Mkurugenzi Mtendaji wa Cargostars ni Dioniz Malinzi, | |
Na Said Mwishehe
KAMPUNI ya Cargostars Ltd ya Tanzania imepewa tuzo ya Teknolojia, Ubora na Ugunduzi kutoka taasisi ya Kimataifa ya Organiser - Otherways Management Association and Consultant (OMAC).
Akizungunza Dar es Salaam jana, Meneja Masoko wa Cargostars, Viola Lema alisema tukio la kupewa tuzo hiyo lilifanyika Machi 26 mwaka huu katika mji wa Berlin, Ujerumani.
Alisema tuzo hiyo ni heshima kubwa kwa kampuni yao ambayo imekuwa kifanya kazi zake kitaifa na kimataifa, lakini akatumia nafasi hiyo kuahidi kutoa huduma bora kama ambavyo wamekuwa wakifanya kwa muda mrefu ili kuhakikisha huduma wanazotoa zinaendelea kuwa bora siku hadi siku."Tunatoa huduma zetu katika nchi mbalimbali duniani, mbali ya Tanzania, hivyo kupata tuzo hii ya kimataifa ni heshima kubwa kwa Kampuni ya Cargostars, lakini pia kwa Tanzania maana ni kampuni yetu tu ndiyo iliyofanikiwa kupewa tuzo hiyo.
"Kwetu Cargostars ni changamoto kubwa, tunatambua wajibu wetu katika kutoa huduma zilizo bora kwa wateja wetu kutoka sehemu mbalimbali, hivyo tunaahidi kuendelea kufanya kila linalowezekana kuendelea kufanya kazi katika kiwango chenye ubora zaidi ili tupate heshima kubwa kama hiyo ya tuzo ambayo tumepewa," alisema Lema.
Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Cargostars ni Dioniz Malinzi, na Lema amefafanua zaidi jumla ya nchi 41 duniani zilishiriki katika tukio hilo la utoaji tuzo.
Alifafanua zaidi kuwa tuzo hiyo ya kimataifa walikabidhiwa na Rais wa taasisi hiyo ya Otherways Management Association and Consultant, Charles Tabeti na kufafanua kuwa makao makuu ya taasisi hiyo yapo nchini Ufaransa, lakini tukio la utoaji wa tuzo lilifanyika Ujerumani.
Akizungumzia kampuni hiyo ya Cargostars Meneja wa Rasilimali Watu, Lulu Komanya alisema kampuni yao siku zote imekuwa ikihakikisha kuwa wanatekeleza majukumu yao kwa kutumia teknolojia ya kisasa, ugunduzi na ubora na tuzo waliyoipata inastahili na ni heshima kwa kampuni na taifa kwa ujumla.
Pia alisema kutokana na ubora wa kazi zinazofanywa na kampuni yao, tuzo waliyoipata ni ya tisa kwani kuanzia mwaka 2003 hadi mwaka 2011 jumla ya tuzo tisa wamepewa kutoka taasisi mbalimbali zinazotambua mchango wao wa kutoa huduma.
No comments:
Post a Comment