Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira Mhe. January Makamba akihutubia wananchi wa Kijiji cha Mwantasi Wilaya ya Kilolo Mkoani Iringa, aliposimama akiwa katika ziara ya kikazi ya kukagua masuala ya mazingira.
Mjumbe wa Kamati ya Mazingira ya Kijiji cha Mwantasi Wilaya ya Kilolo Mkoani Iringa akipokea kiasi cha Shilingi laki moja zilizotolewa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira Mhe. January Makamba kuchangia Mfuko wa Mazingira wa Kijiji.
Waziri wa Nchi Ofisi
ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira Mhe. January Makamba na ujumbe wake wakikagua
mitambo ya kusukuma maji katika Mkoa wa Iringa, wa kwanza kulia ni Mkuu wa Mkoa
wa Iringa Bi. Amina Masenza.
Na Lulu Mussa
Kilolo - Iringa
WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira
Mhe. January Makamba amesisitiza umuhimu wa kutunza Vyanzo vya Maji kwakuwa
shughuli zifanywazo na binadamu kando ya Vyanzo hivyo hupelekea mito hiyo
kukauka.
hayo yamebainishwa leo na Waziri Makamba alipofanya ziara ya
kikazi Kihansi Wilayani Kilolo kuangalia chanzo cha Mto Kihansi. Waziri Makamba
kwa nyakati tofauti amefanya mazungumzo na wanakijiji wa Kijiji cha Mwantasi
ambao wamefanya jitihada za dhati kuhifadhi Vyanzo vya Maji.
Waziri Makamba amewapongea na kuchangia kiasi cha shilingi
laki mbili kwa vijiji vya Mwantasi kwa ajili ya Mfuko wa Mazingira wa Kijiji wenye
lengo la kusimamia masuala za mazingira katika kijiji chao.
"Nawapongeza sana kwa jitihada mlizonazo ikiwa ni pamoja
na kuwa na sheria ndogo ndogo za kutunza mazingira, nami nawaunga mkono kwa
kuchangia kiasi cha shilingi laki moja kwa kijiji cha Mwantasi na laki moja kwa
kijiji cha Wangama ili kuimarisha mfuko huo" Makamba alisisitiza.
Aidha Waziri Makamba amemuagiza Mkurugenzi wa Kilolo
kuhakikisha fani zinazotozwa za uharibifu wa mazingira sehemu ya pesa hizo
zinapelekwa katika vijiji husika ili kukuza mfuko huo na kuwaagiza wajumbe wa
Kamati za Mazingira ngazi ya kijiji kuzitunza fedha hizo benki na kuagiza
matumizi sahihi.
Waziri Makamba anaendelea na ziara ya kikazi katika Mikoa
mbalimbali hapa nchini na leo yuko katika Mkoa wa Morogoro ambapo ametembelea
Mto Kihansi na Ruaha Mkuu.

No comments:
Post a Comment