KATIKA kuendeleza huduma zake kwa jamii, Taasisi ya MO Dewji imeungana kwa pamoja na Taasisi ya Tulia Trust inayomilikiwa na Naibu Spika wa Bunge la Tanzania, Dk. Tulia Ackson kujenga vyoo katika Hospitali ya Rungwe iliyopo mkoani Mbeya. Akizungumza kuhusu ushirikiano huo katika mashindano ya kukimbia ya Tulia Marathon, Mratibu Miradi wa Taasisi wa MO Dewji, Catherine Decker amesema taasisi yao imeamua kushirikiana na Dk. Tulia ili kusaidia kuboresha sekta ya afya ya nchini ambayo kwa sasa bado inakabiliwa na changamoto nyingi.
Catherine alisema Taasisi ya MO Dewji imejikita zaidi katika kusaidia sekta ya elimu, afya na huduma za kijamii na hivyo ushirikiano na Tulia Trust ni mzuri kwao na umekuja ikiwa ni miezi miwili imepita tangu walipotoa msaada mwingine katika wodi ya wanawake katika Hospitali ya SekouToure iliyopo Mwanza na kama taasisi wana miradi nyingi wamepanga kuifanya ili kuunga mkono juhudi za serikali ya awamu ya tano.
Mratibu Miradi wa Taasisi wa MO Dewji, Catherine Decker akizungumza kuhusu ushirikiano wa MO Dewji Foundation na Tulia Trust kujenga vyoo katika wodi ya wanawake katika Hospitali ya Rungwe.Kwa upande wa Naibu Spika wa Bunge la Tanzania na mwanzilishi wa Taasisi ya Tulia Trust, Dk. Tulia Ackson aliishukuru Taasisi ya Mo Dewji kwa udhamini huo ambao umeambatana na mashindano ya kukimbia ya Tulia Marathon na malengo ya kuanzisha mashindano hayo ni kukusanya pesa ili kusaidia kuboresha sekta ya elimu na afya.
Naibu Spika wa Bunge la Tanzania na mwanzilishi wa Taasisi ya Tulia Trust, Dk. Tulia Ackson akizungumza kuhusu ushirikiano wa MO Dewji Foundation na Tulia Trust kujenga vyoo katika wodi ya wanawake katika Hospitali ya Rungwe.

No comments:
Post a Comment