Manchester United imezidi kujichimbia kileleni mwa Ligi Kuu ya England na kuongeza wigo wa pointi nne dhidi ya Manchester City, baada ya kuilaza Wolves mabao 5-0.
Jonny Evans alikuwa wa kwanza kuipatia bao Manchester United, kabla mlinzi wa Wolves Ronald Zubar hajatolewa nje kwa kadi nyekundu baada ya kuoneshwa kadi ya pili ya manjano.
Hali hiyo ilikuwa ni afueni kwa wageni ambapo Antonio Valencia alifunga bao la pili kabla ya Danny Welbeck kutumbukiza wavuni bao la tatu.
Javier Hernandez baadae alipachika bao la nne kwa kuunganisha vyema mpira wa pembeni uliopigwa na Valencia na muda mfupi baadae Steven Fletcher nusura aipatie Wolves bao la kufutia machozi. Alikuwa Hernandez tena aliyeifungia Manchester United bao la tano.
Wolves sasa wameshinda mchezo mmoja tu kati ya michezo 14 iliyopita ya ligi na wanamuweka meneja wao wa muda Terry Connor katika wakati mgumu wakiwa mkiani mwa msimamo wa Ligi.
Hii ni mechi ya tatu Wolves kupoteza wakiwa chini ya Connor katika mechi nne alizosimamia na wameshafungwa mabao 12 katika mechi tatu na wao bila kutumbukiza mpira wavuni.
Kwa kikosi cha Sir Alex Ferguson ushindi huo umewaongezea hazina ya mabao na kupunguza wigo wa mabao dhidi ya Manchester City na sasa kuwa mabao matatu tu.
No comments:
Post a Comment