Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Tabora –Uyui Said Ntahondi
Na Tiganya Vincent , RS-Tabora
7 March 2018
WANACHAMA wa Mfuko wa Afya ya Jamii(CHF) na wasio wanachama wametakiwa kupiga simu kwa Mganga Mkuu wa Wilaya ya Uyui au Diwani wa Kata zao pindi wanapokwenda kutibiwa katika Zahanati na kuambiwa hakuna dawa ili wahusika wachukuliwe hatua.
Kauli hiyo imetolewa jana na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Tabora –Uyui Said Ntahondi wakati akifunga kikao maalumu cha kupitisha a mapendekezo ya marekebisho ya bajeti ya ruzuku ya miradi ya maendeleo ya miundombinu (LGCDG) ya bilioni 1.3 kwa ajili ya mwaka huu wa fedha (2017/18).
Alisema vitendo vya wananchama kwenda kupata matibabu katika Zahanati na kuambiwa kuwa dawa hazipo vimekuwa vikikatisha tamaa wananchi wengine kujiunga na Mfuko huo.
Ntahondi alimwagiza Mganga Mkuu wa Wilaya hiyo na Madiwani kubandika namba za simu zao za mkononi kwenye Zahanati zilizopo katika Kata zao ili wananchi wanapokutana na tatizo hilo na mengine waweze kuwasiliana nao kwa ajili ya kupatiwa ufumbuzi.
Mwenyekiti huyo alisema kuwa mgonjwa hatakiwi kuondoka katika eneo la Zahanati bila Dawa na ikitokea Mwanachama wa CHF akanunua dawa kwa gharama zake kwa sababu ya kuambiwa dawa hakuna basi bili yake italipwa na Zahanati husika kwa kumrejeshea fedha zake.
Ntahondi aliongeza kuwa ni vema kila Zahanati katika Halmashauri hiyo ibandike Mwongozo wa Dawa zote zinazopatikana pale ili mgonjwa ajue orodha ya dawa zilizopo.
Wakati huo huo Mwenyekiti huyo amewataka Madiwani kuhakikisha wanafuatilia taarifa za matumizi ya fedha za miradi mbalimbali ya jamii ili iwe inasomwa na viongozi wa eneo husika kwa wananchi ili wajiridhishe kama utekelezaji wa miradi unalingana na thamani ya fedha iliyotolewa.
Alisema kuwa hatua hiyo itasaidia kuondoa ubadhirifu unaofanywa na baadhi ya viongozi na watendaji wa fedha za sekta mbalimbali ikiwemo afya , elimu na maji.
Ntahondi alisema kuwa ikibainika kuna mapungufu Wahusika watachukuliwa hatua ikiwemo kufukuzwa kazi.kwa Baraza la Madiwani haliwezi kukubali kuona fedha nyingi zinatolewa na Serikali kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali lakini miradi inayotekezwa inakuwa chini ya viwango na hamsaidi mwananchi kama ilivyokusudiwa.
Aliwataadhalisha watendaji ambao wanatarajia kushiriki katika utekelezaji wa miradi mbalimbali baada ya kupata fedha kutoka Serikali kutumia fedha hizo kwa uaminifu na uadilifu ili wasije wakaishia kufukuzwa kazi na kupelekwa Mahakamani.
Ntahodi alisema kuwa hivi mtumishi au Mtendaji yoyote akibainika kutenda kosa la kula fedha za umma , jambo la kwanza watakalofanya ni kumfukuza kazi na kumpeleka Mahakamani na sio kudai alipe.

No comments:
Post a Comment