Waziri wa Miundombinu na Mawasiliano, Hamad Masoud |
Na Faki Mjaka-Maelezo
Zanzibar, SERIKALI ya Mapinduzi
Zanzibar imesema kuwa taarifa zilizozagaa Zanzibar
za kuibuka na kuonekana kwa Meli ya Mv.Spice Islander 1 iliyozama Septemba
Mwaka jana katika mkondo wa Nungwi Mkoa wa Kaskazini Unguja siyo za kweli.
Waziri wa Miundombinu na
Mawasiliano Zanzibar Hamad Masoud Hamad ameyasema hayo hivi leo katika Ukumbi
wa Baraza la Wawakilishi la Zamani Kikwajuni Zanzibar wakati alipokuwa
akizungumza na Waandishi wa habari kuhusiana na utendaji kazi wa Wizara yake.
Amesema kuwa ni kweli kuna
Meli imeonekana katika mkondo huo lakini siyo meli ya Mv.Spice Isalnders 1 bali
ni meli ya uvuvi ya Komoro ambayo ilizama siku nyingi yenye namba za usajili
2NCT 4/2905.
Akielezea kuhusu Meli hiyo na
kuzagaa kwa taarifa amesema taarifa zilikuja toka jana jioni ya saa 12.30
kutoka kwa wavuvi wa Nungwi ambao waliiyona Meli hiyo ambapo Wizara chini ya
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Bahari Zanzibar Abdallah Kombo walitafuta
uhakika wa jambo hilo.
Kwa mujibu wa Kaimu Mkurugenzi
huyo amesema walifanya mawasiliano na kutuma kikosi kazi ambacho kilibaini kuwa
Meli hiyo ya kivuvi ilizama Februari 3 na kuibuka katika Mkondo wa Bahari ya
Hindi Machi 20 kabla ya kuonekana tena siku ya jana katika maeneo ya Mkondo wa
Nungwi.
Aidha Kombo amesema
wameshafanya mawasiliano na vyombo mbalimbali vya bahari kwa lengo la kuwapa
taarifa kuhusu meli hiyo ambayo inaendelea kuzagaa katika bahari.
Kwa upande mwengine Waziri
huyo wa Miundo mbinu amesema jumla ya Tshs 900 Milioni zimetumika kwa ajili ya
kuwalipa fidia wananchi ambao nyumba zao zimepakana na Uwanja wa ndege wa
Kimataifa wa Amani Abeid Karume Zanzibar na kwamba ambao bado hawajalipwa fedha
zao utaratibu unaendelea kwa awamu.
Amesema ni jukumu la Serikali
kuhakikisha inawalipa fidia wale wote ambao nyumba zao zinatakiwa kubomolewa
ili kupitisha ujenzi wa Uwanja huo ambapo kiasi cha Milioni 500 za fidia
zimetengwa kwa ajili ya kukamilisha awamu
nyengine ya malipo ya wale ambao nyumba zao zitaathirika na zoezi hilo.
Akizungumzia kuhusu suala la
kusimamishwa kwa Mkandarasi ambaye amepewa jukumu la kujenga Uwanja huo amesema
jambo hilo si kweli bali ujenzi huo unaendelea
kwa awamu ambapo viongozi wa Wizara hiyo wakiongozwa na Naibu waziri wake wako
nchini China
kuendelea kujadiliana na Mkandarasi huyo jinsi ya kuendeleza ujenzi huo.
Waziri huyo amesema wizara
yake imejipanga vyema kuhakikisha kuwa wanatimiza maelngo waliyojiekea chini ya
Idara za Wizara hiyo ambapo amewaomba wananchi na wadau mbalimbali kuonesha
ushirikiano katika kutimiza malengo ya Wizara.
Waziri Hamad Masoud amefanya
mkutano huo na waandishi wa habari ikiwa ni mwendelezo wa kutekeleza agizo
lililotolewa na Rais wa Zanzibar
na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohammed Shein kwamba kila
kiongozi ana wajibu wa kuhakikisha anawafikishia taarifa wananchi juu ya
utendaji kazi wa Ofisi yake.
No comments:
Post a Comment