Na Habari - Maelezo
WAZIRI wa Kilimo, Mifugo na
Uvuvi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Mwenyekiti wa Chama cha Siasa cha
Alliance for Democraytic Party – ADC, Hamad Rashid Mohamed amesema, Vyama vya
Upinzani vina nafasi kubwa katika kuishauri Serikali inayoongozwa na Rais Dkt.
Ali Mohamed Shein katika masuala ya maendeleo visiwani Zanzibar.
Waziri Hamad Rashid Mohamed
amesema hayo alipohojiwa na Idara ya Habari (Maelezo) leo kuhusiana na
mafanikio yaliyopatikana tangu mapinduzi ya Zanzibar yalipofanyika miaka 53
iliyopita. Amesema, Dkt. Shein amekuwa akivitaka Vyama vya Upindani Visiwani
Zanzibar kushiriki katika masuala ya maendeleo kwa njia mbalimbali. Alitolea
mfano, yeye kabla ya kuteuliwa kuwa Waziri, Chama chake cha ADC kwa
kushirikiana na Wananchi wamejenga uwanja wa mpira wa Gombani, Pemba kwa msaada
kutoka Serikali ya Korea.
Waziri huyo pekee kutoka
Chama cha Upinzani amewabeza Wanasiasa wanaodai kuwa Dkt. Shein hatoi nafasi
kwa Vyama vingine katika kutoa michango yake katika masuala ya maendeleo. “Mimi
mwenyewe nimepewa dhamana ya Uwaziri kupitia chama changu cha ADC na katika
vikao tunavyokaa kila mtu anatoa mawazo yake kuhusiana na masuala ya maendeleo
ya Zanzibar na kama hoja unayotoa ni ya msingi lazima itakubalika. Inapofikia
suala la maendeleo Dkt. Shein haangalii Chama, anaangalia maslahi ya Zanzibar
kwanza.”
Akizungumizia maadhimisho
ya miaka 53 ya Maapinduzi ya Zanzibar Waziri Hamad amesema, Wazanzibar na
Watanzania kwa ujumla wana kila sababu ya kuenzi Mapinduzi hayo ambayo yalikuwa
chachu cha Muungano wa Tanganyika na Zanzibar. Muungano wetu ulizingatia uwepo
wa umoja kwani Serikali ya Kikoloni ilipandikiza mbegu ya kubaguana hata Waafrika
kwa Waafrika wenyewe.
Alifafanua kuwa, mapinduzi
hayo yaliifanya nchi iwe huru zaidi na Wananchi wake waishi kwa amani, umoja na
mshikamano. Chini ya uongozi wa Rais wa Awamu ya kwanza wa Zanzibar marehemu
Sheikh Abeid Aman Karume, Zanzibar ilipata maendeleo makubwa ambapo zilijengwa
nyumba bora za makazi za Wananchi, elimu ilitolewa bure, huduma za afya, maji
na hivyo kufuta kabisa aina zote za ubaguzi uliokuwa umeota mizizi kabla ya
mapinduzi.
Akijibu swali kuhusiana na
masimamo Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Dkt. John Pombe Magufuli juu
ya mageuzi ya kuekelea kwenye uchumi wa Viwanda amesema, kukua kwa uchumi ndio
kigezo cha maendeleo katika Taifa lolote duniani. “Rais anaposema anataka Taifa
liondokane na umasikini inawezekana iwapo tutakuwa na viwanda vidogo vidogo,
vya kati na vikubwa.
Ameeleza kuwa, kutokana na
viwanda Watu watapata ajira, Wakulima watapata soko la uhakika la mazao
wanayozalisha na bidhaa zitakazozalishwa zitauzwa ndani na nje ya nchi kwa kuwa
zimeongezwa thamani. Hivyo katika kufikia malengo hayo lazima tukubali mageuzi
hayo na Wananchi lazima wafanye kazi.
Mwisho alimalizia kwa kutoa
wito wa Zanzibar lazima iwe salama na ibaki salama kwa kusisitiza nchi ni
lazima iwe na Amani, Mshikamano na Utulivu. Inapotetereka ni vema kushirikisha
viongozi wa dini na Wazee wenye busara ili kutanzua matatizokuliko amani
kutoweka. kwa Wazanzibar, kila mmoja ajiiulize ameifanyia nini Zanzibar ili
kuleta maendeleo.
Kwa wanasiasa alitoa wito
kwa kusema njia za kurekebisha makosa zipo kukubali kukaa chini na kuzungumza
kutoa lawana sio suluhisho. Vyama vya siasa vishiriki kikamilifu katika
utekelezaji wa maendeleo ya Zanzibar.


No comments:
Post a Comment