BBC
Muungano wa upinzani Kenya umeendelea kupinga matokeo ya uchaguzi wa urais yanayotangazwa na tume hiyo kwenye mtandao wake.
Viongozi wa muungano wa National Super Alliance wamesema walikutana na wakuu wa Tume ya Uchaguzi Kenya na kuwasilisha rasmi malalamiko yao kupitia barua.
Ajenti mkuu wa upinzani Musalia Mudavadi, ambaye ni naibu waziri mkuu wa zamani, amesema upinzani umepata maelezo zaidi kwamba matokeo ya uchaguzi yalivurugwa baada ya kudukuliwa kwa mitambo ya IEBC.
Wakuu wa IEBC wamekanusha kwamba mitambo ilidukuliwa. Mwenyekiti Wafula Chebukati amesema kulikuwa na jaribio la kudukua mitambo hiyo, lakini halikufanikiwa.
Bw Mudavadi amedai mgombea wa upinzani Raila Odinga ndiye aliyeshinda uchaguzi huo.
“Twamtaka mwenyekiti wa IEBC atangaze matokeo na kumtangaza Odinga na Kalonzo rais mteule na naibu rais mteule wa Kenya mara moja,” amesema Bw Mudavadi.
Nchini Kenya, ni kinyume cha sheria kwa mtu yeyote kutangaza matokeo au kusambaza matokeo ambayo hayajatoka kwa tume ya taifa ya uchaguzi. Ni tume hiyo ya uchaguzi pekee inayoruhusiwa kutangaza matokeo.
Bw Mudavadi ameendelea kuwaomba Wakenya kuwa watulivu.
Sehemu ya soko kuu mjini Garissa, kaskazini mashariki mwa Kenya, imeteketea baada ya mfarakano kati ya wafuasi wa wagombea wawili wa ugavana katika kaunti hiyo.
Fujo zilizuka baada ya matokeo ya uchaguzi huo uliofanyika Jumanne kutangazwa.
Ali Bunow Korane wa chama cha Jubilee chake Rais Kenyatta alitangazwa mshindi.
Taarifa zinasema watu wasioridhishwa na matokeo hayo walichoma moto sehemu za soko hilo.
Hali ya utulivu imerejea lakini wazima moto wameendelea kukabiliana na moto huo.
Korane alipata kura 55 335 (51,48%) naye mpinzani wake wa karibu Nathif Jama Adan wa chama cha Wiper akapata kura 50 471 (46,95%).
Bw Adan ndiye gavana anayeondoka.
BBC
BBC
Mkuu wa utumishi wa umma nchini Kenya Joseph Kinyua amewaamuru watumishi wote wa umma kurejea kazini baada ya "kufanyika kwa uchaguzi wa kufana kwa njia ya amani."
Matokeo rasmi ya uchaguzi wa urais bado hayajatangazwa, ingawa tume ya uchaguzi imedokeza kwamba huenda yakatangazwa baada ya saa sita mchana kesho Ijumaa.
Serikali ilikuwa imetangaza Jumanne pekee, siku ya uchaguzi, kuwa siku ya mapumziko.
Hapa chini ni taarifa iliyotumwa na Bw Kinyua:
BBC
Hali ya kawaida ilirejea mjini Kisumu, magharibi mwa Kenya baada ya polisi kukabiliana na vijana waliokuwa wanaandamana na kufunga barabara katika baadhi ya maeneo.
Mwandishi wetu Peter Njoroge, ametutumia picha hizi:
BBC
BBC
Mgombea wa pili wa urais nchini Kenya Dkt Ekuru Aukot amekubali kushindwa.
Ndiye wa pili kutangaza kushindwa baada ya Dkt Japheth Kavinga Kaluyu kukubali kushindwa jana.
Dkt Aukot amesema anaamini "Wachache walipata fursa ya kusikika, na wengi walishinda."
"Jiwe la Daudi halikumuweza Goliathi wakati huu, na asiyekubali kushindwa si mshindani," amesema.
Ametoa wito kwa Raila: "Hatungekuwa hapa bila wewe, demokrasia ya Kenya ya sasa haiwezi kuzungumziwa bila wewe kuwepo.
Kenya yataka kusonga mbele, Wakenya wanataka kurejelea shughuli za kawaida.
Kwa kuchunguza Fomu 34A tulizopata, tumegundua kwamba hakuna sababu ya kuamini kuna chochote kitabadili matokeo ya sasa."
Amemtaka Rais Kenyatta, akitangazwa mshindi, aunde serikali yake kwa kujumuisha wote.
Dkt Aukot amedokeza kwamba huenda akawania tena urais mwaka 2022.
Soma zaidi kumhusu Dkt Aukot hapa: Ekuru Aukot: ‘Daktari wa Katiba’ anayetaka kuwa rais Kenya
Hata kabla ya matokeo rasmi ya uchaguzi nchini Kenya ujumbe wa kumpongeza mshindi wa urais umechapishwa katika akaunti ya Twitter ya Rais wa Burundi Pierre Nkurunziza.
Bw Nkurunziza anaonekana kumpongeza Rais Kenyatta.
Lakini labda ni afisa wa mawasiliano wa Nkurunziza ambaye ameandika ujumbe huo.
Kwenye maelezo katika ukurasa huo wa Twitter, ambao una wafuasi 59,000, ujumbe wa moja kwa moja kutoka kwa rais huyo unafaa kuwa na sahihi ya PN.
Mwenyekiti wa IEBC Wafula Chebukati amethibitisha kwamba kulikuwa na jaribio la kudukua mitambo ya tume hiyo.
Hata hivyo, amesema wadukuzi hawakufanikiwa.
Muungano wa upinzani NASA ulikuwa umedai mitambo ya tume hiyo ilidukuliwa siku ya uchaguzi na matokeo yaliyokuwa yakipeperushwa katika tovuti ya tume hiyo yalikuwa 'yamechakachuliwa'.
Mwenyekiti wa IEBC Wafula Chebukati anahutubia wanahabari ukumbi wa Bomas, Nairobi akiandamana na Afisa Mkuu Mtendaji Ezra Chiloba.
Bw Chebukati amesema matokeo yamekuwa yakiingia kutoka vituoni usiku na asubuhi.
"Tume imejitolea kutekeleza wajibu wake.
Tunakaribisha taarifa za awali za waangalizi wa uchaguzi wa nchini na hata nje ya nchi, ambao wote wanakubali kwamba uchaguzi ulikuwa wa uwazi, huru na wa haki
Tunawahakikishia Wakenya kwamba tutadumisha kiwango hiki cha uwazi.
Kufikia sasa tumepokea Fomu 34A kutoka vituo 29,499 kati ya vituo vyote 40,883.
Kuhusu Fomu 34B, za kujumlisha matokeo maeneo bunge, tumepokea kutoka maeneo 117 kati ya 290.
Fomu 34B ni za kujumlisha matokeo ya Fomu 34A katika eneo bunge, na zitaongoza tangazo la jumla la matokeo ya urais.
“Tumefanya kila tuwezalo kuhakikisha uchaguzi umekuwa huru na wa haki.
“Tunajizatiti kutoa matokeo haraka iwezekanavyo.
“Tunatarajia matokeo yote yafike kituo cha taifa cha kujumlishia matokeo kufikia saa sita mchana kesho.”
Wafanyakazi wa kuchuma majani ya cha eneo la Kericho, kusini mwa Bonde la Ufa nchini Kenya wamerejea kazini katika mashamba ya kampuni ya Unilever. Walikuwa wamepewa rasmi siku moja kupumzika siku ya uchaguzi Jumanne.
BBC
BBC
Kiongozi wa waandalizi wa uchaguzi wa Umoja wa Afrika (AU) Thabo Mbeki amesema hawawezi kuzungumzia madai ya upinzani kwamba mitambo ya IEBC ilidukuliwa.
Kiongozi huyo mstaafu wa Afrika Kusini amesema jukumu la waangalzii ni kuangalia shughuli ya uchaguzi inavyofanyika.
"Sisi si wachunguzi wa uchaguzi," amesema.
Iwapo tungeona kitu kikifanywa vibaya, kinyume na sheria za Kenya na viwango vya AU, tungeingilia kati.
Katika baadhi ya visa, NASA wamewasilisha malalamiko kwetu kuhusu uchaguzi, mfano kupatikana kwa sajili ya wapiga kura na usalama pia - mfano kusafirishwa kwa maafisa takriban 40 wa polisi kwenda kwingine.
Tuliangazia haya, na baadhi tukawapasha IEBC kuhusu malalamisho ya sajili na kuhusu polisi tukawasiliana na kukutana na waziri wa usalama Dkt Fred Matiang'i.









No comments:
Post a Comment