Afisa Uendeshaji wa Mfuko wa Pensheni kwa
Watumishi wa Umma (PSPF) Bw. Hadji Jamadar akielezea jambo kwa wateja
waliotembelea banda la mfuko huo katika maonesho ya Viwanda yanayoendelea
katika viwanja vya Sabasaba Jijini Dar es Salaam.
Na Jacquiline Mrisho
MFUKO wa Pensheni kwa Watumishi
wa Umma (PSPF) umetoa rai kwa wajasiriamali kujiunga na mpango wa uchangiaji wa
hiari ili kuweza kupata huduma ya hifadhi ya jamii.
Rai hiyo imetolewa leo Jijini
Dar es Salaam na Afisa Uendeshaji wa mfuko huo, Hadji Jamadary wakati wa
uzinduzi wa maonesho ya kwanza ya viwanda vya Tanzania uliofanyika katika
viwanja vya sabasaba jijini humo.
Jamadary amesema kuwa mpango
huo utawawezesha wananchi wasio na ajira rasmi kupata fursa ya huduma ya
hifadhi ya jamii kama wapatavyo wanachama wenye ajira rasmi pia
unawawezesha wanachama walio katika mfuko huo kuweza kujiwekea akiba ya ziada.
“Mpango huu wa hiari ni mfuko
ulio huru ambao unamruhusu mwananchi yoyote mwenye umri kuanzia miaka 18,
mwenye uraia wowote hata kama anafanya kazi ndani au nje ya nchi, hivyo
tunawaomba wananchi wote kuchangamkia fursa hii kwa manufaa ya maisha yao ya
baadae,”alisema Jamadary.
Ameongeza kuwa hadi sasa mfuko
una jumla ya wananchi 98,733 ambao tayari wamejiunga na mfuko huo lakini kwa
kutambua umuhimu wa mfuko huo zaidi ya wananchi 102 wameshajiunga wakati
maonyesho hayo yanayotarajiwa kumalizika mnamo Disemba 11 mwaka huu
yakiendelea.
Aidha, Afisa huyo ametaja jumla
ya mafao 6 yaliyopo katika mfuko huo yakiwemo ya elimu, ujasiriamali, uzee,
kifo, ugonjwa au ulemavu, matibabu na fao la kujitoa pia mfuko huo unatoa fursa
kwa mwanachama kukopa nyumba na viwanja.
Kuhusiana na fao la matibabu,
Jamadary amefafanua kuwa mwanachama atapatiwa bima ya afya yenye gharama
ya shilingi 76,800 kwa mwaka mzima pia ataruhusiwa kuwaingiza wategemezi watano
ambapo kila mmoja atalipiwa kiasi hicho cha fedha kwa mwaka mmoja.
Mpango wa hiari umeanzishwa
mwaka 2013 ukiwa na lengo la kupanua wigo wa uanachama kwa kuandikisha wananchi
waliojiajiri au kuajiriwa katika sekta rasmi au isiyo rasmi.
No comments:
Post a Comment