Na
Daudi Manongi-Maelezo
SERIKALI
kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu, Vijana, Ajira na Watu Wenye Ulemavu kwa
kushirikiana na Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi – VETA wanaendesha
mpango wa kutathmini na kurasimisha ujuzi uliopatikana nje ya Mfumo rasmi wa
Mafunzo.
Kwa mujibu wa Taarifa
ya Katibu Mkuu wa Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Eric Shitindi, imesema
kuwa mpango huo unatoa fursa ya kufanyiwa tathmini ya ujuzi, kupewa mafunzo,
kuziba upungufu na kisha kutunukiwa cheti.
Taarifa hiyo inaeleza kuwa sifa za
mwombaji wa mafunzo hayo ni pamoja na uzoefu usiopungua miaka mitano na umri
usiozidi miaka 45.
Aidha taarifa hiyo imeeleza kuwa fani
mbalimbali zitakazohusika ni Uashi, Useremala, Ufundi Magari (makenika),
upishi, uhudumu wa hoteli, Bar na Migahawa.
Ili kufanya maombi waombaji wanatakiwa
kufika katika ofisi ya Mkurugenzi wa Manispaa, Mji au Wilaya iliyoko karibu ili
kuchukua fomu za kujaza maombi bila malipo yeyote na maombi hayo kuwasilishwa
kuanzia tarehe 5 hadi 25 Januari 2017.
Taarifa hiyo imeongeza kuwa mchakato
wote wa tathmini na urasimishaji wa ujuzi utagharamiwa na Serikali na pia
watakaokidhi sifa, vigezo na masharti watajulishwa kwa ajili ya usaili kuanzia
Tarehe 10 Februari 2017.


No comments:
Post a Comment