Na Frank Shija – Maelezo
07/12/2016
WATANZANIA watakiwa kuunga mkono jitihada za Serikali ya Awamu ya Tano katika Kukuza Uchumi kwa kujiunga pamoja na kuanzisha Viwanda vidogo vidogo na vya kati.
Rai hiyo imetolewa leo na Mkuu wa Wilaya ya Pangani Bi. Zainab Abdallah alipokuwa akifanya mahojiano maalum na mwandishi wa habari hii kuhusu maadhimisho ya miaka 55 ya Uhuru wa Tanzania.
Akizungumzia kauli mbiu ya maadhimisho hayo amesema kuwa inasadifu kile ambacho Serikali imedhamiria kukifanya matharani suala zima la kuifanya Tanzania kuwa nchi ya viwanda kitu ambacho kimeanza kutekelezwa.
“Watanzania wanapaswa kuunga mkono jitihada za Serikali kwa kutekeleza uanzishwaji wa Viwanda vidogo vidogo na vya kati kwani kufanya hivyo kutapunguza ama kuondoa kabisa tatizo la ajira kwa vijana,” alisema Bi. Zainab.
Aliongeza watanzania wanapaswa kushirikiana kwa pamoja katika kuijenga Tanzania ya Viwanda ili kuongeza uzalishaji wa bidhaa za ndani na kuongeza fursa ya ajira kwani viwanda ni eneo linalotoa ajira nyingi kwa wakati mmoja.
Aidha Mkuu huyo wa Wilaya amempongeza Rais Magufuli kwa hatua kadha alizokwishachukua katika kuhakikisha anaweka mazingira rafiki kwa wawekezaji katika sekta ya viwanda akitolea mfano wa hatua ya Kampuni ya Bakhresa kupewa eneo la ekari elfu kumi kwa ajili ya kujenga kiwanda cha kusindika matunda.
Desemba 9 kila mwaka Tanzania imekuwa ikiadhimisha siku ya Uhuru wa Tanzania Bara ambapo kwa mwaka huu kitaifa yatafanyika Dar es salaam na kauli ya mwaka huu ni “Tuunge Mkono Jitihada za Kupinga Rushwa na Ufisadi na Kuhimarisha Uchumi wa Viwanda kwa Maendeleo ya Nchi Yetu.”
No comments:
Post a Comment