Makamu wa Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan
Na Frank Shija,
Maelezo
31/10/2016
WATANZANIA watakiwa
kufanya jitihada za makusudi katika suala zima la utunzaji wa mazingira ikiwa
ni hatua za kukabiliana na athari za Mabadiliko ya Hali ya hewa na Tabia nchi.
Rai hiyo imetolewa leo na Makamu
wa Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan alipokuwa akifungua Tamasha la Kimataifa linalohusu
Mabadiliko ya Tabia ya Nchi linalowakutanisha Wanasayansi, Watafiti na wadau wa
mazingira chini ya Usimamizi wa Kigoda cha Mwalimu Julius Nyerere cha Mazingira
na Mabadiliko ya Tabia ya nchi.
Amesema kuwa suala la
Mabadiliko ya Hali ya Hewa na Tabia nchi siyo hadithi ni jambo ambalo lipo wazi
kuwa ni janga ambalo ipo haja ya kuchukua hatua za makusudi katika kutatua
changamoto zake.
“Wadau wote tuone haja ya
kuyatunza mazingira yetu mwananchi na wadau wa mazingira kwa ujumla, ni muhimu
kwa umoja wetu tukaongeza jitihada za kupanda miti katika maeneo yetu ili
kukabiliana na hali tete ya uharibifu wa mazingira nchini”.Alisema Mama Samia.
Aidha alisema kuwa wakati sasa
umefika wa kuacha uharibifu wa mazingira kuanzia leo na kuanza kuyatunza ili
kukabiliana na athari za Mabadiliko hayo ya Hali ya Hewa na Tabia nchi.
Awali akimkaribisha Makamu wa
Rais, Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhandisi Stella Manyanya
amesema kuwa umefika wakati wakuitazama upya mitaala yetu ili kutoa fursa kwa
elimu ya mazingira inaingizwa katika masomo kuanzia ngazi ya msingi.
Aliongeza kuwa elimu ikitumika
vizuri inaweza kusaidia kwa kuongeza uelewa miongoni mwa jamii hali
itakayopelekea wananchi kutambua namna ya kukabiliana na athari za mabadiliko
hayo na ikiwa ni pamoja na namna ya kuyahifadhi.
Mhandisi Manyanya alisema kuwa
ni faraja kuona Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kinamuenzi Mwl. Nyerere kwa Kuwa
na Kigoda cha Mwalimu kinachohusiana na Mazingira kwani ni ukweli kwamba
Mwalimu alikuwa Mwanamazingira na Muhifadhi wa Mazingira ndiyo maana utaona
aliweza kuweka maeneo mengi ya Hifadhi za Taifa.
Kwa upande wake Makamu Mkuu wa
Chuo Kikuu cha Dar es Salaam Profesa Rwekaza Mukandala alisema kuwa imekuwa ni
kawaida duniani kote kuwa na Vigoda ambavyo utumiwa kama njia ya kuwaenzi
baadhi ya watu kwa michango yao.
Wao kama Chuo Kikuu cha Dar es
Salaam wanamuenzi Baba wa Taifa kwa kuwa na Kigoda cha Mwalimu ambacho
kilianzishwa mwaka 2008 kikiwa kimoja na kuongeza kuwa mpaka kufikia sasa
vimeanzishwa Vingine viwili ambacho kimoja kinahusu Elimu ya Maendeleo na
kingine ndicho hiki cha Masuala ya Mazingira ambacho kinafanya kazi nzuri sana.
Naye Mkurugenzi wa Kituo cha
Mafunzo ya Mabadiliko ya Tabia ya nchi, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam amabye pia
ndiye Mwenyekiti wa Kigoda cha Mwalimu Julius Nyerere cha Mazingira na
Mabadiliko ya Tabia nchi, Profesa Pius Yanda amesema mkutano huo wa siku TANO
utakuwa na jukumu kubwa la kujadili kwa kina namna bora ya kukabiliana na
athari za mabadiliko ya Tabia ya nchi.


No comments:
Post a Comment