TANGAZO


Thursday, March 15, 2012

Balozi mpya wa China nchini ataja vipaumbele vyake

Balozi mpya wa China nchini, Bw. Lu Youqing

Na Aron Msigwa – MAELEZO.
15/3/2011, Dar es salaam.
Balozi mpya wa China nchini Tanzania Bw. Lu Youqing  amesema  atahakikisha kuwa anatumia muda wa uongozi wake kuwatumikia wananchi wa China na Tanzania na kuhakikisha kuwa  ushirikiano uliopo kati ya nchi hizi katika nyanja  za kiuchumi, kisiasa, kiutamaduni na kijamii unadumishwa.
 Akizungumza na waandishi wa habari katika ofisi za ubalozi huo leo jijini Dar es salaam amesema  Tanzania ni miongoni mwa  nchi za bara la Afrika ambazo uchumi  wake unakua kwa kasi kufuatia maendeleo na  mabadiliko ya sayansi na teknolojia yanatokea duniani.
Amesema China ikiwa ni nchi ya pili duniani kwa maendeleo itaendelea  kushirikiana na mataifa mbalimbali katika bara la Afrika kuimarisha na kutetea amani, umoja, kushiriki katika utatuzi wa migogoro mbalimbali inayotokea katika  nchi za Afrika na kusaidia nchi marafiki katika mipango ya maendeleo.
“Hivi sasa uchumi wetu unakua kwa kasi sana na kufikia pato la taifa la dola za kimarekani trilioni 7.5 kwa mwaka sawa na asilimia 9.2 maendeleo haya ni makubwa ” amesema.
Amefafanua kuwa maendeleo yaliyopo nchini China kwa kiasi kikubwa yamechangiwa na mfumo  na sera nzuri za uchumi zilizopo pamoja na  mabadiliko ya wananchi kifikra na kitabia na kuongeza kuwa kuna juhudi mbalimbali zilizofanywa katika kuinua uchumi wa China zikiwemo utoaji wa huduma bora kwa wananchi, uzingatiaji wa masuala ya ajira, matumizi ya sayansi na teknolojia na utoaji wa elimu bora kwa wananchi.  
Katika kuhakikisha kuwa ushirikiano baina ya China na Tanzania unaendelezwa katika nyanja mbalimbali balozi Lu amesema katika kipindi cha uongozi wake nchi yake itaendelea kuchangia kutoa nafasi za ajira kupitia makampuni mbalimbali ya kichina na miradi mbalimbali  inayoanzishwa nchini  Tanzania katika sekta ya kilimo, mawasiliano, utengenezaji wa miundombinu mbalimbali zikiwemo barabara, madaraja na ujenzi wa mitandao ya mawasiliano.
“Kihistoria tuna ushirikiano mkubwa sana  baina ya Tanzania na China katika  miradi mbalimbali inayoanzishwa pamoja na miradi ya ushirikiano ya reli ya Tazara na kiwanda cha Urafiki “ amesema Balozi  Lu.
Ameongeza kuwa nchi yake itaendelea kushirikiana na Tanzania katika nyanja ya  elimu katika utoaji wa ufadhili na nafasi za masomo kwa watanzania kwenda nchini humo kujifunza masuala mbalimbali  na kuongeza kuwa  nchi yake itaendelea kutoa fursa kwa wasanii mbalimbali waliopo nchini kwenda  China kujifunza masuala mbalimbali ili kuboresha kazi zao na tasnia ya sanaa kwa ujumla.

No comments:

Post a Comment