Mmoja
wa Madaktari Bingwa akifafunua jambo wakati wa mkutano na waandishi wa habari uliofanyika
katika Ofisi za Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam jana. Madaktari hao kwa
kushirikiana na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam wameandaa zoezi wa upimaji wa
Afya kwa wakazi wa jiji hili litakalofanyika mapema wikiendi hii katika viwanja
vya Mnazi Mmoja kuanzia saa 2:00 Asubuhi.
Na Frank Shija, MAELEZO.
23/09/2016.
WAKAZI wa jiji la Dar es Salaam
na viunga vyake wametakiwa kujitokeza katika zoezi la upimaji wa Afya zao siku
ya jumamosi na jumapili za tarehe 24 na 25 Septemba katika viwanja vya mnazi
mmoja Jijini Dar es Salaam.
Wito
huo umetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Paul Makonda alipokuwa akiongea
na waandishi wa habari ofisini kwake kuhusiana na zoezi hilo jana Jijini Dar es
Salaam.
Makonda
amesema kuwa Ofisi yake imeandaa zoezi
la kiafya kwa wanachi wote wa mkoa wa Dar es Salaam ili wapate fursa ya kujua
afya zao ili waweze kujikinga na magonjwa yanayoweza kujitokeza, na kuepuka
matumizi ya gharama kubwa za matibabu na kuzia vifo visivyo vya lazima.
“Natoa
wito kwa wananchi wote wa Mkoa wa Dar es Salaam na viunga vyake wajitokeze kwa
wingi siku za jumamosi tarehe 24 na jumapili tarehe 25 Septemba katika Viwanja
vya Mnazi Mmoja kuanzia majira ya saa mbili asubuhi waje kuchunguza Afya zao,
huduma hii itatolewa na Madaktari Bingwa bila malipo yoyote” Alisema Makonda.
Aliongeza
kuwa upimaji huo umelenga zaidi magonjwa kumi makubwa yasiyopewa kipaumbele
ambapo aliyataja kuwa ni pamoja na Shinikizo la Damu, Kisukari, Saratani ya
Matiti, Saratani ya Shingo ya uzazi, Tezi Dume,Saratani ya ngozi kwa watu wenye
Alibinism, na magonjwa mengiyo kadri ya uhitaji wa mwananchi.
Zoezi
hilo halitakuwa na ubaguzi hivyo ni vyema mtanzania yeyote atakayekuwepo Jijini
Dar es Salaam katika siku hizo za zoezi la upimaji, akatumia fursa hiyo
kujipatia huduma ya kuchunguza hali ya Afya yake bila ya malipo.
Awali
akizungumza katika kikao hicho Mganga Mkuu wa Manispaa ya Kinondoni Dkt. Aziz
Msuya amesema kuwa watanzania wengi wamekuwa wanashindwa kupata huduma ya
vipimo kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo gharama kubwa kwa baadhi ya vipimo
na umbali wa mahali inapopatikana huduma husika.
Huduma
hii ya upimaji wa Afya unafanyika ikiwa ni mara ya kwanza kwa Ofisi ya Mkuu wa
Mkoa wa Dar es Salaam kwa kushirikiana na Madaktari Bingwa kutoka Hospitali ya
Taifa ya Muhimbili, Taasisi ya Saratani ya Ocean Road, Taasisi ya Moyo ya
Jakaya Mrisho Kikwete, Hospitali za Rufaa za Mkoa wa Dar es Salaam, Hospitali
ya Agakhan pamoja na Taasisi ya CCP Medicine.



No comments:
Post a Comment