Na Hussein Makame, NEC
TUME ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imevitaka vyombo
vya habari kuialika tume hiyo iwapatie elimu ya mpiga kura ili kukuza uelewa wa
vyombo hivyo juu ya sheria, kanuni, na taratibu zinazoongoza uchaguzi na
kufahamu majukumu ya tume hiyo.
Alisema NEC imejipanga kutoa elimu ya mpiga kura
nchi nzima na iko tayari kupokea maombi ya kwenda kutoa elimu hiyo kwa wamiliki
wa vyombo vya habari, wahariri na wafanyakazi wote wa vyombo hivyo ili kukuza
uelewa wa sekta hiyo.
“Niwaombe
vyombo vya habari, tumeanzisha programu ya elimu ya mpiga kura tualikeni kwenye
vyombo vyenu vya habari, mtualike tuje tuzungumze na nyinyi vyombo vya habari
kimoja baada ya kingine” alisema Bw. Kailima na kufafanua kuwa:
“Sisi tunataka kuzungumza na wewe mmiliki wa
chombo na watumishi wako na viongozi wenzako wote ili tukueleweshe kuhusu
Sheria ya Taifa ya Uchaguzi na Sheria ya Uchaguzi ya Serikali za Mitaa,
utaratibu mzima wa uchaguzi na uijue Tume ili unapoandika ujue ninachoandika si
cha kubahatisha.”
Bw. Kailima alisema elimu hiyo kwa vyombo vya
habari pia itaviwezesha kuwa na uelewa mpana juu ya masuala mbalimbali ya
uchaguzi na kutoa changamoto kwa mtendaji huyo wa NEC pindi anapopata na nafasi
ya kuzungumza nao.
Katika kutekeleza mkakati endelevu wa kutoa elimu
ya mpiga kura nchi nzima, Bw. Kailima ameanza kutoa elimu hiyo kupitia
televisheni mbalimbali nchini na kwamba yuko tayari kuzungumza na vyombo
mbalimbali kutekeleza mkakati huo.
Kwa upande mwingine, Bw. Kailima amewataka
Watanzania wakisikia kuna maonesho au mkutano ambapo Tume inashiriki wafike
banda la NEC waulize maswali wapate ufahamu na watapata uelewa mkubwa juu ya
mchakato wa uchaguzi.
Akizungumza kwa nyakati tofauti, Bw. Kailima
alisema NEC itahakikisha inatumia maonesho, mikutano na mikusanyiko mbalimbali
ikiwemo mikutano ya kidini ili kutoa elimu ya mpiga kura ikiwemo shule za
sekondari nchini.
Alisema lengo kuu la kutekeleza hayo ni
kuhakikisha ifikapo mwaka 2020 wananchi wawe wamepata uelewa wa kutoa kuhusu
taratibu za uchaguzi na kufahamu majukumu ya Tume ili kupunguza malalamiko na
upotoshaji unaofanywa katika kipindi cha uchaguzi.
Tayari Bw. Kailima ameshatoa elimu ya mpiga kura
kupitia televisheni za Shirika la Utangazaji la Zanzibar (ZBC) na Televisheni
ya Afrika Mashariki (EATV) na amesema NEC inajipanga kutoa elimu hiyo kupitia
vyombo vya habari na mitandao ya kijamii.
Alisema aidha NEC itatoa matangazo kwenye vyombo
vya habari kuziomba Asasi za Kiraia zinazoweza kutoa elimu ya mpiga kura kutuma
maombi ili kupatiwa ridhaa ya kutoa elimu hiyo kwa umma.
No comments:
Post a Comment