
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Roma Makani
Na Beatrice Lyimo-Maelezo, Dodoma
07/09/2016
SERIKALI imeunda timu ya wataalamu inayoendelea na kazi ya kutatua na kupatia suluhisho migogoro mbalimbli ya ardhi nchini.
Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii Mhandisi Ramo Kamani alipokuwa akijibu swali la Mhe. Dkt Shukuru Kawambwa lililohusu mpango wa Serikali katika kumaliza mgogoro kati ya TANAPA na vitongoji vya Kitame, RAZABA Gama-Makani katika kata ya Makurunge wilayani Bagamoyo.
Mhandisi Kamani amesema kuwa mgogoro baina ya kijiji cha Makarunge na hifadhi, unaonesha wananchi hawakushirikishwa katika zoezi la uwekaji mipaka ambapo zoezi hilo liliwashirikisha kikamilifu kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu ikiwa ni pamoja na kufanyika kwa mkutano na wanakijiji hao.
Aidha, Mhandisi Kamani amesema kuwa mgogoro wa baina ya shamba la RAZABA na hifadhi umetokana na utata wa eneo la takribani hekta 3,441, ambapo juhudi za kutatua mgogoro huo zinaendelea kufanyika kwa kushirikisha ngazi za vijiji, wilaya, mkoa na wizara husika na kutolewa maelekezo ikizingatia athari za mazingira.
Kwa upande wa mgogoro baina ya Gama-makani na hifadhi, Mhandisi Kamani amesema kuwa mgogoro huo unatokana na malalamiko ya wananchi kuwa baadhi yao walifidiwa wakati wa uanzishwaji wa hifadhi ambapo hawakuwa wamiliki wazawa wa maeneo hayo.
“Mgogoro huu unatokana na malalamiko ya wananchi kuwa baadhi ya wananchi ambao walifidiwa wakati wa uanzishwaji wa hifadhi katika eneo hilo, hawakuwa wamiliki wazawa wa maeneo hayo, ingawa taarifa zinaonesha kuwa mchakato wa malipo ya fidia ulifuata taratibu muhimu ikiwemo ushirikishwaji wa karibu wa uongozi wa wilaya ya Bagamoyo, Serikali za kata na Serikali za vijiji husika,” amefafanua Naibu Waziri huyo.
Migogoro yote iliyoainishwa inahusiana na hifadhi ya taifa Saadani iliyoanzishwa kisheria kwa tangazo la serikali (GN) Na. 281 la mwaka 2005.
KIVUTIO CHA KIMONDO KUENDELEA KUONGEZA
MAPATO YA SERIKALI
Na Beatrice Lyimo-Maelezo, Dodoma.
07/09/2016
SERIKALI inaendelea kutangaza Kimondo kilichopo Wilaya ya Mbozi Mkoani Mbeya ikiwa ni kivutio muhimu na adimu nchini na duniani kwa ujumla.
Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii Mhandisi Ramo Kamani leo mjini Dodoma alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Vwawa Mhe. Japhet Hasungu lililohusu mpango wa Serikali katika kuhamasisha watalii wa ndani na nje kuja kuangalia Kimondo hicho.
Naibu Waziri huyo amesema kuwa Serikali imekuwa inaendelea kuhamasisha kwa kukitangaza Kimondo hicho kwa kutumia njia mbalimbali ikiwemo vipindi vya runinga na nakala za machapisho mbalimbali.
“Uhamasishaji umefanyika kwa kutumia njia mbalimbali ndani na nje ya nchi ikiwa ni pamoja na vipindi vya runinga vya ZAMADAMU na Utalii wa ndani na kutumia machapisho ya Tanzania ya “The land of great Heritage Sites” na “Tanzania Cultural Heritage Resources” ambapo nakala zake husambazwa katika maonesho mbalimbali na Balozi zetu pamoja na jarida la “Ifahamu Idara ya mambo ya kale”” na jarida la Maliasili,” alifafanua Naibu Waziri huyo.
Aidha, Mhandisi Kamani aliongeza kuwa juhudi hizo limepelekea ongezeko la idadi ya watalii na mapato ambapo kati ya mwaka 2012/2013 na 2014/2015 watalii waliongezeka kutoka 990 hadi 1,681 pamoja na mapato kuongezeka kutoka shilingi 811,000 hadi 2,426,00.
Mbali na hayo, Mhandisi Kamani alitoa wito kwa Halmashauri ya Wilaya ya Mbozi na wadau wengine kujitokeza kuboresha mazingira na miundombinu ya eneo la kimondo hicho ili kuweza kuzidi kuvutia watalii wengi na kuongeza pato la taifa.
Kimondo hicho kinaendelea kuiweka Tanzania katika ramani ya dunia katika masuala ya utalii ambapo kinaaminiwa kuwa ni kati ya vimondo nane vikubwa zaidi duniani kinachokadiriwa kuwa na uzito wa tani 12, urefu wa mita 3.3, upana wa mita 1.63 na kimo cha mita 1.22.

No comments:
Post a Comment