Marehemu Salum Mtondoo |
Na Halima Mohammed, Zanzibar
MWAKILISHI wa jimbo la Bububu wilaya ya Magharibi Unguja Salum Amour Mtondoo (49) amefariki dunia baada ya kusumbuliwa na maradhi ya moyo.
Mtondoo ambae alichaguliwa kushika wadhifa huo katika uchaguzi mkuu wa 2010 kupitia chama Cha Mapinduzi (CCM) alifariki dunia jana katika Hospitali ya Rufaa ya Mnazimmoja.
\Taarifa Kwa vyombo vya habari iliyotolewa na Baraza la Wawakilishi Zanzibar imesema kuwa kifo hicho na kuwataka wananchi wa Zanzibar kuwa na subra katika kipindi hichi kigumu cha msiba.
“Tumepokea kwa mshtuko msiba huu lakini tunawaomba wananchi wa Jimbo la Bububu na wazanzibari wote kuwa wastahamilivu pamoja na familia ya marehemu”, alisema Spika wa Baraza la Wawakilishi Pandu Ameir Kificho.
“Tunamuomba Mwenyezimungu aijaalie familia ya Marehemu pamoja na wananchi wa Jimbo la Bububu, subira na utulivu katika kipindi hiki kigumu cha msiba” aliongeza Kificho.
Nae Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Bw. Vuai Ali Vuai alisema kuwa msiba huo sio wa CCM pekee bali ni wa taifa zima.
“Tumepokea kifo hichi kwa mshtuko mkubwa lakini tuelewe kwamba hii ni kazi ya mungu haina makosa tunachotakiwa tuwe na subra”, alisema.
Marehemu alizaliwa tarehe 14/ 12/ 1962 huko Bububu , Wilaya ya Magharibi , Unguja na kupata elimu yake ya msingi na Sekondari katika Shule ya Bububu kuanzia mwaka 1969 hadi 1979 .
Marehemu Mtondoo katika uhai wake aliwahi kufanyakazi ya Usimamizi wa Kiwanda cha COTEX mnano mwaka 1983 hadi mwaka 1985 na Baadae kufanyakazi za Ujenzi katika ushirika wa BBB 1986 hadi mwaka 1992.
Mbali ya kazi hizo , Marehemu aliwahi kufanyakazi za biashara kuazia mwaka 1992 hadi mwaka 2010.
Katika shughuli za kisiasa, marehemu amewahi kushika nyadhifa mbali mbali katika Chama cha Mapinduzi ikiwemo mjumbe wa Kamati ya siasa ya Tawi na nafasi za ujumbe katika jumuiya ya wazazi Wilaya hadi Mkoa.
Marehemu ameacha vizuka na watoto 10 na anatarajiwa kuzikwa leo.
Mwenyezimungu aiweke roho ya Marehemu mahali pema peponi. Amin.
No comments:
Post a Comment