Mkuu wa Mkoa wa
Kagera Meja Jenerali Mstaafu Salum Kijuu akiongea na waandishi wa habari leo
mjini Bukoba alipokuwa akitoa taarifa ya hatua zilizochukuliwa na Serikali
katika kurejesha hali baada ya maafa ya tetemeko la ardhi lililoukumba mkoa
huo.
Na
Eleuteri Mangi, MAELEZO, Bukoba
SERIKALI inaendelea na juhudi za kurejesha miundombinu iliyoharibiwa na tetemeko ili
kuhakikisha wananchi wanapata huduma za msingi za kijamii ikiwemo shule za
msingi, sekondari, barabara na vituo vya afya.
Akitoa
taarifa ya urejeshwaji wa hali baada ya tetemeko la ardhi la Septemba 10 mwaka
huu kwa waandishi wa habari leo mjini Bukoba, Mkuu wa Mkoa wa Kagrea Meja
Jenerali Mstaafu Salum Kijuu amesema
kuwa Kamati ya Maafa tayari imetoa vifaa vya ujenzi ili kuhakikisha hali ya
miundombinu inarejea na kuwahudumia wananchi.
Aidha,
Watanzania walioguswa na janga tetemeko wametakiwa kuendelea kuwachangia
Wanakagera ili kuwarejeshea maisha yao ya kawaida.
Katika
kurejesha hali, tayari vifaa mbalimbali vimetolewa ikiwemo mabati 4,496 ya geji
30, mbao 98, misumari ya bati kilo 110 na misumari mchanganyiko kilo 558 ili
kurekebisha na kujenga miundombinu kulingana na uharibifu uliotokea.
“Tumetoa
kipaumbele katika kurejesha miundombinu ya huduma za kijamii kwenye halmashauri
za wilaya zilizoathirika ili kamati za maafa za wilaya ziweze kukarabati
miundombinu ya kutolea huduma za kijamii kama shule za sekondari na msingi,
vituo vya kutolea huduma za afya vilivyoharibiwa na tetemeko ili huduma hizo
muhimu ziweze kurejea mara moja na kutoa huduma kwa wananchi” amesema Meja
Jenerali Mstaafu Kijuu.
Katika
kuhakikisha wananchi wananchi wanapata mahitaji muhimu, Meja Jenerali Mstaafu
Kijuu amesema kuwa Kamati ya Maafa imeendelea kugawa mahitaji kwa wananchi
walioathirika na tetemeko kadri inavyoyapokea kutoka kwa wadau mbalimbali.
Mahitaji
yaliyogawiwa kwa wananchi ni pamoja na unga wa sembe kilo 4,350, sukari mifuko
1,014, mchele kilo 103,400, maharagwe kilo 5,753, mahindi kilo 50,000 majani ya
chai tani 3, maji katoni 850, mafuta ya kula lita 249, sabuni katoni 26,
mashuka 90, mablanketi ya watu wazima na watoto 2,680, vyandarua 1,274, sare za
wananfunzi 570, magodoro 694, mahema 127 na matrubali 5,760.
Kuhusu
watu waliopata majeraha, Meja Jenerali Mstaafu Kijuu amesema wamebakia majeruhi
sita, ambapo katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Kagera wamebakia majeruhi
wawili, Hospitali ya Mugana majeruhi mmoja, na Hospitali ya Rufaa ya Bugando
majeruhi watatu na majeruhi wote wanaendelea kupata huduma za matibabu na hali
zao zinaendelea vizuri.
Mkuu
huyo wa mkoa amesema kuwa awali baada ya tetemeko la ardhi kulikuwa na majeruhi
440 ambapo tayari majeruhi 434 wametibiwa na kuruhusiwa katika Hospitali ya
Rufaa ya mkoa na vituo mbalimbali vya afya kwenye mkoa huo.
Kwa
upande wa misaada iliyopokelewa na kamati ya maafa, Meja Jenerali Mstaafu Kijuu
amesema kuwa kamati ya maafa imepokea misaada ya mahitaji mbalimbali yenye
thamani ya zaidi ya shilingi 1,094,478,950 ambayo imeendelea kugawiwa kwa wananchi
kadiri ilivyokuwa inaletwa na wananchi na wadau wengine.
Aidha,
Mkuu huyo wa mkoa amewashukuru wananchi pamoja na wadau mbalimbali ambao
wameendelea kutuchangia kwa fedha taslimu na hundi katika akaunti maafa
inayojulikana kwa jina la “Kamati Maafa Kagera 0152225617300 CRDB BUKOBA.” ambapo
hadi Oktoba 03 mwaka huu zimepokelewa jumla ya shilingi bilioni
3,481,069,473.43 na kuwaasa wananchi wasikatishwe tamaa kuchangia kutokana na
tukio la hivi karibuni la kufunguliwa akaunti nyingine ambayo siyo halali na
kuwahakikishia kuwa suala hilo limedhibitiwa na hakutakuwepo na udokozi wala
matumizi mabaya ya fedha zinazochangwa wala vifaa vinavyochangiwa.
Wakati
huo huo, Mkuu wa mkoa amesema kuwa mitandao ya simu ya M-pesa 0768196669, Tigo
Pesa 0718069616, na Airtel Money 0682950009 hadi kufikia Oktoba 03 2016 zimepokelewa
jumla ya shilingi milioni 4,750,927.
Zaidi
ya hayo Meja Jenerali Mstaafu Kijuu aesema kuwa Kamati ya Maafa inaendelea
kuwahudumia wananchi walioathirika na tetemeko mkoani Kagera wanaotoa malalamiko,
ushauri, maoni na taarifa mbalimbali kutoka kwa wananchi waloathirika katika
tetemeko.
Malalamiko
yanaweza kuletwa kwa kamati kupitia za namba za simu zilizotolewa katika Ofisi
ya Mkuu wa Mkoa 0621155777na Ofisi ya Waziri Mkuu 0621155888 na kujibiwa au
kuelekezwa wanachotakiwa kufanya ili kupata huduma ya misaada.
Kupitia
namba hizo za simu kamati imepokea jumla ya simu 82 kutoka maeneo mbalimbali na
wananchi kuhudumiwa na kupata misaada waliotarajia na kuwataka wananchi
kuendelea kutumia simu hizo ili kutatuliwa kero zao hasa kuhusu misaada.
Mkuu
wa mkoa alitumia nafasi hiyo kuwaomba wananchi wote ambao waliathirika na
tetemeko la ardhi na nyumba zao kuharibiwa wahakikishe wanaanza kurejesha
miundombinu ya nyumba zao kama baadhi yao walivyokwisha kufanya wasisubiri
kujengewa na kuongeza kuwa Serikali inajenga miundombinu iliyoharibiwa ya
kutolea huduma za jamii.
No comments:
Post a Comment