Hali halisi ya Mto Ruaha kwa sasa, kina cha maji kimeshuka sana na kusabisha vifo kwa baadhi ya wanyama wanaotegeme Mto huo. Upungufu wa kina hicho unatokana na shughuli za kibinadamu pembeni mwa mto huo.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais
(Muungano na Mazingira) Mhe. January Makamba akiwa na watendaji kutoka shamba
la Umwagiliaji la Madibila ambapo inasemekana maji mengi yanapotea hivyo
kuadhiri mtiririko wa maji katika mto Ruaha Mkuu.
NA Lulu Mussa, safarini Mbarali
WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais mwenye dhamana ya
kusimamia Muungano na Mazingira Mheshimiwa January Makamba ameshiriki katika
zoezi la kupanda miti katika Shule Msingi Mlandege katika Manispaa ya Iringa
Mjini.
Waziri Makamba amesema kuwa suala la kupanda miti ni agenda
ya kitaifa sasa na kuanzia mwakani kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais Tawala za
Mikoa na Serikali za Mitaa, Wanafunzi wa Shule za Msingi na Sekondari wanapo
ripoti mashuleni ni lazima aje na miti ili ndipo apokelewe.
"Ndugu zangu wana Iringa, tumeazimia kupanda miti kwa
wingi ili kunusuru nchi yetu kuwa jangwa, maana tafiti zinaonyesha kuwa zaidi
ya asilimia sitini na moja (61) ya nchi yetu ni inatishia kuwa jangwa, hivyo ni
wajibu wetu kunusuru hali hii" Makamba alisisitiza.
Waziri Makamba pia alitoa onyo kwa wachafuzi wa chanzo cha
maji cha Mto Ruaha ikiwa ni pamoja na jamii zinazofanya shughuli za kilimo,
ufyatuaji wa matofali na ujenzi pembezoni mwa mto huo kuondolewa na kwa wale watakaokaidi
kushtakiwa mara moja na kuahidi kurudi tena kufuatilia utekelezaji wa agizo
hilo.
Kwa upande mwingine Waziri Makamba ametembelea Hifadhi ya
Taifa ya Ruaha na kujionea upungufu wa maji kwa kiwango kikubwa katika Mto Huo.
Kaimu Mhifadhi wa Hifadhi ya Ruaha Bw. Moronda B. Moronda amebainisha kuwa
upungufu huo si tu una athari kwa wanyama bali ikolojia nzima ya eneo hilo, na
kubainisha kuwa kilimo cha umwagiliaji katika mashamba ya Mbarali ni chanzo
kikuu cha tatizo hilo.
Kufuatia taarifa hiyo, Waziri Makamba alitembelea mashamba
makubwa ya Mpunga na kuagiza kufanyika kwa Ukaguzi wa mazingira kwa kuwa suala
hilo ni la kisheria kwa mujibu wa sheria ya Mazingira ya mwaka 2004.
Pili, Waziri Makamba ameagiza kuundwa kwa kikosi kazi
kitakachojumuisha wajumbe kutoka Mikoa ya Mbeya, Songwe, Iringa, Dodoma,
Morogoro na wadau wa mazingira ili kubaini hasa chanzo cha tatizo hilo ili
kupata ufumbuzi wa haraka.
Waziri Makamba anaendelea na ziara yake ya kikazi ya kukagua
hali ya mazingira nchini, hii leo amewasili katika Mkoa wa Njombe.

No comments:
Post a Comment