TANGAZO


Monday, March 12, 2012

Maalim Seif anena, 'Changamoto chachu ya maendeleo'

Makamu wa Kwanza wa Serikali ya Zanzibar, Maalim Seif Shariff Hamad




Na Khadija Khamis-Maelezo Zanzibar.
        
 Makamu wa Kwanza wa Rais Maalim Seif Sharif Hamad amesema  changamoto zinazotokea katika utendaji kazi katika Taasisi mbali mbali  ni chachu  katika kuleta maendeleo  na kujikwamua pale tulipofika.
 Amesema bila ya kuwa na changamoto  maendeleo yataendelea kusuasua  kwani kutakuwa hakuna  hatua itakayopigwa mbele katika kuleta mafanikio.
 Maalim Seif aliyaeleza hayo leo wakati akizungumza na uongozi wa Vyombo vya Habari vya Serikali ikiwemo Idara ya Habari Maelezo,Shirika la Utangazaji Zanzibar ZBC na Gazeti la Zanzibar ikiwa ni mfululizo wa kutembelea Idara za Wizara ya Habari Utamaduni Utalii na Michezo.
 Amesema vyombo vya habari ndio kiungo kikubwa  kati ya wananchi na Serikali hivyo ni vyema  kufanya kazi kwa uadilifu na kuweza kukabiliana na vikwazo ambavyo vinaweza kurudisha nyuma  juhudi mbali mbali zinazochukuliwa na wananchi na hata Serikali.
 Akizungumzia juu ya mafunzo kwa wanahabari, Maalim Seif alizitaka taasisi hizo kuwa na mpango mzuri wa kuwapeleka waandishi wa habari masomoni na katika mafunzo mengine ili waweze kukabiliana na kasi ya maendeleo ya teknolojia ambayo kwa sasa inakwenda kwa kasi kubwa.
 Amesema masomo humjengea uwezo mwana habari wa kuweza kutumia kifaa chochote  na  kuweza kuibua  mambo kadha  ikiwemo uwezo wa kumkabili mtu yeyote bila ya woga au wasi wasi.
 Amewataka waandishi wa habari katika Idara hiyo kuendelea kuwa wabunifu katika uandishi na kuandika habari zilizofanyiwa utafiti wa kina bila ya woga wowote
 Maalim Seif alisisitiza haja ya kuwa na vifaa vya kisasa vinavyokwenda na wakati ili kuweza kufanya kazi kwa ufanisi , haraka na kwa wepesi zaidi.
 Mapema Makamu wa Kwanza wa Rais aliipongeza Idara ya Habari kwa  utendaji wake  hasa kwa vile inatoa huduma ndani na nje ya nchi na kuishauri kuanza kupeleka taarifa zake katika  vituo vyengine  vya kigeni kama BBC,AFP  CNN  na REUTERS ili kuweza kutumia  taarifa hizo na kuitangaza Zanzibar.
 Akizungumzia suala la mishahara alisema kuwa viwango vya mshahara kwa wafanyakazi wa Vyombo vya habari ni vidogo  kulingana na hali halisi na kupendekeza viwango hivyo kubadilishwa kulingana na wakati uliopo.
 “Binadamu ni binadamu anaangalia maslahi yake tukisema uzalendo tu wengi watashindwa”alisema Maalim Seif
 Katika Ziara hiyo Maalim Seif alitembelea Idara ya Habari Maelezo,Shirika la Magazeti ya Serikali,Shirika la Utangazaji la Zanzibar ZBC pamoja na maeneo ya Mitambo ya kurushia matangazo ya Shirika hilo.   

No comments:

Post a Comment