Na Daudi Manongi - Maelezo
RAIS wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli amewataka Wakuu wa
Mikoa,Wilaya na Wakurugenzi wa Halmashauri kuondoa utitiri wa kodi uliopo
kwenye Mazao ili wakulima waweze kunufaika kutokana na kujiongezea kipato.
Agizo hilo
alimetolewa leo wakati akihutubia wakazi wa Wilaya ya Bukoba na Watanzania kwa ujumla
akiwa katika ziara ya kikazi ya siku mbili Mkoani Kagera.
“Nawaagiza Wakuu wa
Mikoa,Wilaya pamoja na Wakurugenzi wa Halmashauri kupitia upya Kodi zilizopo
katika bidhaa mbalimbali kama Kahawa na Pamba, hakikisheni mnaondoa utitiri huu
wa Kodi ili wafanyabiashara hawa wafaidike na mazao yao,” Alisema Rais
Magufuli.
Aidha Rais Magufuli
amewaahidi Watanzania kuwa atahakikisha anafanya kazi usiku na mchana bila
kujali itikadi, dini na makabila ili kuhakikisha nchi inasonga mbele katika nyanja
zote za kimaendeleo.
Akizungumzia maendeleo
ya michango mbalimbali kwa ajili ya wathirika wa tetemeko la Ardhi mkoani
Kagera Rais Magufuli amesema kuwa mpaka sasa simenti iliyochangwa ni zaidi ya
tani 30,600 na mabati zaidi ya elfu 31,000 ambapo wananchi wameshaanza kupewa
na kujengea.
Amewahimiza wananchi
walioathirika na tetemeko la Ardhi kutotegemea Serikali kuwafanyia kila kitu na
badala yake waanze kujenga na watumie msimu huu wa mvua kulima ili kujipatia
chakula.
Pia Rais Magufuli
amewashukuru na kuwapongeza wahisani waliochangia Maafa ya Kagera na kuwataka
kuendelea na moyo huo katika kulijenga Taifa letu.


No comments:
Post a Comment