TANGAZO


Tuesday, November 28, 2017

Uchaguzi Kenya2017: Rais Uhuru Kenyatta aapishwa

Kenyatta na Ruto wafunga sherehe kwa maombi

Rais Kenyatta na Naibu Rais William Ruto wamekamilisha sherehe za leo uwanja wa Kasarani kwa maombi, Bw Kenyatta ameongoza kwa Kiingereza na Bw Ruto kwa Kiswahili.
Baadaye, wimbo wa Jumuiya ya EAC umechezwa na kisha wimbo wa taifa la Kenya kuhitimisha sherehe za leo.
Wageni wameanza kuondoka uwanjani, wakianza na viongozi wa nchi.

Kenyatta awahimiza Wakenya kuishi kama majirani

Kwa mara nyingine, Bw Kenyatta amewahimiza Wakenya kuishi kama majirani. Amesema majirani hufaana sana na ndio hutegemewa wakati wa shida.
Ameagiza watahiniwa wote wa darasa la nane waliofanya mtihani wao mwaka huu wawe wamefahamu shule za sekondari watakazojiunga nazo kabla ya Krismasi.

Kenyatta: Mwafrika yeyote atapata viza akifika Kenya

Rais Kenyatta ametangaza kwamba Mwafrika yeyote atapewa viza akifika katika kiingilio chochote mpakani au viwanja vya ndege Kenya.
Amesema hataweka masharti kwamba lazima mataifa mengine yafanye hivyo.
Amechukua hatua sawa na iliyochukuliwa na Rwanda majuzi.
Nchini Rwanda hata hivyo, ni raia wa taifa lolote lile.
Ameahidi pia kufufua moyo wa Jumuiya ya Afrika Mashariki. Amesema wananchi wa nchi wanachama watahesabiwa kama Wakenya. Watahitajika tu kutumia kitambulisho. Wanaweza kuingia au kutoka na kufanya kazi, kumiliki mali au hata kuoana bila kuwekewa masharti.
Amesema hata hivyo kwamba sheria nayo itatumika kwa njia sawa.

Kenyatta: 'Siasa si chakula'

Rais amesema siasa zimetumiwa vibaya Kenya kutatiza ustawi wa taifa "badala ya ilivyo nchi za Asia."
Amesema "hakuna aliyewahi kula siasa".

Kenyatta: Tutazungumza na mahakama kuhusu kesi

Rais Kenyatta amesema atazungumza na Idara ya Mahakama kujadiliana kuhusu kuharakishwa kwa kesi ambazo zimekwama miaka mingi.
Aidha, amesema watazungumzia kesi nyingi ambazo zinatumiwa kukwamisha miradi ya serikali.

Kenyatta: Gharama ya umeme itapunguzwa usiku

Rais Kenyatta amesema kuanzia Desemba mwaka huu, gharama ya umeme itapunguzwa usiku, kwa asilimia 50, kati ya saa nne usiku na saa thenashara alfajiri.
Amesema hii ni kusaidia ukuaji wa uchumi wa saa 24.

Kenyatta: Nitaangazia umoja wa taifa na huduma ya afya

Kenyatta amesema ana malengo mawili muhula wake wa mwisho. Kwanza kuimarisha uwiano na umoja miongoni mwa Wakenya.
Amesema ameanza kuwasiliana na viongozi wote na kueleza nia yake ya kuendeleza umoja.
Amesema lengo la pili ni kuhakikisha huduma ya afya inawafikia Wakenya 100%.
Katika miaka mitano ijayo, nitahakikisha Wakenya 13 milioni wanafaidi kupitia huduma ya NHIF. NHIF itafanyiwa mageuzi pamoja na sheria za kusimamia kampuni za bima za kibinafsi.
Amesema atafanikisha mpango wa kumiliki nyumba na makazi.
"Kwa miaka mitano ijayo serikali yangu itaangazia kuhakikisha watu wengine 500,000 wanajipatia nyumba," amesema.

Uwanja wa Jacaranda ni kama mahame

Uwanja wa Jacaranda, Embakasi jijini Nairobi ambapo muungano wa upinzani Kenya Nasa ulipanga kufanya mkutano umebaki kama mahame.
Polisi wamezingira milango yote ya kuingia uwanja huo.
Mwandishi wetu Roderick MacLeod ametutumia picha hii ya hali ilivyo ndani ya uwanja:
Jacaranda
BBC

Kenyatta: Najivunia ugatuzi na miundo mbinu

Rais amesema anajivunia mambo manne ambayo serikali yake ilitimiza miaka minne iliyopita. Mwanzo ugatuzi wa mamlaka na rasilimali, pili ni msingi wa ukuaji wa kiuchumi na kibiashara. Pia ujenzi wa reli ya kisasa na kusambazwa kwa umeme mashinani.
"Tatu tumewekeza katika mageuzi yanayoboresha utoaji wa huduma ya afya. Aidha, upanuzi wa miundo mbinu ya hospitali na Bima ya Afya ya Taifa (NHIF).
"Nne, tumefanyia mageuzi mfumo wetu wa elimu. Kurejesha imani katika mfumo wa mitihani na kuimarisha tena taasisi za elimu."

Kenyatta: Tunaweza kujenga Kenya tunayojivunia

Rais amesema kwa pamoja, bila kujali tofauti za kidini na za kijamii, Wakenya wanaweza kujenga Kenya imara na inayostawi kwa pamoja.
Lakini amesema lazima waacha kuangazia makovu ya kale, na pia kwa kufuata sheria.
"Sheria lazima itawale. Inafaa kuwa kimbilio kwa kila Mkenya na hakuna yeyote anafaa kuvunja sheria au kwenda nje ya mfumo wa sheria bila kujali ukubwa wa malalamiko yako.
"Niwakumbushe, Mahakama ya Nje ilipotutaka tujitee, tulitii. Mahakama ya Juu ya Kenya ilipofuta uchaguzi wetu, hata baada ya kushindwa, baada ya kuambiwa utaratibu ulikuwa muhimu kuliko kula, tuliheshimu uamuzi huo.
"Serikali yangu imedhihirisha kujitolea kuheshimu sheria. Tunatarajia raia wote wengine wafanye hivyo."
"Katiba yetu imeunda mihimili mitatu huru ya serikali...lazima kila mtu afanye kazi yake."
"Matamanio ya binadamu wakati mwingine huzidi kipimo, na yasipodhibitiwa, yanaweza kulibomoa taifa. Ili kuishi pamoja, lazima watu wakubaliane kufuata sheria fulani. Kenya ni nchi ya watu zaidi ya 40 milioni. Tumeishi pamoja ishara kwamba hata tukitofautiana huwa twajua jinsi ya kuungana tena.
"Matatizo mengi hutokea tunapokosa kufuata sheria hizi. Miezi minne iliyopita, tumefanyia majaribio sheria hizi. IEBC, Mahakama, Idara za Usalama. Hizi zote zimefanyiwa majaribio na siasa, na zimesalia imara.
"Uamuzi usipoenda unavyotaka, unaheshimu, hiyo ni demokrasia.
"Tumejifunza kwamba taasisi zetu ni kakamavu kuliko tulivyodhani awali."
"Hatufai kubomoa taasisi zetu kila wakati zikikosa kutoa matokeo tunayotaka."

Kenyatta: Leo ni mwisho wa shughuli yetu ya uchaguzi

Kenyatta amesema leo ni siku ya 123 tangu kufanyika kwa uchaguzi Agosti 8 na kusema shughuli ya uchaguzi sasa imefikia kikomo, na akasisitiza tena.
Anaonekana kupuuzilia mbali upinzani ambao umekuwa ukisisitiza kwamba uchaguzi wa 26 Oktoba haukuwa huru na wa haki na kwamba uchaguzi mpya unafaa kuandaliwa.

Kenyatta: Nitakuwa rais wa Wakenya wote

Bw Kenyatta amesema aliwasikiliza kwa makini wapinzani wake uchaguzini na kwamba atatekeleza baadhi ya mawazo na mapendekezo yao.
"Naahidi kulinda ndoto za wote na maono ya wote, walionipigia kura na waliokosa kunipigia kura. Nitakuwa rais wa wote. Na nitajitolea muda wangu na nguvu kujenga madaraja, kuunganisha Wakenya na kuleta ustawi."

Kenyatta aishukuru mahakama kwa maamuzi huru

Bw Kenyatta amesema Mungu aliyajibu maombi na kwamba atawafikisha Wakenya mbali.
Ameishukuru tume ya uchaguzi kwa kuendesha uchaguzi, chini ya shinikizo nyingi.
Ameisifu Mahakama na kusema ilifanya maamuzi yake kwa uhuru.

Kenyatta: Asanteni sana Wakenya

Rais Kenyatta sasa anahutubu na ameanza kwa kuwashukuru waliohudhuria.
Ameomba kuhutubia kwa Kiingereza kwa sababu ya wageni.

Museveni awahimiza Wakenya wazingatie amani

"Hamjambo Wakenya?" ameanza, na kusema amefika kutuma hongera, na kuwapongeza Wakenya kwa kudumisha amani.
"Nawaomba Wakenya wote wakumbuke mambo matatu manne muhimu. Jambo la kwanza ni amani. Jambo la pili ni ustawi wa jamii. Jambo la tatu maendeleo. Na jambo la nne siasa."
"Msifikirie siasa peke yake mkasahau yale mengine matatu."

Lungu: Kama marafiki tulikuwa na wasiwasi

Rais wa Zambia Edgar Lungu amealikwa kuhutubu kwa niaba ya viongozi wengine wa mataifa.
"Wakenya Mpo? Asante sana," ndivyo alivyoanza.
Amewapongeza Wakenya.
"Tuna furaha sana kwamba shughuli hii imekamilika, tunawahimiza tu mrejee kazini. Kama marafiki, tulikuwa na wasiwasi kwamba shughuli hii ilichukua muda mrefu. Tunatumai mtalifikiria hilo siku za usoni.
Ali Bongo Ondimba wa Gabon pia amealikwa kuhutubu na kusema anajivunia sana leo kuwa Mwafrika.
"Nyinyi watu wa Kenya mmetufanya kujionea fahari sana," amesema.
"Wananchi wa Kenya hamjambo? Tumekuja hapa kusema hongera, hongera sana," huyo naye ni Paul Kagame wa Rwanda.
Kumalizia ni mwenyekiti wa sasa wa Jumuiya ya Afrika Mashariki Yoweri Museveni.

Ruto: Tumekusanyika pia kusherehekea demokrasia

Bw Ruto amesema leo pia Wakenya wamekusanyika kusherehekea demokrasia ya Kenya, baada ya uchaguzi.
"Kwamba tuna uwezo wa kuamua mustakabali wetu, kuwachagua viongozi wetu na mwelekeo wa taifa letu la Kenya."
Amesema uchaguzi wa wakati huu ulikuwa na mambo mawili wakuu, tofauti na ule wa 2013.
Kwamba serikali iliungana chini ya chama cha Jubilee na upinzani uliungana chini ya Nasa.
Ripoti
Amesema pia badala ya ukabila, kampeni ziliangazia zaidi masuala ya umuhimu kwa wananchi.
"Hizi ni ishara za hatua tulizopiga kama taifa kuelekea kwenye siasa zilizokomaa," amesema.
Ameahidi kumuunga mkono Rais Kenyatta kuunganisha jamii mbalimbali za Kenya.
"Sote (kama Wakenya) lazima tuungane pamoja na kukataa chuki, ukabila, migawanyiko na kukataa ghasia," amesema, na kuongeza kuwa muhimu zaidi ni ustawi na maendeleo ya nchi, mambo ambayo ameeleza kuwa hayawezi kupatikana bila amani.
"Na amani haiwezi kupatikana bila haki, na haki haiwezi kupatikana bila kuheshimu sheria," amesema.

William Ruto ahutubu Kasarani, aongoza wimbo

Baada ya kipindi cha burudani, Naibu Rais Ruto ameanza kuhutubu. Amesema wamefika walipo sio kwa nguvu zao bali mapengi ya Mungu.
"Ndio nimesikia mkiimba asubuhi, kwa si uchawi ni maombi."
Anaongoza wimbo: Hakuna Mungu kama Wewe.

Sherehe rasmi ya kumuapisha rais yakamilika

Msajili wa mahakama Anne Amadi ametangaza kwamba sasa sherehe rasmi ya kumuapisha Rais na Naibu wake imekamilika. Maafisa wakuu wa mahakama na Rais na Naibu wake wamepigwa picha kadha.
Sehemu inayofuata ya sherehe, ambayo ni burudani na hotuba sasa inaanza.
Mizinga 21 itafyatuliwa pia kwa heshima ya Rais.

Maraga amtambulisha Naibu Rais Ruto

Baada ya Bw Ruto kula kiapo na kutia saini hati za kiapo, Jaji Mkuu amemtambulisha kama Naibu Rais kwa wananchi Kasarani.

Maraga amtambulisha Naibu Rais Mteule

Jaji Mkuu David Maraga sasa anamtambulisha Rais Mteule William Ruto ambaye pia atalishwa kiapo cha utiifu na kiapo cha kuhudumu kama Naibu Rais wa Kenya.

Maraga: Namtambulisha sasa Rais Wakenya

Jaji Mkuu Maraga: "Wananchi, sasa ni furaha yangu kuu kumtambulisha kwenu Rais wa Jamhuri ya Kenya."

Biblia ya uhuru yatumiwa kumwapisha Uhuru Kenyatta

Mfawidhi wa sherehe amefafanua kwamba nakala ya Biblia iliyotumiwa kumwapisha Rais ni ile iliyotumiwa kumwapisha rais wa kwanza wa Kenya Jomo Kenyatta ambaye ni babake rais wa sasa.
Nakala ya Katiba ni iliyotiwa saini wakati wa kurasmishwa kwa Katiba ya sasa mwaka 2010 uwanjani Uhuru Park.
Usalama umeimarishwa uwanjani Uhuru Park.
Gari la Uhuru
BBC

HABARI ZA HIVI PUNDEKenyatta aapishwa kutekeleza majukumu ya urais

Msajili wa Mahakama Anne Amadi, anamlisha sasa kiapo cha kutekeleza majukumu ya afisi ya rais.
Rais Kenyatta: "Nitatekeleza majukumu yangu, na wajibu wangu katika afisi ya rais wa Kenya, na kwamba nitatenda haki kwa wote kwa mujibu wa katiba hii kama ilivyo kwenye sheria, na sheria za Kenya bila woga, mapendeleo au ubaguzi au nia mbaya. Ewe mwenyezi Mungu nisaidie."
Baadaye, ametia saini viapo vyote viwili, kisha cheti cha kuapishwa, kuthibitisha kwamba sherehe ya leo imefanyika.
Jaji Mkuu David Maraga pia ataweka saini yake kwenye stakabadhi zote tatu (vipao viwili) na cheti cha kuapishwa kwa Rais.

HABARI ZA HIVI PUNDERais Kenyatta ala kiapo cha utiifu

Rais Kenyatta: "Naapa kwamba nitakuwa mwaminifu, kikamilifu, kwa Jamhuri ya Kenya, kwamba nitatii, nitahifadhi, kulinda na kutetea Katiba ya Kenya kama ilivyo kwenye sheria, na sheria nyingine zote za Jamhuri. Na kwamba nitalinda mipaka na heshima ya watu wa Kenya. Ewe Mwenyezi Mungu nisaidie."

Maraga amtambulisha Rais Mteule Uhuru Kenyatta

Jaji Mkuu David Maraga amesema kwa mujibu wa Katiba na Sheria: "Mimi David Kenani Maraga, Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Kenya, hapa, namtambulisha kwa watu wa Kenya Rais Mteule Mheshimiwa Uhuru Kenyatta." Hadhira inashangilia.

Maraga aalikwa jukwaa la kumwapisha Rais

Bi Amadi amekaribishwa jukwaa la kumwapishia rais. Amemtambua Rais mteule Uhuru Kenyatta, huku hadhira ikishangilia. Amemtambulisha mkewe rais, Margaret, Naibu Rais mteule na mke wake William Ruto na Rachel.
Amewatambua pia wageni wengine waheshimiwa.

Msajili wa mahakama ajiandaa kumlisha kiapo rais

Msajili wa Mahakama Anne Amadi amechukua usukani, ambapo anatarajiwa kumlisha kiapo rais mbele ya Jaji Mkuu David Maraga.
Anafafanua kuhusu utaratibu wa kulishwa kiapo ulivyo kwenye katiba na sheria.

No comments:

Post a Comment