Katibu
Tawala wa Mkoa wa Dar es Salaam, Bi. Theresia Mmbando akizungumza kuhusu ripoti
ya hali ya maendeleo ya utekelezaji wa
Mpango wa kunusuru kaya maskini (TASAF III) alipokutana na waandishi wa habari
(hawapo pichani) leo Jijini Dar es Salaam.(Picha
na Frank Shija, Maelezo)
Na Abushehe Nondo
& Frank Shija, Maelezo, Dar es Salaam.
JUMLA ya kaya 26,248
zimenufaika na mpango wa kunusuru kaya maskini (TASAF III) kwa kupatiwa jumla
ya shilingi Bilioni 6.6 katika mkoa wa Dar es Salaam.
Hayo yamebainishwa na
Katibu Tawala wa Mkoa wa Dar es Salaam Theresia Mmbando wakati akiongea na
waandishi wa habari leo Jijini Dar es Salaam.
Mmbando amesema kuwa
utambuzi wa kaya maskini ulianza mwezi Januari 2015 kwa kushirikisha wilaya za
Kinondoni, Temeke na Ilala ambapo jumla ya kaya 26,248 zilizoandikishwa na
kupokea ruzuku kila baada ya miezi
miwili kwa kuzingatia mzunguko wa malipo.
Aliongeza kuwa
wanufaika wa mpango huo wamepatikana kutokana na ushirikishwaji wa jamii husika
ambapo jamii yenyewe ilibainisha majina ya walengwa katika maeneo yao.
Aidha Mmbando amesema
kuwa pamoja na mafanikio hayo kuna baadhi ya changamoto zilizojitokeza katika
kutekeleza mpango huo ikiwemo baadhi ya kaya zilizokidhi vigezo kukataa kuandikishwa,
kuandikishwa kwa kaya zisizokuwa na sifa, pamoja na kupokea ruzuku pungufu.
Katika kukabiliana na
changamoto hizo, Mmbando amesema mpaka sasa jumla ya kaya 609 zimeondolewa
katika kwenye mpango huo ikiwemo kaya 141 (Ilala), kaya 296 (Kinondoni) na kaya
172 (Temeke).
Kwa upande wake
Mratibu wa TASAF Mkoa wa Dar es Salaam, Esterine Sephania amesema kuwa suala la
udanganyifu wa kuandikishwa kwa walengwa wasiokuwa na sifa linaanzia katika
ngazi ya serikali za mitaa ambapo huko ndiko wanaleta majina.
Aliongeza kuwa
kutokana na udanganyifu uliojitokeza katika zoezi hilo takribani shilingi
milioni 2.2 zimepotea kupitia udanganyifu uliotokana na uandikishwaji kwa watu
wasiokuwa na vigezo.


No comments:
Post a Comment