Imetolewa leo Tarehe 6/2/2018
· JAJI MUTUNGI ASHIRIKIANA NA LIPUMBA KUVUNJA AMRI YA MAHAKAMA KUU NA KUENDELEZA WIZI WA FEDHA ZA RUZUKU YA CUF:
· LIPUMBA NA WASHIRIKA WAKE WAPANGA NJAMA ZA KUTAKA KUWAVUA UANACHAMA MADIWANI WA CUF-MKOA WA DAR ES SALAAM:
Kama mjuavyo CUF-Chama Cha Wananchi, bado kinapita katika changamoto kubwa za utekelezaji wa majukumu yake ya kikatiba, kisheria na kidemokrasia nchini kutokana na vitendo vinavyofanywa dhidi yake na Lipumba na washirika wake akiwemo Msajili wa Vyama vya Siasa nchini Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Francis Katabazi Mutungi, Jeshi la Polisi Tanzania na Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini(RITA).
Pamoja na hujuma hizo, CUF-Chama Cha Wananchi kimeendelea kuenzi tunu yetu ya Taifa ya amani na utulivu kwa kujiepusha na ulipizaji kisasi kwa kujichukulia sheria mkononi jambo ambalo ndilo lililokuwa lengo la wasaliti hao. CUF-Chama Cha Wananchi kiliamua kuwasilisha mahakamani hujuma zote zinazofanywa dhidi yake; ambazo kwa kiasi kikubwa zinahusika na uvunjaji wa sheria za nchi, ili haki iweze kutendeka kwa mujibu wa Katiba ya CUF-Chama cha Wananchi ya mwaka 1992 (Toleo la 2014) na sheria za Jamhuri ya muungano wa Tanzania.
1. BAADHI YA HUJUMA ZILIZOFANYWA NA LIPUMBA NA WASHIRIKA WAKE KUTAKA KUKIDHOOFISHA CHAMA CHA CUF:
Lipumba na washirika wake baada ya kuona wanachama na viongozi wa CUF TAASISI hawachokozeki na wamejiepusha kufanya fujo na hivyo kufifisha ndoto za mpango wao wa kumtumia Msajili wa vyama vya siasa Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Francis Katabazi Mutungi, kukifutia usajili CUF-Chama Cha Wananchi; waliamua kutafuta njia mbadala za kukidhoofisha Chama;
a) Njia ya kwanza ni kuwafukuza uanachama viongozi wa kiserikali; hasa wabunge na madiwani na hivyo kuiwezesha Tume ya Taifa ya Uchaguzi kuitisha uchaguzi mdogo ambapo CCM ilitegemea kujipatia ushindi na kuiacha CUF bila uwakilishi kwenye vyombo vya maamuzi. Aidha njia hiyo ingelishawishi baadhi ya viongozi hao wa serikali kwa tiketi ya CUF-Chama cha Wananchi na wanachama kuingiwa woga na hivyo kujisalimisha ili kumpatia uungwaji mkono msaliti Lipumba.
Baada ya kuwafukuza wabunge nane (8) na Madiwani wawili wa Viti Maalum kinyume cha Katiba ya CUF-Chama cha Wanachi ya mwaka 1992 (Toleo la 2014), mnamo mwezi Julai 2017, Wabunge hao wahanga na wengine kumi na tisa wa majimbo walifungua kesi Mahakama Kuu ya Tanzania kanda ya Dar es Salaam na kufanikiwa kupata AMRI YA ZUIO (Temporary Injunction Order) ambazo zilimfanya msaliti Lipumba na wenzake kukwama katika hujuma dhidi yao.
Kupitia mashauri ya madai Na.447/2017 na Na.21/2017 Mahakama Kuu imemzuia msaliti Lipumba na washirika wake kuwajadili au kufanya jambo lingine lolote dhidi ya Wabunge hao, na kwa wale nane wa Viti Maalumu ambao walivuliwa uanachama Tarehe 23 Julai, 2017. Mahakama imesitisha utekelezaji wa kufukuzwa kwao mpaka hapo kesi zao za msingi (Misc.Civil Cause No. 21/2017 na Misc.Civil Cause No. 143/2017) zitakaposikilizwa na kutolewa uamuzi. Hatua hiyo kimsingi ilimfunga mikono msaliti Lipumba katika kuendeleza hujuma dhidi ya CUF TAASISI kwa ujumla.
b) Njia ya pili ni kufanya matukio ya kihuni ya kuvamia vikao vya wanachama na hata mwanachama mmoja mmoja kwa lengo la kuwafanyia fujo, kuwapiga na kuwajeruhi kama vile uvamizi wa Mabibo (Vina Hotel) na Temeke. Aidha matukio ya utekaji wa viongozi na wanachama wa CUF umeendelea kufanywa kutokana na Jeshi la polisi kuendelea kuwalinda wahalifu wanaotokana na msaliti Lipumba bila kuwachukulia hatua stahiki na hili yamkini kutokana na maelekezo ya msajili wa vyama vya siasa kwa Jeshi hilo kupitia kwa IGP kwa mujibu wa barua Kumbu. Na. HA.322/362/14/88 ya tarehe 28 Septemba, 2016 aliyoandikiwa msaliti Lipumba kumfahamisha hivyo.
Barua hiyo ilinakiliwa kwa IGP. Tukio la hivi karibuni la jaribio la utekaji lilifanyika Tarehe 18 Januari, 2018 ambapo wafuasi wa msaliti Lipumba; miongoni mwao, Abdallah Machela, Shaibu Issa (maarufu kwa jina la Mrangi) na Jacob Nchimbi (dereva) na wenzao wengine wakiwa na gari T 866 BGW (NISSAN SAFARI) walijaribu kutaka kumteka Naibu Mkurugenzi wa Habari na Uenezi Mhe. Mbarala Maharagande katika eneo la Amana Hospitali, Ilala.
Tukio hilo lilitolewa taarifa kituo kidogo cha polisi Ilala na kupewa Na. ILA/RB/184/2018. Ikumbukwe kuwa huyu Shaibu Issa ndiye mshiriki mkuu wa matukio ya utekaji na uvamizi na mpaka sasa ameshiriki matukio zaidi ya manne na mashauri yanaendelea mahakamani.
2. MPANGO WA KUZIFUTA KESI ZILIZOPO MAHAKAMANI:
Baada ya kuona hatua zao zote zina dalili ya kupoteza mwelekeo, msaliti Lipumba na Msajili wa vyama vya siasa Jaji Francis Katabazi Mutungi, wakishirikiana na Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA) na ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) walifanya njama za kusajili wajumbe wapya wa Bodi ya Wadhamini ya CUF-Chama Cha Wananchi ili waweze kuzifuta kesi zote zilizofunguliwa Mahakama Kuu dhidi yao na hivyo kujinusuru na fedheha kubwa ya maamuzi ya Mahakama. Njama hizo zilihusisha kughushi nyaraka (kosa la jinai) za kumbukumbu za CUF-Chama cha Wananchi katika Masijala ya RITA.
Njama hizo ovu zilisababisha Mhe. Ally Saleh (MB) kufungua mashauri mawili (Misc. Civil Cause No.13/2017 na Misc. Civil Cause No. 51/2017) ambayo yamewezesha kutolewa amri ya zuio (Temporary Injunction Order) kwa wajumbe hao feki kujihusisha na jambo lolote la CUF-Chama cha Wananchi. Hatua hiyo ilimfanya msaliti Lipumba abanwe zaidi kwa sababu mmoja ya wajumbe wa Bodi yake feki ni Thomas Daudi Malima aliyekuwa mtia sahihi katika akaunti yao Na. 2072300456 ya NMB Tawi la Temeke.
Akaunti hiyo ilifungwa na Bodi halali ya CUF-Chama cha Wananchi Tarehe 30 Januari, 2017 na taarifa kupelekwa NMB Makao Makuu na kwa Meneja wa NMB Tawi la Temeke kupitia barua kumbukumbu Na.CUF/HQ/BRT/005/017/0 ya Tarehe 30/01/2017 lakini Meneja huyo amekaidi na anaendelea kuitumia kupitisha fedha zinazotolewa na msajili wa vyama vya siasa Jaji Francis Katabazi Mutungi kwa msaliti Lipumba na genge lake, licha ya amri ya Mahakama Kuu ya Tarehe 31 Machi, 2017 iliyozuia kufanya hivyo. Amri hiyo ilikabidhiwa kwa msajili wa vyama vya siasa Jaji Francis Katabazi Mutungi kupitia barua Kumb. Na. CUF/HQ/AKM/BD/017/001 ya Tarehe 3 April, 2017.
Aidha kwa mujibu wa kumbukumbu tulizonazo Meneja huyo wa NMB Tawi la Temeke amemruhusu Thomas David Malima kuchukua fedha jumla ya Tshs.140,000,000/= kati ya tarehe 30 Desemba, 2017 na 17 Januari, 2018 na hivyo kukiuka amri ya Mahakama Kuu ya zuio iliyotolewa Tarehe 19 Desemba, 2017 kupitia shauri Na. 51/2017.
Kutokana na UKIUKWAJI HUO WA AMRI ZA MAHAKAMA na kuzingatia msimamo wa Mahakama Kuu ya Tanzania kupitia Jaji Mkuu Prof. Ibrahim Hamis Juma; kuwashughulikia viongozi wa serikali na kisiasa wanaovunja amri za Mahakama, jopo la wanasheria wa CUF-Chama cha Wananchi limeshakamilisha taratibu za kisheria kuwafikisha mahakamani ili wajibu tuhuma zinazowakabili.
3. KUFUNGULIWA KWA AKAUNTI MPYA YA KUTOROSHEA FEDHA ZA RUZUKU:
Msaliti Lipumba akishirikiana na msajili wa vyama vya siasa Jaji Francis Katabazi Mutungi amefungua akaunti nyingine (Na. 22910021328) ya kutoroshea fedha za ruzuku katika benki ya NMB tawi la Malindi Zanzibar Tarehe 2 Januari, 2018. Hatua hiyo ni katika kutapatapa kuficha wizi wa ruzuku unaokiuka amri za mahakama ambao msajili wa vyama vya siasa Jaji Francis Katabazi Mutungi ameendelea kuufanya kumsaidia msaliti Lipumba kukidhi haja zake na wahuni anaowahifadhi Ofisi Kuu ya CUF-Chama cha Wananchi pale Buguruni. Aidha ufunguaji wa akaunti mpya huko Zanzibar, unalenga kukwepa amri ya mahakama iliyomzuia Thomas David Malima kujihusisha na masuala ya CUF-Chama cha Wananchi, ambapo kwa kufungua akaunti mpya wameteua watia sahihi wapya ambao ni: Haroub Mohamed Shamus, Khalifa Suleiman Khalifa na Mohamed Habib Mnyaa. Suala la Meneja huyo wa NMB Malindi Zanzibar kuwaruhusu kufungua akaunti kinyume na amri ya Mahakama Kuu, na agizo la Bodi halali la kufunga kwa muda akaunti zote zenye jina la CUF-Chama cha Wananchi na kutofunguliwa akaunti mpya kwa jina hilo nchi nzima, linafuatiliwa kwa hatua za kisheria.
4. KUHUSU NJAMA ZA LIPUMBA NA WASHIRIKA WAKE KUTAKA KUWAVUA UANACHAMA MADIWANI WA CUF MKOA WA DAR ES SALAAM:
Kufuatia hatua madhubuti zilizochukuliwa na uongozi halali wa CUF-Chama cha Wananchi, msaliti Lipumba na genge lake wamejikuta hawana njia rahisi za kuihujumu CUF kama ilivyokuwa hapo awali na hivyo kuendelea kupoteza uhalali wa kuikalia Ofisi Kuu ya CUF iliyopo Buguruni Dar es Salaam. Aidha wameingia katika mgogoro na washirika na wafadhili wao CCM na serikali zake kutokana na malengo yao kuelekea kutofanikiwa. Kwa muktadha huo, na baada ya kushauriana na mwanasheria wake Mashaka Ngole, msaliti Lipumba amepanga njama za kutaka kuwafukuza uanachama madiwani kwa tiketi ya CUF-Chama cha Wananchi mkoa wa Dar es salaam; wakiwemo wastahiki Manaibu Meya, kutokana na madiwani hao kukataa kumsaidia msaliti Lipumba na genge lake katika kampeni za uchaguzi mdogo jimbo la Kinondoni. Msaliti Lipumba na genge lake wamejikuta katika wakati mgumu kwa uamuzi wao wa kusimamisha mgombea wakipingana na uamuzi wa UKAWA wa kusimamisha mgombea mmoja kutoka miongoni mwa vyama washirika.
Uamuzi huo wa Lipumba ambao umetafsiriwa kuwa ni mpango wa kutaka kuzigawa kura ili kuisadia CCM ishinde, umeshitukiwa na wananchi wa jimbo la Kinondoni na kusababisha kususiwa mikutano yao ya kampeni na wadau mbalimbali.
Tayari jopo la wanasheria wa Chama (CUF TAASISI) wamejipanga kukabiliana na hujuma hiyo vilivyo.
Tutaendelea kutoa taarifa kwa wanachama wote na umma wa Watanzania kwa ujumla juu ya kila kinachoendelea kwa wakati muafaka. Tunatoa wito kwa wanachama wote, wapenda mabadiliko na demokrasia kwa ujumla kuzidi kuwa wastahimilivu na kuongeza kasi ya ushiriki wa shughuli mbalimbali za CUF Taasisi katika hatua hizi za mwisho za kumalizana na Wasaliti wa Mabadiliko na Demokrasia nchini.
CUF NI TAASISI IMARA, YENYE VIONGOZI MAKINI
HAKI SAWA KWA WOTE
____________________________________
MBARALA MAHARAGANDE
NAIBU MKURUGENZI WA HABARI,UENEZI
NA MAHUSIANO NA UMMA
TAREHE 6/2/2018
MAWASILIANO: Airtel-0784 001 408
Vodacom/ Tigo: 0767/ 0715 062 577
email:maharagande@gmail.com


No comments:
Post a Comment