TANGAZO


Tuesday, January 9, 2018

BALOZI SEIF IDDI APOKEA MATEMBEZI YA VIJANA KUADHIMISHA MIAKA 54 YA MAPINDUZI YA ZANZIBAR

Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM Balozi Seif Ali Iddi akiyapokea Matembezi ya Vijana 1,000 wa Umoja wa Vijana {UVCCM} walioanzia Mwera kuadhimisha Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar ya Mwaka 1964 hapo Afisi Kuu ya CCM Kisiwandui.(Picha zote na Hassan Issa – OMPR – OMPR – ZNZ)
Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM Balozi Seif Ali Iddi akiyapokea Matembezi ya Vijana 1,000 wa Umoja wa Vijana {UVCCM} walioanzia Mwera kuadhimisha Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar ya Mwaka 1964 hapo Afisi Kuu ya CCM Kisiwandui.
Balozi Seif akipokea Picha ya Muasisi wa Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar ya Mwaka 1994 Marehemu Mzee Abeid Aman Karume kutoka kwa Mkuu wa Matembezi ya Umoja wa Vijana ambae pia ni Mjumbe wa NEC Nd. Asya Khamis.
Balozi Seif akizungumza  Vijana walioshiriki katika matembezi ya kuadhimisha Miaka 54 ya Mapinduzi ya Zanzibar hapo katika viwanja vya Afisi Kuu ya CCM Kisiwandui Mjini Zanzibar.
Baadhi ya Viongozi wa Chama cha Mapinduzi wakifuatilia matukio mbali mbali yaliyojiri katika kilele cha Matembezi ya kuadhimisha Miaka 54 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar.

Na Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
9/1/2018.
MJUMBE wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM Balozi Seif Ali Iddi alisema Taifa linawategemea Vijana kusimamia kwa vitendo Mapinduzi ya kuondoa maovu yote yaliyolikabili Taifa ikiwemo Dawa za Kulevya na udhalilishaji Kijinsia ambao kwa kiasi kikubwa unatishia ustawi wa Taifa.

Alisema Taifa kupitia Serikali zote mbili inahitaji kuona Vijana wake Nchini wanakuwa chemchem ya kustawisha Maendeleo badala ya kuwa dimbwi la vurugu na matatizo.

Balozi Seif Ali Iddi alisema hayo wakati akiyapokea Matembezi ya Vijana 1,000 wa Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi {UVCCM} kuadhimisha Miaka 54 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar hapo katika Viwanja vya Afisi Kuu ya CCM Kisiwandui Mjini Zanzibar.

Alisema Mapinduzi yametekelezwa na Wazalendo wa Visiwa vya Zanzibar  kwa lengo la kuondoa matendo mabaya ikiwemo  ufisadi, uzembe, uonevu ubaguzi wa aina zote zile pamoja na mambo yote yanayorejesha nyuma  au kukwamisha juhudi za kujiletea maendeleo.

Balozi Seif alisema Dhama hiyo ya Mapinduzi Daima ya Marehemu Mze Abeid Aman Karume  ya kuondoa mabaya na kuleta mambo mema warithi wake wa halali ni Vijana ambao Serikali ina wajibu wa kuwajengea mazingira bora ikiwemo suala la ajira litakalowawezesha  kuwa na utulivu wa kutekeleza  jukumu walilokabidhiwa na Taifa.

Alisema ukosefu wa ajira kwa Vijana hapa Nchini sio nzuri na ni miongoni mwa changamoto zinazohitaji ushirikiano wa karibu kati ya Vijana na Serikali na ushahidi uko wazi wa nafasi moja ya ajira kugombaniwa na zaidi ya Vijana 20.

Alisema miongoni mwa juhudi za Serikali katika kukabiliana na ukosefu wa ajira kwa Vijana ni kuongeza nafasi za mafunzo ya kazi za amali hapa Nchini ambapo vituo vua amali Viwili vinategemewa kujengwa  Makunduchi Mkoa wa Kusini Unguja na Mtambwe Mkoa wa Kaskazini Pemba.

Alieleza Vituo hivyo vitafanya  idadi ya Vituo Vinne vya amali nchini ambavyo vinategemewa kuchukuwa  idadi kubwa ya Vijana ambao watakapomaliza mafunzo yao watakuwa na uwezo wa kujiajiri wao wenyewe badala ya kusubiri ajiza za Serikalia mabzo kwa kipindi hichi bado finyu.

Balozi Seif alieleza mpango mwengine wa uhakika  wa kupambana na changamoto hiyo ni ule wa kukuza Uchumi kwa njia ya kukaribisha Wawekezaji katika sekta ya Utalii  itakayokuwa na uwezo mkubwa wa kubeba Vijana wengi.

Alieleza Mrdi mkubwa kuliko wote uliowekezwa Afrika Mashariki wa Zanzibar Amber Resort wenye thamani ya Dola za Kimarekani Bilioni 1.6 sawa na shilingi za Kitanzania Trilioni 2.1 unategemewa mkombozi kwa Vijana wengi Visiwani Zanzibar.

Balozi Seif  amewapongeza Vijana wa Uzalendo wao wa kulitumikia Taifa la Tanzania kwa moyo thabiti bila ya kutegemea malipo yoyote.

Akizungumzia joto lililomo miongoni mwa Vijana wa CCM  la kutaka kuifuta mara moja Serikali ya Umoja wa Kitaifa lilotokana na kutoshiriki katika  Uchaguzi  Chama Shiriki ya Umoja huo Balozi Seif alisema hilo ni suala la Kikatiba.

Balozi Seif  alifahamisha kwamba uondoaji wa Suala hilo unahitaji unaliza wa uwepo wa kura ya Maoni itakayotoa ridhaa ya Wananchi mfumo upi wanauhitaji kuufuata.

Hata hivyo Balozi Seif aliwaomba Wanachama wa Chama cha Mapinduzi na Wananchi wote wanaounga mkono Chama hicho kujitahidi kukiimarisha  ili unapofika wakati wa uchaguzi CCM inanyakua viti vingi na kuondoa haja ya kuunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa.

Mapema Kaimu Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Vijana wa CCM Zanzibar Nd. Abdulghafar  Idrissa alisema Vijana wa Umoja huo wameridhika na utekelezaji wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kuwaletea Maendeleo Wananchi wote.

Alisema Jamii inaendelea kushuhudia miradi mbali mbali mikubwa na midogo inayoibuliwa na Serikali katika pembe zote za Visiwa vya Zanzibar ikilenga kustawisha maisha ya Wananchi wote bila ya ubaguzi.

Hata hivyo Kaimu Naibu Katibu Mkuu huyo wa UVCCM Zanzibar alielezea masikitiko yake kutokana na baadhi ya Watendaji wa Serikali ngazi za kati wenye tabia ya kuwasengenya na kuwanyanya Vijana wa CCM wakati wanapohitaji huduma katika Taasisi wanazozisimamia.

Alitoa onyo kwa watendaji hao ambao wote wanaeleweka kuacha tabia hiyo kwani dawa yao yao ya kuwatangaza hadhani itatangazwa ndani ya mwaka mmoja kuanzia sasa.

Akitoa salamu Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa CCM Tanzania { UVCCM} Nd. Kheir James alisema katika kuyalinda Mapinduzi Matuykufu ya Zanzibar ya Mwaka 1964  asiyejua asili yake anastahiki kuwajibishwa.

Nd. Kheir alitahadharisha wazi kwamba Mtu au kikundi kinachojitokeza kuchezea shere Mapinduzi ya Zanzibar  awe makini kupata dhoruba za Vijana wa Chama cha Mapinduzi chenye asili ya Mapinduzi hayo.

Alisema ili Mapinduzi yaendelee kuwa na Heshima lazima Jamii iyalinde na kuyatetea kupitia Vijana watakaokuwa tayari kujitolea muhanga kwa kulinda heshima hiyo ya Taifa.

No comments:

Post a Comment