Baadhi ya wastaafu mbalimbali wakiwa tayari kwa ajili ya kufanyiwa uhakiki mkoani Pwani. Uhakiki huu unahusisha wanaolipwa kupitia Wizara ya Fedha na Mipango Pekee.
Na Daudi Manongi,
Maelezo
Tarehe: 10.10.2016
WIZARA ya Fedha na
Mipango imeanza zoezi la Uhakiki wa Wastaafu wanaolipwa na wizara hiyo katika
mkoa wa Pwani, Kibaha. Uhakiki huu hautausisha wastaafu wanaolipwa kupitia
mifuko ya hifadhi za jamii kama vile PSPF, NSSF, PPF na GEPF.
Hayo yamebainishwa na
Mkaguzi wa Ndani Mkuu wa Serikali Bw.Mohamed Mtonga alipokuwa akiongea na
waandishi wa Habari kuhusu mpango huo wa uhakiki ulioanza leo mkoani Pwani.
“Uhakiki huu
unatokana na utaratibu uliojiwekea Wizara ya Fedha na Mipango wa kufanya
uhakiki wastaafu ili kuhuisha orodha ya malipo ya wastaafu na inasaidia kubaini
mabadiliko ya taarifa za wastaafu kama vile kufariki na hivyo kuepuka kulipa
wasiostahili”Alisema Bw. Mtonga.
Aidha akizungumzia
kuhusu utaratibu wa uhakiki huu amesema kuwa zoezi hili litafanyika nchi nzima na limeanzia katika Mkoa wa Pwani wilaya ya
Kibaha na litafanyika kuanzia leo tarehe 10 mpaka tarehe 14 mwezi huu na
kuendelea kwenye wilaya zote za mkoa wa pwani mpaka tarehe 21 mwezi huu.
Baada ya uhakiki
katika mkoa wa Pwani zoezi litaendeshwa kikanda nyanda za juu kusini katika
mikoa ya Mbeya, Iringa, Rukwa, Njombe, Songwe na Katavi kuanzia tarehe 31
Octoba mpaka tarehe 11 Novemba mwaka huu.
Pia zoezi litafanyika
katika kanda ya kati likijumuisha mikoa ya Dodoma, Morogoro na Singida kuanzia tarehe 21 mpaka 25 Novemba.
Akizungumza na
waandishi wa habari mwakilishi wa wazee wastaafu Bw.Benedict Kalaguza amesema
kuwa wanaishukuru serikali kwa kufanya uhakiki huu wa wastaafu na kwamba zoezi
limekuwa ni zuri lisilokuwa usumbufu wowote na limeboreshwa zaidi kwa kutumia
teknolojia nzuri zaidi.
Aidha Wastaafu
wanaohakikiwa wanatakiwa kufika kwenye vituo hivyo wakiwa na nyaraka kama Kadi
ya Benki, Picha za passport mbili, Barua ya Ajira ya Kwanza, Barua ya Kustaafu
au kupunguzwa kazi kazini, barua ya Tuzo la Kustaafu, Nakala ya Hati ya Malipo
ya kiinua mgongo au mkupuo, kitambulisho cha pensheni na barua ya Kudhibitishwa
kazini.
No comments:
Post a Comment