Mwanasiasa mkongwe, Waziri mstaafu katika Serikali Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Seif Khatib
Na Judith Mhina - Maelezo
KATIKA kuadhimisha miaka 53 ya Mapinduzi ya Zanzibar Idara ya
Habari - MAELEZO ilipata fursa ya kufanya mahojiano na Mwanasiasa Mkongwe,
Waziri Mstaafu katika Serikali ya Awamu ya Kwanza, Pili, Tatu na ya Nne ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mtaalamu wa Lugha ya Kiswahili Dkt. Mohammed
Seif Khatib kuhusiana na maadhimisho hayo. Yafuatayo ni maswali na majibu katika
mahojiano hayo:
SWALI: Zanzibar imetimiza miaka 53 ya Mapinduzi
ni jambo gani muhimu la kuwaeleza Wazanzibar?
JIBU:
Kwa lugha fupi nasema “Mapinduzi Daima” Mapinduzi yaliyofanywa
mwaka 1964 yanahitaji kuendelezwa kwa sababu yamesaidia ukombozi wa Waafrika,
yameondoa utawala wa Uingereza na Waarabu. Madhila ya Zanzibar hayawagusi
Waafrika wa Zanzibar peke yake, bali pia Waafrika wa Tanzania Bara. Mapinduzi hayo yalikusudia kuondoa madhila
hayo, yaani utumwa, masuria kufanyishwa kazi, kuteswa kudhalilishwa kunyanyaswa kudharauliwa na
kuuzwa kama samaki. “Mapinduzi Daima” maana yake ni endelea kutekeleza yale
yaliyokusudiwa na “Mapinduzi” yaani kupata huduma bora za afya, elimu, maji,
Umeme na makazi bora
SWALI:
Mheshimiwa Mohammed Seif Khatib wewe ni kati ya watu wachache
waliobobea katika siasa na umeitumikia Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar,
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Unadhani muelekeo uliopo mpaka sasa unaleta hali halisi ya matarajio ya
Mapinduzi yaliyofanyika mwaka 1964?
JIBU
Muelekeo upo kwa maana ya “Ndio au Hapana” kwa sababu miisingi
ya Mapinduzi Zanzibar ni kubadilisha hali ya Wazanzibar wanyonge waliowemgi katika maeneo
ya elimu, afya, maji umeme na makazi bora ambapo Rais wa Kwanza wa Zanzibar na
Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Hayati
Shekh Abeid Amani Karume aliltimiza lengo.
Sababu za kiuchumi Zanzibar ni kisiwa na kina eneo dogo sana
la kuwekeza kwenye sekta mbalimbali za uzalishaji na sekta ambayo ni kubwa ya uvuvi
haijaendelezwa kwa sababu wananchi wana zana
duni za uvuvi.
Mara baada ya Mapinduzi uchumi wa Karafuu ulikuwa mzuri na
bei katika soko la dunia ilikuwa kubwa. Idadi ya watu wakati wa Mapinduzi ilikuwa
laki tatu na nusu, karafuu ilikuwa na bei nzuri sana kwenye soko la dunia sasa imeshuka
sana bei duniani na Idadi ya watu imeoongezeka mpaka milioni moja na nusu, hii
ina maana tunatakiwa kuzalisha mara sita zaidi ya tulivyokuwa tunazalisha 1964.
Sekta ya ujenzi inaongeza majengo makubwa makubwa na eneo la
Zanzibar haliongezeki. Hivyo kwa sasa inatubidi kunoa bongo zaidi kuwa na
viwanda ambavyo havihitaji maeneo
makubwa ili kujenga uchumi wetu.
Utamaduni wa waswahili wa kutegemea babu, bibi, shangazi,
mjomba, baba mdogo na mambo kama hayo, pia tabia ya Wazanzibar kuchagua kazi za
kufanya na kutotambua kazi ndio msingi
wa maendeleo inadhoofisha uchumi wa
Zanzabar.
Dhamira ya Serikali ya kusaidia elimu bure maji bure,
wafadhili wanasema hapana hatutatoa msaada kama hamtozi fedha kwenye huduma
tunazowachangia. Mfano Wajapani walisimamia mradi wa maji Serikali iliposema
itatoa maji bure mfadhili alikataa kwa hiyo serikali ikabidi ifate masharti
lakini wananchi hawana uwezo.
SWALI: NIni maoni yako kuhusu Serikali ya Mapinduzi
ya Zanziibar kuelekea kwenye uchumi wa viwanda vidogo, vyakati na vikubwa?
JIBU:
Baada ya Mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1964, Serikali
ilianzisha viwanda vya Sigara, Manukato, Kiwanda cha viatu, Ngozi, sabuni,
chuma na Nguo. Viwanda hivi vilikufa kwa sababu havikustahili kuwepo Zanzibar.
Mfano ni lazima uwe na uhakika wa upatikanaji wa malighafi, mali ghafi nyingi zilitoka
Bara gharama ya kusafirisha mpaka Zanzibar iliongeza gharama ya uzalishaji. Uanzishwaji
wa soko huria uliviua viwanda vya ndani kwa kuwa bidhaa zitokazo nje ziliuzwa kwa bei rahisi ukilinganisha na za Zanzibar.
Ushauri wangu Zanzaibar iwe na kiwanda cha kuchakata na
kusindika samaki, kiwanda cha matunda pia kitakuwa cha muda maana miaka 20
ijayo hakutakuwa na eneo la kulima matunda wala karafuu hapa Zanzibar. Maana maendeleo
yanafanya majengo makubwa kujengwa zaidi na ardhi ni ileile haiongezeki hali
hii itafanya ukulima upungue.
Mimi nadhani mambo ambayo Zanzibar wanaweza kufanya ni mambo
matatu: “Mosi viwanda vya samaki Pili,
utalii wa utamaduni na wa kutembelea maeneo ya
kihistoria na Tatu Utalii wa matibabu, yaani kujenga hospitali inayojitosheleza
kwa vifaa na madaktari, wakati watalii wakija Zanzibar kwa matembezi ya maeneo ya kihistoria
na utamaduni, anapata nafasi ya kupewa matibabu. Utalii huu ni maarufu sana nchi
za Urusi na China.
Pia kwa vijana wa Zanzibar wapewe maeneo ya ardhi Tanzania Bara
waweze kulima na kuzalisha chakula ambacho kitapelekwa Zanzibar. Zoezi hili litatoa
nafasi ya vijana kujifunza na kuwa na tabia ya kujituma na kupenda kazi.
SWALI Rais kwa kwanza wa Zanzibar Hayati
Shekh Abeid Amani Karume ni kati ya
Marais wachache wa Afrika ambao walijitolea kuhakikisha kila mwananchi anaishi
kwenye makazi bora nini maoni yako kuhusu suala hili?
JIBU;
Shekhe Karume, aliweka msingi huo kwa sababu kulikuwa na
kambi tatu.
Kwanza Mji Mkongwe kwa Wazungu, Waarabu, Wahindi ambao ni Watawala, Matajiri na
Wafanyabiashara.
Pili, Ng’ambu waliishi Waswahili Matopasi, Makuli, Wapishi - kazi
yao kuhudumia wakazi wa Mji Mkongwe
Tatu, Shamba kazi yao ilikuwa kulima eneo hili waliishi Waafrika masikini sana, kazi yao ni kuzalisha
mazao mbalimbali kwa ajili ya kulisha wakazi
wa Mji Mkongwe. Nyumba za Waafrika hawa zilikuwa
za matope, nyasi ni vibanda vibanda vibovu
tu.
Hivyo, mara baada ya
Mapinduzi Rais Karume aliona lazima abadilishe hali ya maisha ya watu waliokuwa
wanaishi katika umaskini uliokidhiri ndio akajenga nyuma za makazi bora Unguja
na Pemba.
SWALI: Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inalipi
la kujivunia kutokana na miaka 53 ya Mapinduzi Tukufu ya Zanzibar?
Lipo la kujivunia ambalo ni mpaka leo Mapinduzi yanakumbukwa
naona fahari sana kwa hilo. Kama sio Mapinduzi mpaka kesho Sultani angeendelea
kutawala kama sio yeye mwanae au mjukuu wake.
Pili, wakati wa sherehe hizi za Mapinduzi miradi na mipango
mbalimbali ya maendeleo inazinduliwa. Hii
inaendeleza dhamira ileile ya Mapinduzi yaliyokusudiwa
mwaka 1964.
SWALI: Suala la Nidhamu kwa Watumishi wa
Umma, Taasisi, Mashirika na Idara za Serikali linatiliwa mkazo sana na Rais wa
Zazibar Mheshimiwa Dkt. Ali Mohammed Shein hili unalizungumziaje?
Suala gumu kidogo maana sina takwimu. Hili ni tatizo kubwa
sana Zanzibar, Wazanzibar wengi hawajali kazi hawaoni kama maisha yao
wanategemea kazi mpaka imekuwa sehemu ya utamaduni wa Wazanzibar. Hivyo lazima
mfumo mzima ubadilike na kuona watu wana wajibu wa kazi. Nadhani Rais anahitaji
kuungwa mkono kwa hili maana akiachiwa mwenyewe hataliweza ni lazima
tulichukulie kwa mtazamo wa pamoja ili kuijenga Zanzibar.
Zanzibar ni ndogo sana na desturi ya Wazanzibar kila siku
watu wapo mazikoni harusini kwa shangazi, kwa dada nyakati za kazi huwezi
kuamini lakini hayo ndio maisha ya kawaida ya Wazanzibar.
SWALI: Miaka 53 ya Mapinduzi hali ya kisiasa
ikoje Zanzibar?
JIBU:
Hali ya siasa sio nzuri sana inaviza maendeleo ya Wazanzibar,
hali hii hujitokeza katika kipindi maalum wakati wa uandikishaji wapiga kura,
uchaguzi na mara baada ya uchaguzi.
Zanzibar kuna upinzani wa hujuma na vitisho kwa kambi zote mbili
za vyama viwili vikubwa vya siasa katika kipindi hicho maalum wakati wa kujiandikisha
kupiga kura wakati wa kupiga kura na baada ya kura, ikipita kipindi hicho nchi
inatulia na kuwa salama.
SWALI:
Nini maoni yako kuhusu Mgogoro huo wa kisiasa?
JIBU:
Ni gumu sana chimbuko lake ni viongozi wa Chama cha Mapinduzi
- CCM na Chama cha Wananchi - CUF lakini siku viongozi wa Zanzibar wakubwa
katika Kambi mbili wataamua kukaa pamoja na kulitatua, litatatuliwa viongozi hao
wakubwa wa CUF na CCM wakikaa na kuamua
itakuwa.
SWALI: Unadhani kwa nini vyama vya siasa vya
Upinzani vinalalamika kuwa Demokrasia inakandamizwa Zanzibar?
JIBU:
Nadhani tabia au hulka ya nchi za Afrika za kupinga kila kitu
wakati wa uchaguzi ili mradi upande wake umeshindwa.
SWALI: Una wito gani kwa Wanzanzibar na
Watanzania kwa ujumla?
JIBU:
Kuna haja ya kujenga makumbusho ya kisasa ili kizazi cha sasa
na cha baadaye waone na kujua nini
kilitokea kwa nini tunasheherekea Mapinduzi na kwa nini tuko huru sasa. Ni vema
kuonyesha katika picha, maandishi na sura halisi historia ya Zanzibar kabla ya
Waajemi, Wareno, Waarabu, Waingereza na sasa Serikali ya Mapinduzi.
Vijana wengi ukiwaambia nchi hii kulikuwa na unyanyasaji wa Waafrika
hawakubali maana hawajiu historia waelezwe kwa nini tuko huru, kuna wasioitakia
mema Zanzibar wanapotosha historia hiyo.
Lazima watu wajue watu walitoka Kongo, Malawi, Kigoma na
Tabora wakibebeshwa pembe za Ndovu au Tembo na kusafiri mpaka Bagamoyo,
kusafirishwa na boti mpaka visiwani na kuwekwa sokoni kuuzwa kama samaki katika
soko la watumwa. Lazima wajue hiyo sio hadith ya kufikirika ni kweli.
Aidha, wengine wakifanyishwa kazi za suluba, masuria, matopasi
na kuitwa watumwa maana wametoka Bara. Hivyo
sherehe hizi zinatuhusu wote Watanzania wa Bara na Visiwani.


No comments:
Post a Comment