na Ramadhan Othman, Ikulu)


Baadhi ya wajumbe wa Kamati mbalimbali wakimsikiliza Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein, alipokuwa akizungumza na wajumbe hao katika uzinduzi wa Baraza na kamati za Uhakika wa chakula na Lishe, ngazi ya Taifa, ukumbi wa Salama, Bwawani Hotel, mjini Zanzibar.


Baadhi ya wajumbe wa Kamati mbalimbali, wakifuatilia hotuba ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein, alipokuwa akizungumza nao katika uzinduzi wa Baraza na kamati za Uhakika wa chakula na Lishe, ngazi ya Taifa, Bwawani Hotel, mjini Zanzibar.


Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein, akizungumza na vingozi mbalimbali, wakatiwa uzinduzi wa Baraza na Kamati za Uhakika wa Chakula na Lishe, ukumbi wa Salama, Bwawani Hotel, mjini Zanzibar leo. Kulia ni
Mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Chakula na Kilimo nchini, Dianna Allen Tempelman na kushoto ni Makamo wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi.



Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein, akizungumza katika uzinduzi huo. Kulia ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo na Maliasili Othman Affani Maalim na Mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Chakula na Kilimo
nchini, Dianna Allen Tempelman. 


 Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein, akimkabidhi kitabu cha utambulisho cha Sheria na Sera ya Uhakika wa Chakula na Lishe, Makamo wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Baraza la Uhakika wa Chakula na Lishe, ikiwa kama ishara ya uzinduzi wa Baraza la Kamati
za uhakika wa Chakula na Lishe ngazi ya Taifa, Wilaya na Shehia, ukumbi wa Salama Bwawani Hotel, mjini Zanzibar leo. 


Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein, akimkabidhi nakala ya kitabu cha utambulisho cha Sheria na Sera ya Uhakika wa Chakula na Lishe, Mwakilishi wa Shehia ya Jambiani, Kikadini na Kizimkazi, Suleiman Ali Hassan kwa Upande wa Unguja wakati wa uzinduzi huo.



Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein, akimkabidhi nakala ya kitabu cha utambulisho cha Sheria na Sera ya Uhakika wa Chakula na Lishe, Mwakilishi wa Shehia ya Pujini na Mbuzini Pemba, Fatma Bakari Hamadi, wakati wa uzinduzi wa Baraza la Kamati za uhakika wa Chakula na Lishe katika ngazi ya Taifa, Wilaya na
Shehia, ukumbi wa Salama, Bwawani Hotel, mjini Zanzibar leo. 


Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein, (katikati mbele), akiwa katika picha ya pamoja na Wajumbe wa Baraza la Uhakika wa Chakula na Lishe, baada ya kulizindua rasmi Baraza hilo, ukumbi wa Salama, Bwawani Hotel, mjini Zanzibar leo.






Dk. Shein azindua Baraza, Kamati za Uhakika wa Chakula




Na Rajab Mkasaba,
Ikulu Zanzibar


TATIZO kubwa linalopelekea uwezo wa wananchi kushindwa kukimu mahitaji yao ya kila siku ni kuwa sehemu kubwa ya kipato chao kinakwenda katika ununuzi wa chakula kutokana na ongezeko la bei kupanda mara kwa mara.

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk. Ali Mohamed Shein, aliyasema hayo leo katika uzinduzi wa Baraza na Kamati za Uhakika wa Chakula na Lishe katika ngazi ya Taifa, Wilaya na Shehia, hafla iliyofanyika huko katika ukumbi wa Salama katika Hoteli ya Bwawani, mjini Zanzibar

Viongozi mbali mbali walihudhuria wakiwemo Mawaziri, Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi, Makatibu Wakuu, Wakurugenzi na viongozi wa Kamati hizo.

Katika hotuba yake Dk. Shein alieleza kuwa ongezeko hilo linachangiwa kwa kiasi kikubwa na ukosefu wa upatikanaji wa chakula hicho.

Alisema kuwa pamoja na matatizo mbali mbali yanayosababisha kupanda kwa bei ya chakula duniani ikiwemo gharama za usafirishaji, mizozoz katika nchi mbali mbali na sababu nyenginezo.

Kutokana na hali hiyo, Dk. Shein alisisitiza kuwa si sahihi kwa baadhi ya wananchi kuona kuwa Zanzibar pekee ndio bei za bidhaa zimekuwa zikipanda mara kwa mara bali tatizo hilo ni la dunia nzima.

Alieleza kuwa  katika muda huu ambapo demokrasia inazidi kuenea wananchi mijini na vijijini kila kukicha wanahitaji kufanya mambo mengi zaidi katika kujiletea maendeleo yao. “Masuala haya yote yanajumuishwa kwenye kasha moja, maarufu kwa jina la uhakika wa chakula na lishe’,alisema Dk. Shein.

Aidha, Dk. Shein alisema kuwa hizo ni changamoto ambazo viongozi katika taasisi na sekta mbali mbali wana wajibu wa kushirikiana na wananchi pamoja na wataalamu mbali mbali katika kuzitafutia ufumbuzi wa kudumu na kueleza kuwa uzinduzi huo ni hatua muhimu katika kuzishajiisha taasisi kusimamia na kutoa muongozo juu ya utekelezaji wa masuala ya uhakika wa chakula na lishe.

“Lengo ni kuhakikisha kuwa nchi yetu inajihakikishia usalama wa chakula na lishe na inauwezo wa kukabiliana na hali tete ya upungufu wa chakula na janga la njaa kupitia utekelezaji thabiti wa kisera na kisheria.

Pamoja na hayo Dk. Shein alieleza kuwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imejidhatiti katika kuitekeleza Sera hiyo inayoufanya umasikini kuwa agenda muhimu ya maendeleo.

Alisema kuwa Serikali inashughulikia masuala ya uhakika wa chakula na lishe kwa upana wake kwa kuzingatia fungamano la uhakika wa chakula na lishe na juhudi za kupunguza umasiki na kuharakisha maendeleo kama ilivyofafanuliwa katika MKUZA.

Kupitia Sera ya Uhakika wa Chakula na Lishe, Dk. Shein alisema kuwa Serikali itaendeleza juhudi zake katika kuhakikisha wananchi wanashirikishwa katika kuwafikishia huduma muhimu na za msingi ikiwa ni pamoja na kuwapatia haki ya kumiliki ardhi, kuwawezesha kuanzisha biashara ndogo ndogo, maji safi na salama, kuunga mkono miradi inayotegemea nguvu kazi na kuwapatia mikopo midogo midogo.

Dk. Shein alieleza kuwa haki ya chakula ilipitishwa na Umoja wa Mataifa mwaka 1989 na kuridhiwa na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mwaka 2002 ikiwa ni miongoni mwa nchi zinazotambua haki hiyo.

Alisema kimsingi haki ya chakula inasisitiza kwaamba chakula ni haki ya kila binaadamu hivyo basi makundi yaliyo kwenye hatari ya kupatwa na ukame au ukosefu wa chakula yanahitaji kipaumbele katika kuhakikisha kuwa wana uhakika wa chakula na lishe.

Sambamba na hayo, Dk. Shein alieleza kuwa katika kutekeleza agizo la Umoja wa Mataifa, Baraza la Wawakilishi limetunga Sheria ya Uhakika wa Chakula na Lishe namba 5 ya mwaka 2011, Sheria ambayo ameitia saini tarehe 6 Julai mwaka jana.

Akitoa neno la shukurani Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Idd ambaye pia, ndiye Mwenyekiti wa Baraza la Taifa la Uhakika wa Chakula na Lishe alisema kuwa kuna kila sababu ya kutekeleza majukumu kwa ufanisi mkubwa zadi kwa kuzingatia kuwa chakula na lishe ni lazima viende pamoja.

Mapema Waziri wa Kilimo na Maliasili Mhe. Suleiman Othman Nyanga alieleza kuwa  kila Mzanzibari ana haki ya kupata chakula na lishe ikwia ni haki ya kuishi maisha salama na yenye afya njema.

Pia, Waziri Nyanga alisisitiza mashirikiano ndani ya Kamati hizo ili ziweze kutekeleza kwa ufanisi majukumu yao.

Nae Mwakilishi Mkaazi wa  Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Chakula Duniani Tanzania Bi Dianna Allen Tempelman, alieleza kuwa Shirika hilo litaendelea kuuunga mkono juhudi hizo za Zanzibar na kueleza kuwa hatua hiyo ni ukombozi katika suala zima la chakula na lishe nchini.

No comments:

Post a Comment