Mgombea urais wa Republican nchini Marekani Donald Trump amelalamika akisema kuwa yeye ni mwathiriwa wa kampeni mbaya katika historia ya Marekani.
Amesema hayo huku wanawake zaidi wakijitokeza na kumlaumu kwa kuwanyanyasa kimapenzi.
Trump alitaja madai dhidi yake kama yaliyo ya uongo asilimia 100.
"Si vigumu kupata watu kadha ambao wako tayari kutoa madai ya uongo kunipaka matope," aliambia mkutano wa kampeni Ijumaa.
Kwa sasa imesalia chini ya mwezi mmoja kabla ya uchaguzi mkuu kufanyika, na Bw Trump amewaambia wafuasi wake kuwa uchaguzi huo umeibwa.
Mmoja wa wake wanaomlamu, Summer Zervos anasema kuwa Trump alijaribu kujilazimisha kwake kwenye hoteli ya Beverly karibu mwongo mmoja uliopita.
Kura za maoni za hivi punde zinaonyesha kuwa mgombea wa chama cha Democratic Hillary Clinton anaendelea kuongoza.
Umaarufu wa Bw Trump pia unadidimia katika baadhi ya majimbo yanayoshindaniwa sana.
Tuhuma za karibuni zaidi zimetoka kwa mshiriki wa zamani wa shindano la Apprentice ambaye anasema alinyanyaswa kimapenzi na Bw Trump mwaka 2007.
Mwanamke mwingine naye anasema alidhulumiwa na mgombea huyo mapema miaka ya 1990.
Akiongea katika jimbo la North Carolina, mgombea huyo wa Republican alisema tuhuma hizo ni za uongo, na wanaozitoa wanalenga kujipatia umaarufu na pesa na kwamba wanaongozwa na siasa.
"Au kwa sababu ya kimsingi tu kwamba wanataka kuzuia wimbi letu, wanataka kusimamisha kampeni yetu. Ni rahisi sana," alisema.
No comments:
Post a Comment