Naibu Waziri wa
Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Eng. Edwin Ngonyani, akisalimia wananchi wa
kata ya Chilonwa, wilayani Chamwino mkoani Dodoma alipotembelea wilayani hapo ljana,
ikiwa ni kutekeleza ahadi yake ya kukagua daraja la Chilonwa kwa Mbunge wa jimbo la Chilonwa, Mhe.
Joel Makanyaga.
Mbunge wa jimbo la Chilonwa, Mhe. Joel Makanyaga, akifafanua jambo kwa Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Eng. Edwin Ngonyani (kushoto kwa Mbunge), alipofika jimboni hapo kukagua daraja la Chilonwa, wilayani Chamwino mkoani Dodoma jana.
Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Eng. Edwin Ngonyani, akizungumza na wananchi wa kata ya Chilonwa, wilayani Chamwino mkoani Dodoma jana mara baada ya kukagua daraja la Chilonwa lililopo mkoani humo.
Muonekano wa Daraja la
Chilonwa lililopo kata ya Chilonwa, wilayani Chamwino mkoani Dodoma. Daraja
hilo ni kiungo kati ya mkoa wa Dodoma, Manyara na Arusha.
Sehemu ya daraja la Chilonwa iliyoathirika kutokana na shughuli za kibinaadamu kama vile kilimo na hivyo kupelekea kwa daraja hilo kufukiwa na mchanga na kuwa fupi.
WANANCHI wa kata ya
Chilonwa, wilaya Chamwino mkoani Dodoma wameiomba Serikali kuchukua hatua za
haraka kujenga daraja la Chilonwa lililopo katika kata hiyo ili kutatua
kero ya usafiri kwa wananchi hao na maeneo jirani hususan katika
kipindi cha masika.
Wakieleza kero yao kwa Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Eng. Edwin Ngonyani, wananchi hao wamesema wanaamini kuwa ujio wa Naibu Waziri huyo katika kata yao kutaleta ufumbuzi wa kero hiyo.
"Tunaamini sasa tutapata mwarobaini wa daraja hili kwani tatizo hili ni la muda mrefu, siku hadi siku daraja linakuwa fupi kutokana na kufukiwa na mchanga na hivyo hupelekea maji kujaa darajani hapa kipindi cha masika na watu kushindwa kuvuka", amesema mmoja wa wananchi hao.
Aidha, wananchi hao
wamemwomba Naibu Waziri huyo kurekebisha daraja hilo kwa kulijenga juu zaidi
ili kupitisha maji na kupitika katika vipindi vyote vya mwaka kutokana na
kwamba lililopo sasa lipo chini zaidi mara baada ya kufukiwa na mchanga.
Wananchi hao wameeleza
masikitiko yao kwa Naibu Waziri huyo hususan katika kipindi cha masika ambapo wamesema
hutumia kiasi cha shilingi elfu kumi kuvushwa kutoka sehemu moja kwenda
nyingine na wengine hupoteza maisha wakiwa wanavuka.
Sambamba na hilo
wananchi hao wamependekeza kuwa ujenzi wa daraja hilo uhusishe wataalamu
waliobobea na ambao watahakikisha daraja hilo linakamilika mapema na kwa
viwango.
Kwa upande wake Naibu
Waziri Ngonyani, amewataka wananchi hao kuacha tabia ya kufanya shughuli za
kibinaadamu kama kilimo katika njia ya mto kwani hali hiyo hupelekea udongo
kumung’unyuka na hatimaye mchanga kufunika daraja.
Amemtaka Mbunge wa
jimbo la Chilonwa, Mhe. Joel Makanyaga, kwa kushirikiana na viongozi wa kata na
kijiji kuhamasisha wananchi kuacha kufanya shughuli za kibinaadamu kando ya
mto.
Amefafanua kuwa Wizara
yake kupitia Wakala wa Barabara (TANROADS), mkoani Dodoma itahakikisha kwanza ina utengeneza mto
huo kwa kuelekeza maji yote katika mto.
Naye, Mbunge wa jimbo
la Chilonwa, Mhe. Joel Makanyaga, amempongeza Naibu Waziri huyo kwa kutembelea
jimboni hapo na kuahidi kuwasimamia wananchi wake katika kulinda miundombinu
hiyo.
Naibu Waziri Ngonyani
leo ametembelea na kukagua Daraja la Chilonwa, wilayani Chamwino mkoani Dodoma
ikiwa ni kutekeleza ahadi yake ya kutembelea na kukagua daraja hilo kwa Mbunge
wa jimbo la Chilonwa, Mhe. Joel Makanyaga.
Imetolewa
na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano.

No comments:
Post a Comment