KESHO Tarehe 8 Machi, 2018 ni maadhimisho ya siku ya wanawake duniani (Women's Day) JUKECUF inaungana na Wanawake wote duniani katika siku hii adhimu kuhamasisha Haki, Usawa, Uadilifu na fursa sawa za kuchangia Maendeleo ya mwanadamu na mazingira yake duniani kote.
Moja ya Dhumuni kubwa la kuazimishwa kwa Siku hii duniani ni kupinga aina yoyote ya uonevu, unyanyasaji, ubaguzi na unyanyapaa wa aina zote dhidi ya Mwanamke.
JUKECUF inaungana na wanawake wa Kitanzania wote wapenda Haki na maendeleo ya Taifa lao kukataa aina yeyote ile ya uonevu unyanyasaji unaofanywa na Utawala usiozingatia misingi ya Sheria na Katiba ya nchi yetu na au unyanyasaji wa Mwanamke unaofanya na mtu mmoja mmoja mahala anapoishi.
Serikali isiyozingatia utawala wa haki na sheria na kusababisha umwagaji wa Damu, utekaji, ushambuliaji na kuumizwa vibaya kwa raia unasababisha Wanawake kuwa Wahamga wakubwa wa matukio hayo tukitaja mfano mmoja wa kupotea kwa Mwandishi wa Habari wa MCL Ndugu Azory Gwanda. Hakika anayeteseka ni Mkewe na Watoto.
JUKECUF inaitaka Serikali ya Awamu ya Tano kuchukua hatua za haraka na za makusudi kuirejesha nchi yetu katika hali ya Amani na Usalama wa Raia na mali zao kwa kuanzisha Mjadala mpana wa Kitaifa na wadau wote muhimu nchini ikiwa ni pamoja na Maridhiano ya Kisiasa yatakayotoa Fursa kwa wadau wote kufanya siasa za Kistaarabu na kuepusha maafa.
JUKECUF pia inavitaka Vyombo vya Ulinzi na Usalama kufanya kazi kwa weledi, kwa mujibu wa Sheria na kuepuka mihemko ya kisiasa na kutumiwa vibaya na wanasiasa.
JUKECUF tunaitaka Serikali ya Rais Magufuli kuchukua hatua za makusudi kutekeleza sasa kwa vitendo Mikataba yote ya Kimataifa, Itifaki na Matamko ya Kimataifa yanayopinga aina zote za unyanyasaji wa Wanawake, ambayo Serikali yetu imeridhia kwa kusaini. (CEDAW na DECLARATION FOR HUMAN RIGHTS- 1948)
JUKECUF inaitaka Serikali ya Rais Magufuli kuheshimu kwa vitendo Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania iliyopo kwa ujumla wake na kuheshimu Haki za Binadamu. Tunaitaka Serikali kuimarisha Uchumi wa nchi kwa kuweka mazingira maridhawa ya mfumo wa Biashara, ukusanyaji wa kodi, na kuimarisha mifuko ya Wanawake katika kujikwamua Kiuchumi.
JUKECUF inatoa wito kwa Rais John Magufuli kurejesha mchakato wa kupatikana lwa Katiba Mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa madhumuni ya kuepusha nchi yetu na Maafa makubwa yanayoweza kutokea siku za usoni endapo hakutakuwa na mipaka ya uwajibikaji wa Mihimili ya Dola na kuwa na Tume Huru za Uchaguzi kwa pande zote za Muungano.
JUKECUF tunaitaka Wizara ya Jinsia, Wanawake, Wazee na Watoto kuenenda kulingana na jina la Wizara, tunataka kuona Wizara ikisimama kwa miguu yake kumtetea Mwanamke, kumtetea msichana ikiwemo kuhakikisha hakuna vikwazo vyovyote vitavyompelekea Mtoto wa kike kushindwa kufikia malengo ya kupata ELIMU.
JUKECUF inaungana na Wanademokrasia na Wanaharakati kupitia Wakili Fatma Karume na wenzike kufungua Mashauri ya Kikatiba Mahakama Kuu kwa madhumuni ya kuimarisha na kuirejesha nchi yetu katika misingi ya demokrasia ya kweli na uwanja sawa wa ushindani kwa vyama vyote vya siasa na kulinda Haki za Wapiga Kura.
JUKECUF ipo tayari kushirikiana na wadau wote wenye nia njema ya kupigania haki za wanawake na haki za binadamu kwa ujumla katika nchi yetu. Tunawataka wanawake wote bila ya kujali itikadi za vyama kuungana pamoja katika siku hii adhiimu kupiga vita aina zote za manyanyaso, uonevu, dhuluma, ubaguzi na kupiga vita viashiria vyote vinavyoweza kuipeleka nchi yetu katika machafuko, kupotea kwa Amani na Usalama wa Raia na Mali zao.
HAKI SAWA KWA WOTE
Imetolewa Leo Tarehe 7 Machi, 2018 Na;
SEVERINA SILVANUS MWIJAGE
Makamo Mwenyekiti- JUKECUF-TAIFA
Makamo Mwenyekiti- JUKECUF-TAIFA
Mawasiliano: 0757245082 / 0712296880


No comments:
Post a Comment