Mkurugenzi
wa TEHAMA – TAMISEMI, Erick Kitali alipokuwa akizungumza na wafanyakai wa
Halmashauri (hawapo pichani) wakati wa kufunga mafunzo ya siku nane yaliyohusu Mfumo
ulioboreshwa wa kuandaa Mpango wa Bajeti za Mamlaka ya Serikali za Mitaa ujulikanao
kama PlanRep jana Mjini Morogoro.
Meneja
Mifumo ya TEHAMA kutoka kwenye Mradi wa Uimarishaji Mifumo ya Sekta za Umma
(PS3), Revocatus Mtesigwa akizungumza na wafanyakazi wa Halmashauri (hawapo
pichani) waliopewa mafunzo ya Mfumo ulioboreshwa wa kuandaa Mpango wa Bajeti za
Mamlaka ya Serikali za Mitaa ujulikanao kama PlanRep wakati wa ufungaji wa
mafunzo hayo uliofanyika jana Mjini Morogoro. Kutoka kushoto ni Mkurugenzi wa
TEHAMA – TAMISEMI, Erick Kitali na Mmoja wa wawezeshaji wa mafunzo hayo,
Christopher Masaaka. Mmoja wa wawezeshaji wa mafunzo hayo, Christopher Masaaka akiwaasa wafanyakazi wa Halmashauri (hawapo pichani) waliopewa mafunzo ya Mfumo ulioboreshwa wa kuandaa Mpango wa Bajeti za Mamlaka ya Serikali za Mitaa ujulikanao kama PlanRep wakati wa ufungaji wa mafunzo hayo uliofanyika jana Mjini Morogoro.Kushoto ni Mkurugenzi wa TEHAMA – TAMISEMI, Erick Kitali.
Na Jacquiline Mrisho – Maelezo, Morogoro.
WAFANYAKAZI wa Halmashauri nchini wamekumbushwa kuacha kufanya kazi kwa mazoea ili waweze kwenda na kasi kubwa katika kuiletea nchi maendeleo.
Rai hiyo imetolewa jana Mjini Morogoro na Mkurugenzi wa TEHAMA – TAMISEMI, Erick Kitali alipokuwa anafunga mafunzo ya siku nane yaliyohusu Mfumo ulioboreshwa wa kuandaa Mpango wa Bajeti za Mamlaka ya Serikali za Mitaa ujulikanao kama PlanRep.
Kitali amesema kuwa wafanyakazi wengi wa Halmashauri nchini wamekuwa wakifanya kazi vile wanavyotaka wao huku baadhi yao wakishindwa kufata utaratibu uliowekwa lakini kwa sasa wakati huo umepita hivyo kila mmoja anatakiwa ajitume kwa kuangalia mbele zaidi na kufanya kazi ambayo itabaki kuwa historia nzuri kwa wananchi.
“Rais wetu Dkt. Magufuli anajitahidi kuipeleka nchi mbele kimaendeleo na kama mjuavyo Halmashauri zote ziko chini ya TAMISEMI ofisi ambayo iko chini ya Ofisi ya Rais hivyo hatutakiwi kumuangusha Mkuu wetu, tunatakiwa kwenda na kasi zaidi ya aliyokuwa nayo yeye,” alisema Kitali.
Kitali ameongeza kuwa zamani watu walikuwa wakipelekwa kwenye semina wanafanya kama sehemu ya kutalii lakini kwa sasa ukipewa mafunzo kama hayo unakuwa umepewa jukumu ambalo kwa namna moja ama nyingine unatakiwa ulifanyie kazi.
Aidha, Kitali amewataka wafanyakazi waliopewa mafunzo ya PlanRep wakayafanyie kazi kwa kuwapa ujuzi wenzao waliowaacha katika vituo vyao vya kazi ili kwa pamoja waweze kupanga mipango na bajeti makini kwani siku zote umoja ni nguvu na utengano ni udhaifu.
Kwa upande wake Meneja Mifumo ya TEHAMA – PS3, Revocatus Mtesigwa amewahakikishia wafanyakazi hao kuwa wameyachukua maoni yao na watakwenda kuyafanyia kazi kwa ajili ya kuuboresha zaidi mfumo huo.
“Mfumo sio kitu cha kukamilika kwa siku moja, kila muda unatakiwa uboreshwe hivyo kwa kuwa nyie ndio mtakaoenda kuutumia na mmetoa mapendekezo mengi ya kuuboresha zaidi basi mawazo yenu tumeyachukua na tutayafanyia kazi ili kuleta matokeo mazuri,” alisema Mtesigwa.
Mtesigwa ametoa rai kwa wafanyakazi waliopewa mafunzo hayo kufanya vizuri katika Halmashauri zao kwa kuwafundisha wenzao kwa juhudi ili waweze kuchaguliwa kuwa wawezeshaji watakaokuwa wanatembea nchi nzima kuwafundisha wengine kwani mradi huo ni mkubwa na bado unahitaji wawezeshaji wengi.
Mafunzo haya ya siku 8 yamefadhiliwa na Shirika la Msaada la Marekani (USAID) pamoja na Serikali ya Tanzania, mafunzo yalihusisha maafisa wa Serikali wanaotumia mfumo huo wa PlanRep wakiwemo; Waganga Wakuu, Makatibu wa Afya, Maafisa TEHAMA, Wachumi, Wahasibu na Maafisa Mipango wa Serikali.


No comments:
Post a Comment