TANGAZO


Saturday, December 3, 2016

BALOZI SEIF IDDI AZINDUA KAMBI YA UCHUNGUZI WA AFYA ZA WANANCHI KITUO CHA AFYA CHA MAHONDA ZANZIBAR

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi akikata utepe kuashiria kuzindua Kambi ya uchunguzi wa Afya  katika Kituo cha Afya Mahonda chini ya Watalaamu kutoka Jumuiya ya Kimataifa ya Baps Charities. Kushoto ya Balozi Seif Ali Iddi  ni Muweka Hazina wa Jmuiya ya Baps Charities Bwana Kapil Dave. (Picha zote na Hassan Issa – OMPR – ZNZ) 
Daktari dhamana ambaye pia ni Mkuu wa Kitengo cha Macho Hospitali Kuu ya Mnazi Mmoja Dr. Slim Mo’h Mgeni wa kwanza kutoka Kulia akimpatia maelezo Balozi Seif anayeshuhudia uchunguzi wa Macho katika Kambi ya afya iliyowekwa Kituo cha Afya Mahonda. 
Balozi Seif akimvisha Miwani Mmoja wa wananchi baada ya kumaliza kufanyiwa uchunguzi wa Afya na kubainika anahitaji kuwa na miwani ya kusomea. 
Msongamano mkubwa wa wananchi waliojitokeza kufanya uchunguzi wa Afya katika Kituo cha Afya Mahonda chini ya Madaktari na wataalamu wa Jumuiya ya Kimataifa ya Baps  Charities. 

Na Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
2/12/2016.
MAKAMU wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema utamaduni wa kupima afya kila baada ya kipindi ni jambo la msingi linalomuwezesha Mwanaadamu kuendelea kuishi vizuri kwa matumaini.

Alisema vipo baadhi ya vifo vya kushitua vinavyowashangaza watu katika maeneo mbali mbali lakini vikichunguzwa chanzo chake hubainika kuwa ni ukosefu wa utambuzi  wa maradhi yaliyokuwa yakimsumbua marehemu ambayo wataalamu walikuwa na uwezo wa kuyatibu.

Balozi Seif Ali Iddi ambae pia ni Mwakilishi wa Jimbo la Mahonda alisema hayo wakati akizindua  rasmi Kambi ya Siku mbili ya Uchunguzi wa maradhi mbali mbali yanayowasumbua wananchi pamoja na kutolewa dawa bure, miwani za kusomea kwa wale watakaobanika kuwa na matatizo ikiwemo pia operesheni za Macho.

Kambi hiyo iliyofunguliwa katika Kituo cha Afya Mahonda inaendeshwa chini ya udhamini wa Jumuiya ya Kimataifa ya kuhudumia jamii ya Baps Charities ikijumuisha wataalamu na Madaktari Bingwa wapatao kumi kutoka Nchini India na Dar es salaam.

Balozi Seif aliwaeleza wananchi hao waliojitokeza kufanya uchunguzi wa Afya zao kuwa na tahadhari ya kujiepusha na ongezeko la maradhi ya kisukari na shindikizo la Damu kwa kuwaona wataalamu wa afya pale wanaoanza kuona dalili za maradhi hayo.

 Alisema vifo vingi vinavyotokea ndani ya jamii  kwa sasa vinaripotiwa kuhusisha maradhi ya Kisukari na sindikizo la Damu ambayo hatimae mgonjwa anaishia kukumbwa na maradhi ya kiharusi.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliipongeza na kuishukuru Jumuiya hiyo ya Kimataifa ya kuhudumia Jamii ya Baps Charities kwa mchango wake mkubwa wa kusaidia jamii yenye kipato cha chini na mazingira magumu.

Mapema Mweka Hazina wa Jumuiya ya Baps Charities Bwana Kapil Dave alisema Taasisi yao imeamua kutoa huduma za Afya kwa jamii ya kipato cha  chini baada ya kubaini ongezeko kubwa la gharama katika upatikanaji wa huduma za afya.

Bwana Kapil aliwatoa hofu Wananchi kwamba huduma za Afya pamoja na Dawa zinazotolewa na Wataalamu na Mabingwa wa Taasisi hiyo hazina mashaka yoyote baada ya kufanyiwa uhakiki na vyombo vinavyohusika Kimataifa.

Mweka Hazina huyo wa Jumuiya ya Baps Charities aliishukuru Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar pamoja na watendaji wote wa Sekta ya Afya waliochangia kuwajengea mazingira bora ya uchunguzi pamoja na utowaji wa huduma za Afya hapa Zanzibar.

Bwana Kapil alifahamisha kwamba ushirikiano huo wa pande mbili ndio uliowawezesha wataalamu wa Afya wa Baps kurejea kutoa huduma tena  Zanzibar baada ile huduma waliyotowa mwanzo katika Kijiji cha Paje Mkoa wa Kusini Unguja kipindi kilichopita.

Wataalamu na Mabingwa hao wa Sekta ya Afya kutoka Baps Charities wanafanya uchunguzi wa maradhi mbali mbali pamoja na kutoa dawa bure ikiwemo miwani za kusomea kwa Wananchi wanaofika kwenye Kambi hiyo.

Zaidi ya Wananchi 1,000 kutoka sehemu mbali mbali za Majimbo na Shehia zilizomo ndani ya Wilaya ya Kaskazini “B” wamejitokeza kufanya uchunguzi wa afya zao na kupatia dawa pamoja na ushauri.

No comments:

Post a Comment