Meneja
wa Wakala wa Barabara Nchini (TANROADS). Mkoa wa Lindi, Eng. Issack Mwanawima
(mwenye koti la draft), akimweleza Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano,
Profesa Makame Mbarawa (kushoto), hatua iliyofikiwa katika ujenzi wa maegesho
hayo, Mkoani humo, wakati Waziri huyo alipotembelea mradi huo hivi karibuni.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa (kulia), akiangalia ujenzi wa wa maegesho ya kivuko unaojengwa katika mkoa wa Lindi alipotembelea mradi huo hivi karibuni. Mradi huo utahusisha maegesho ya kivuko na ujenzi wa mita 150 za barabara ya lami upande wa Kitunda.
Tinga Tinga likiendelea na ujenzi wa maegesho ya kivuko Mkoani lindi. Ujenzi wa maegesho hayo unatarajiwa kukamilika mwezi Novemba mwaka huu.
Meneja wa Bandari ya Mtwara, Eng. Juma Kijavara (katikati),
akimuonesha Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa
(kushoto), eneo la gati ya Lindi ambalo litatakiwa kuchimbwa ili kuongeza kina
cha gati hilo, alipotembelea gati hiyo hivi karibuni.
Meneja wa Bandari ya Mtwara, Eng. Juma Kijavara (katikati), akifafanua jambo kwa Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa (kushoto), wakati Waziri huyo alipotembea alipotembelea gati la Lindi kuona hatua mbalimbali za utekelezaji wa upanuzi wa gati hiyo hivi karibuni.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa (kushoto), akienda kuangali sehemu ya kwanza ya upanuzi wa gati la Lindi ambalo kwa sasa linatakiwa kuongezewa kina ili meli kubwa ziweze kutia nanga.
SERIKALI imesema ujenzi wa maegesho ya kivuko Mkoani Lindi
utakamilika mwezi Novemba mwaka huu ili kurahisisha usafirishaji wa abiria na
mizigo kwa wakazi wa eneo la Kitunda Mkoani Lindi.
Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Ujenzi,Uchukuzi na Mawasiliano,
Profesa Makame Mbarawa alipokagua maendeleo ya ujenzi wa maegesho hayo na kusema ujenzi huo
umegharimu kiasi cha Tsh, bilioni 1.8 ambazo zitahusisha maegesho ya Kivuko na
kujenga barabara ya kiwango cha lami mita 150 upande wa Kitunda Mkoani Lindi.
‘Tuliahidi na sasa tunatekeleza, nimefurahi kuona ujenzi
unaendelea vizuri na ninawahakikishia mwezi Novemba tutakuja kuzindua kivuko’ alisema
WazirI Profesa Mbarawa.
Aidha, Waziri Mbarawa amemtaka Mkandarasi anaejenga magesho hayo
kuzingatia thamani ya fedha wakati wa ujenzi wake ili mradi huo uweze kudumu
kwa muda mrefu.
"Hakikisha unajenga maegesho haya kwa kuzingatia viwango
tulivyokubaliana, hatutaki kuona kasoro mara tu baada ya mwezi mmoja, hizi ni
fedha za walipa kodi na tunategemea miundombinu hii ikae muda mrefu," alisisitiza Waziri Prof. Mbarawa.
Kwa upande wake Msimamizi wa Mradi huo, Meneja wa Wakala wa Barabara
nchini (Tanroads), mkoa wa Lindi, Eng. Issack Mwanawima amemuhakikishia Waziri
Profesa Mbarawa kuwa watasimamia mradi kwa kuzingatia viwango katika ujenzi huo
na kuhakikisha unakamilika kama mkataba unavyosema.
Katika hatua nyingine Waziri Profesa Mbarawa amekagua maendeleo ya
ujenzi wa Gati la Lindi na kusema kuwa Serikali imetenga fedha kwa ajili ya
kuongeza kina cha Gati hiyo mara baada ya kutokea changamoto ya upana wa Gati hiyo
kuwa mdogo.
‘Baada ya kujenga sehemu iliyopo sasa tuligundua kuwa bandari
inatakiwa kuongezwa kina hivyo tukalazimika kufanya usanifu upya ili tuongeze
upana wa mita 60 mpaka 500kwa eneo lote vinginevyo meli zisingeweza kufunga
nanga’ alisisita Waziri Prof Mbarawa.
Waziri Prof. MBARAWA aliongeza kuwa lengo la Serikali katika
kufanya usanifu upya ni kuhakikisha Gati ya Lindi inakidhi
mahitaji halisi na kuchochea uchumi wa mkoa huo.
Kwa upande Meneja Bandari ya Mtwara Eng. JUMA Kijavara amesema
Mamlaka ya Bandari Nchini TPA imejipanga na iko katika hatua za mwisho za
mazungumzo na Mkanadarasi ili aanze kazi hiyo.
Mradi wa upanuzi wa Gati la Lindi utahusisha miradi ya Gati hiyo,
Bandari ya Lushungi pamoja na bandari ya Kilwa.
Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi,
Uchukuzi na Mawasiliano.






No comments:
Post a Comment