TANGAZO


Saturday, November 25, 2017

NEC YASISITIZA AMANI NA USALAMA UCHAGUZI MDOGO WA MADIWANI KATA 43

Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi Jaji Semistocles Kaijage

Na Clarence Nanyaro – NEC 
25/11/2017 ARUSHA.
TUME ya Taifa ya Uchaguzi  (NEC) imevitaka vyama vya Siasa na wadau mbalimbali wa Uchaguzi kuhakikisha kuwa Uchaguzi Mdogo wa Madiwani utakaofanyika kesho (Jumapili) Novemba 22, 2017 unafanyika kwa amani na Utulivu na kutoa wito kwa wananchi kujitokeza kwa wingi kupiga Kura.

Akisoma risala kwa umma leo Jijini Arusha  Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya uchaguzi Jaji Semistocles Kaijage amesema kuwa Wapiga Kura wapatao 333,309 wanatarajiwa kupiga Kura kuwachagua Madiwani katika Kata 43 za Tanzania Bara na kuongeza kuwa uchaguzi huo utafanyika katika Vituo 884 vya Uchaguzi ambako ndipo Wapiga kura walijiandikishia kupiga kura katika Uchgauzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani wa Mwaka 2015.

Amesema kuwa tofauti na Chaguzi zilizopita,Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC)  kwa kuzingatia masharti ya sheria ya Uchaguzi ya Serikali za Mitaa kifungu cha 62 imewaruhusu wapiga kura ambao ama kadi zao za kupigia kura  zimepotea au kuchakaa  au kufutika kutumia vitambulisho mbadala kwenda katika vituo walivyojiandikisha ili waweze kupiga kura katika uchaguzi huu.

Jaji Kaijage amesisitiza  kuwa masharti ya Mpiga Kura kuruhusiwa kutumia kitambulisho mbadala yatazingatia  sharti la kwamba majina ya mpiga kura lazima yafanane kwa herufi  na majina yaliyoko katika kitambulisho mbadala ambayo yako katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura.

Ameeleza kuwa katika kutekeleza hatua hiyo, vitambulisho mbadala ambavyo Tume ya Taifa ya uchaguzi imeruhusu  vitumiwe na Wapiga kura katika uchaguzi mdogo wa Udiwani ni leseni ya udereva, kitambulisho cha uraia kinachotolewa na Mamlaka ya utambulisho nchini (NIDA), pamoja na pasi ya Kusafiria.

Aidha, katika risala hiyo Jaji Kaijage amewataka Wasimamizi na Wasimamizi wasaidizi wa Uchaguzi katika vituo vya kupigia kura kutoa kipaumbele  kwa makundi maalum wakati wa kupiga kura. Aliyataja makundi hayo kuwa ni Wenye ulemavu wa aina mbalimbali, Wajawazito, Wenye watoto wachanga, Wazee na Wagonjwa.

Kuhusu Mawakala wa vyama  vya siasa katika vituo vya Kupigia kura,Jaji Kaijage aliwasihi kufuata na kuzingatia,sheria Kanuni  na taratibu zinazoongoza Uchaguzi katika kipindi chote cha Kupiga,Kuhesabu na  kujumlisha kura vituoni.

Aidha, Jaji Kaijage, amewataka Wananchi,wapenzi na Wakereketwa wa vyama kutofanya kampeni ya aina yeyote katika siku ya upigaji kura ikiwemo kusambaza Vipeperushi, kuwa na bendera za Vyama vyao, na mavazi na kuwataka wananchi kueshimu sheria za nchi wakati wote wa upigaji Kura,kuhesabu na kujumlisha kura.

Katika Uchaguzi huu mdogo unaofanyika leo,Mkoa wa Arusha unaongoza kwa kuwa na Kata Nane ambazo zinafanya Uchaguzi huo. Kata hizo ni Ambureni,Makiba Maroroni, Leguruki na Ngabobo katika Halmashauri ya Meru,Kata ya Musa katika Halmashauri ya Arusha, Kata ya Muriet katika Jiji la Arusha na Kata ya Moita katika Halmashauri ya Wilaya ya Monduli.

Uchaguzi huu ni wa Pili tangu kuanza kwa Mwaka huu,ambapo Tume ya Taifa ya Uchaguzi inatakiwa kufanya Uchaguzi wa Madiwani mara mbili kwa Mwaka kwa Mujibu wa sheria. Uchaguzi mdogo mwingine wa Ubunge na Udiwani ulifanyika Januari 22, 2017.

No comments:

Post a Comment