Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Angellah J. Kairuki (Mb) akitoa ufafanuzi wa masuala ya kiutumishi wakati wa kipindi cha TUNATEKELEZA kilichorushwa na Runinga ya Taifa (TBC-1). Kushoto ni muongozaji wa kipindi hicho Bi. Eshe Muhidin.
WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais-Menejimenti ya Utumishi wa Umma na
Utawala Bora Mhe. Angellah J. Kairuki (Mb) alisema hayo hivi karibuni katika
kipindi cha mahojiano ya moja kwa moja katika Runinga ya Taifa (TBC) na
kusisitiza waajiri wanawajibu wa kuondoa mtumishi yeyote asiyestahili mara moja.
“Tumefanya
zoezi mahsusi kuwaondoa kwenye orodha ya malipo ya mishahara watumishi
wasiostahili. Watumishi wanaoondolewa ni
wale walioacha kazi, kufukuzwa kazi, kumalizika kwa muda wa ajira ya mkataba na
kugombea nafasi za kisiasa. Kuanzia tarehe 01 Machi, 2016 hadi tarehe 20
Agosti, 2016 jumla ya watumishi 16,127 wameondolewa na wasingeondolewa
kwa wakati wangeisababishia Serikali
hasara ya Shilingi 16,014,697,390 kwa mwezi mmoja” Mhe. Kairuki aliainisha.
Alisema
hatua zinachukuliwa kwa wote waliobainika kuhusika katika suala hilo ambapo hadi
tarehe 20 Agosti, 2016 jumla ya watumishi
839 walifikishwa Polisi na TAKUKURU ili kutoa maelezo; na uchunguzi unaendelea hatimaye hatua za kisheria
zichukuliwe kulingana wa ushahidi
utakaopatikana.
Waziri
Kairuki alisema lengo la Serikali ni kuhakikisha kwamba fedha zote zilizolipwa
kwa watumishi wasiostahili zinarejeshwa Serikalini akibainisha kuwa toka mwezi
Machi, 2016 hadi mwezi Julai, 2016 jumla fedha zilizorejeshwa ni Shilingi
14,403,046,089.27 na zoezi ni endelevu.
Waziri
Kairuki alisema Mfumo wa Taarifa za Kiutumishi na Mishahara (HCIMS)
unaimarishwa kulingana na mahitaji na kutaja maeneo yaliyoimarishwa ikiwamo; Uwezo
wa kutambua na kuzuia kuajiriwa watu wenye majina yanayofanana; Kuongeza moduli
ambayo inamwezesha mwajiri kufanya uhakiki wa watumishi kwa kutumia taarifa
mbalimbali zikiwemo za Kitambulisho cha Taifa; Uwezo wa kuwaondoa kwenye orodha
ya malipo ya mishahara watumishi waliofikisha umri wa kustaafu na ambao hawana
mikataba; Kuongeza Moduli ya Utambuzi wa Kituo cha Kazi cha mtumishi (Service Delivery Point) na hilo limeanza
kwa Idara za Afya, Elimu, Kilimo na Mifugo; na Wigo wa matumizi ya mfumo
umepanuliwa ili kuwawezesha Wakuu wa Idara za Afya, Elimu (Sekondari/Msingi),
Kilimo na Mifugo kutumia na kuona taarifa za watumishi walio chini yao.
Akiongea kuhusu mkakati wa kuboresha Maadili katika Utumishi wa Umma
alisema
pamoja na mambo mengine Serikali
inasimamia kukuza uelewa wa Maadili kwa Watumishi wa Umma kupitia mafunzo
na kuendeleza ushiriki wa Asasi za Kiraia (AZAKI) katika kuhamasisha wananchi kuzingatia
maadili na kuacha kutoa vishawishi kwa watoa huduma. Pia, kuhakikisha kila
Taasisi ya Umma ina Mkataba wa Huduma kwa Mteja na dawati la kupokea,
kushughulikia malalamiko na kutoa mrejesho kwa wananchi.
Waziri
Kariuki aliongeza pamoja na ofisi yake kuhakikisha Watumishi wa Umma wanatoa Kiapo cha Ahadi ya Uadilifu
na kusimamia viapo hivyo, pia inaandaa Mfumo wa Kielektroniki unaojulikana kama
“Watumishi Portal” ambao utakuwa na
moduli ya kupokea malalamiko, maoni na kero mbalimbali kutoka kwa Watumishi wa
Umma na kuhamasisha Taasisi za Umma kuwa na kituo mahususi cha utoaji huduma (One Stop Service Centre) ili kupunguza
kero kwa wananchi wanaofuata huduma.
Eneo la Uwajibikaje hali
ikoje?
Waziri Kariuki alisema Serikali imekuwa
na utaratibu wa kupima utendaji wa Mtumishi Mmoja mmoja kwa kutumia Mfumo wa
Wazi wa Mapitio na Tathmini ya Utendaji Kazi (OPRAS).
Hata hivyo, alisema “Serikali inalenga kuimarisha
mfumo wa uwajibikaji katika ngazi ya Taasisi ili kuhakikisha Taasisi za Umma
zinatekeleza majukumu yake ipasavyo kwa kuanzisha Mfumo wa Mikataba ya Utendaji
Kazi katika Taasisi zote za Umma kuanzia mwaka wa fedha 2017/18”.
Alifafanua
kuwa Mkataba huo ni makubaliano ya kimaandishi kati ya Taasisi za Umma na
Serikali ambayo yatatekelezwa na Taasisi husika katika kipindi cha mwaka mmoja
na Mkataba utajikita katika kupanga na kupima utendaji wa
Taasisi na utakuwa
na malengo, shabaha, vigezo na viashiria vya utendaji ambavyo vitatekelezwa na
Taasisi katika mwaka husika.
Waziri
Kairuki alianisha kuwa Mkataba huo utaainisha wajibu wa Serikali katika
kuwezesha Taasisi kufikia malengo na shabaha na utekelezaji wake utafanyiwa
tathmini kila mwisho wa mwaka na matokeo yake kutangazwa kwa umma.
Miongoni mwa faida za mfumo huo ni kuziwezesha Taasisi za
Umma kuimarisha uchaguzi wa vipaumbele katika ngazi ya Taasisi na upangaji
mipango ya utekelezaji kila mwaka; kuimarisha ufuatiliaji na upimaji utendaji
kazi; na kuimarisha uwajibikaji na uwazi.
Usimamizi wa Maadili kwa viongozi wa Umma
ukoje?
Waziri Kairuki alieleza kumekuwepo na malalamiko ya ukiukwaji
wa maadili dhidi ya viongozi wa Umma na hadi kufikia Agosti 2016, malalamiko
200 yalipokelewa ambapo kati ya malalamiko hayo, malalamiko 142 yalihusu Sheria
ya Maadili na malalamiko 58 hayakuhusu Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma.
“Uchunguzi wa awali umefanyika kwa malalamiko 11
yanayohusu ukiukwaji wa Sheria ya Maadili. Aidha, malalamiko 58 ambayo hayakuhusu
ukiukwaji wa Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma walalamikaji walipewa
ushauri na mengine yalielekezwa kwenye mamlaka zinazohusika. Malalamiko hayo
yalihusu pamoja na mambo mengine masuala ya rushwa na migogoro ya ardhi” Mhe.
Kairuki alifafanua.
Aliongeza hatua zinazochukuliwa dhidi ya Viongozi wa
Umma wanaothibitika kukiuka Sheria ya maadili ni pamoja na kufikishwa katika Baraza
la Maadili lililoundwa kwa mujibu wa kifungu cha 26 cha Sheria ya Maadili ya
Viongozi wa Umma ili kufanya uchunguzi wa kina.
Kuanzia mwaka 2010/11 hadi 2015/16 jumla ya mashauri
69 ya ukiukwaji wa Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma yalifanyiwa kazi na
Baraza la Maadili, kati yake mashauri 38 yalithibitika kukiuka Sheria ya
Maadili na Viongozi na wahusika kupewa adhabu mbalimbali ikijumuisha Onyo (12),
Onyo Kali (19), Faini ya shilingi milioni moja (1), kushushwa cheo (3) na
kuondolewa katika wadhifa (3).
Waziri Kairuki mwenye dhamana na Utumishi wa Umma na
Utawala Bora nchini alisema miongoni mwa mashauri hayo yalihusu kutowasilisha
Tamko la Rasilimali na Madeni, kutoa tamko la uongo, matumizi mabaya ya
madaraka na mali ya umma na mpaka wakati huu Sekretarieti ya Maadili ina malalamiko 12 yakufikisha
mbele ya Baraza la Maadili.
Pamoja na hayo, alisema ipo mikakati ambayo Serikali inaitumia
katika kukuza maadili ya viongozi wa umma nchini ikiwamo kutoa elimu kuhusu
Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma ambapo katika mwaka wa fedha 2015/16,
Viongozi wa Umma 7,442 walipatiwa elimu kuhusu Sheria ya Maadili ya Viongozi wa
Umma, Mgongano wa Maslahi na Maadili ya Utumishi wa Umma.
Hali ikoje kuhusu Nyaraka na
Siri za Serikali?
Waziri
Kairuki alisema kwa mujibu wa Sheria ya Usalama wa Taifa ya mwaka 1970 na
Sheria ya Kumbukumbu na Nyaraka ya Mwaka 2002 ni kosa la jinai kwa mtu yeyote kutoa
au kuvujisha taarifa zenye zuio kwa wasio walengwa.
Aliainisha
kuwa Serikali imekuwa ikichukua hatua kuhusu
hilo ikiwamo kuwashitaki wahusika mahakamani kwa kuvunja sheria, Kuwachukulia
hatua za kinidhamu watumishi wa Umma na hatimaye kufukuzwa kazi, kushushwa cheo
na kupunguziwa mshahara, Kutoa elimu kwa watumishi na wananchi juu ya Sheria na
Kanuni zinazosimamia masuala ya utoaji wa taarifa, nyaraka na siri za Serikali.
Hatua nyingine zinazochukuliwa ni Kuendelea
kusimamia Sheria ya Usalama wa Taifa Na. 3 ya mwaka 1970 na Sheria ya
Kumbukumbu na Nyaraka ya Mwaka 2002, Mwongozo wa Matumizi Bora, Sahihi na
Salama ya Vifaa vya TEHAMA wa mwaka 2012 na Kanuni za Maadili ya Utendaji
katika Utumishi wa Umma za mwaka 2005, pia kuimarisha matumizi na usalama wa mifumo
ya TEHAMA ili kudhibiti uvujaji wa nyaraka na siri za Serikali kupitia mitandao
ya kijamii.
Matumizi
ya TEHAMA yakoje Serikalini?
Waziri Kairuki alisema matumizi ya Teknolojia
ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) yamepunguza gharama za uendeshaji wa kazi
mbalimbali za Serikali akitolea mfano wa uendeshaji wa semina na mikutano kwa
njia ya mawasiliano ya video (Video
Conference) ambapo mikutano ya Serikali
hufanyika kwa gharama nafuu kwani haimlazimu mshiriki kusafiri; na uendeshaji
wa mafunzo ambapo mwezeshaji mmoja anaweza kuendesha mafunzo kwa watendaji katika
zaidi ya kituo kimoja.
Alisema hadi sasa huduma hii ipo katika
Mikoa yote isipokuwa mikoa ya Geita, Katavi, Njombe, Simiyu na Songwe ambayo Serikali
ipo katika mkakati wa kufikisha huduma hiyo, pamoja na hilo taasisi 77
zimeunganishwa kwenye Mtandao wa Mawasiliano ya Serikali (GovNet) hivyo kufanya
mawasiliano kulipia muda wa maongezi.
“Azma ya Serikali ni kutatua kero zinazowakabili wananchi katika kupata huduma mbalimbali
katika Taasisi za Umma” Waziri Kairuki alisema na kuelezea utekelezaji wa miradi
kama Mawasiliano ya ndani
ya ofisi (electronic Office) kupitia
Ofisi ya Rais-Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Wakala ya Serikali Mtandao
(eGA), Utunzaji wa Kumbukumbu na Nyaraka (electronic
Records) kupitia Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa, Ununuzi wa Umma
kwa njia ya Mtandao (e-Procurement system)
kupitia PPRA na MSD, na Huduma za Kitabibu kwa njia ya mtandao (Telemedicine system) kupitia Hospitali
ya Taifa ya Muhimbili.
Mapambano
dhidi ya rushwa
Waziri
Kairuki alieleza Serikali imekuwa ikichukua hatua katika kuzuia na kupambana na
rushwa nchini mfano kwa kufuatilia
fedha za Miradi ya Maendeleo kupitia Ofisi za Kanda za TAKUKURU kwa lengo la
kuhakikisha thamani ya miradi inayotekelezwa inaendana na kiasi cha fedha
kilichotolewa ambapo ufuatiliaji huo umeiwezesha Serikali kuokoa kiasi cha Shilingi
Bilioni 39.34.
“Tumewasilisha
majalada 297 kwa Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) kwa ajili ya kuombewa
kibali cha mashitaka ambapo majalada 229 yalipata kibali cha kuwafikisha
watuhumiwa mahakamani” Waziri Kairuki alifafanua.
Aliongeza
mikakati ya serikali ni pamoja na kuhuisha
Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Na. 11 ya 2007 ili kujumuisha makosa ya
uhujumu uchumi na kutaifisha mali zilizopatikana kwa njia ya Rushwa na Ufisadi.
Kuhusu kaya masikini hali hali ikoje?
Waziri
Kairuki alisema Mpango wa Kunusuru Kaya Masikini ambao
utachukua miaka kumi unatekelezwa katika Halmashauri zote za Tanzania Bara
pamoja na Zanzibar.
“Katika kipindi cha miaka minne mpango
umetekelezwa Vijiji, Mitaa na Shehia 9,960 ambayo ni sawa na wastani wa
asilimia 70. Kaya 1,358,268 zimetambuliwa ambapo kati ya hizo, Kaya 1,110,377
zimeandikishwa” Waziri Kairuki alisena na kuongeza kaya 1,110,377
zimehawilishiwa fedha kwa kulipwa ruzuku katika awamu 16 ili kuziwezesha kuwekeza
katika lishe, afya na elimu.
Mpango wa Uendeshaji wa Shughuli za Serikali kwa Uwazi
unatekelezeka?
Waziri Kairuki alisema Mpango
wa Uendeshaji wa Shughuli za Serikali kwa Uwazi (Open Government Partnership) ulianza kutekelezwa nchini toka mwaka
2012/13, na umejikita katika kuweka uwazi zaidi katika uendeshaji wa shughuli
za Serikali; Ushirikishwaji wa Sekta za Umma na Binafsi katika utekelezaji wa
Mpango; Uwajibikaji wa Serikali kwa Wananchi; Matumizi ya Teknolojia na
Ubunifu; na Mapambano dhidi ya Rushwa.
Alisema miongoni mwa yaliyofanyika ni pamoja
na kuongezeka kwa uwazi kuhusu bajeti ya Serikali kwa kuandaa kijitabu cha “Citizen
budget” kilichoandaliwa kwa Kiswahili na
lugha rahisi kwa kuchapishwa kwenye tovuti ya Wizara ya Fedha na Mipango.
Pia, taarifa za utekelezaji za sekta za kipaumbele Afya, Elimu na Maji kuchapishwa
katika Tovuti za sekta hizo na kukamilika kwa zoezi la upembuzi yakinifu wa
Takwimu Huria (Open Data) ili kuongeza uwazi wa takwimu na taarifa
mbalimbali;
Waziri
Kairuki alisisitiza kuwa Serikali inaendelea kutekeleza Mpango wa Uendeshaji wa
Shughuli za Serikali kwa Uwazi kwa mikakati mbalimbali ikiwamo, kuendelea na
utekelezaji wa kuwa na uwazi katika bajeti ya Serikali kwa kuweka taarifa za
bajeti kwenye tovuti mbalimbali kwa lugha nyepesi na kwa Kiswahili na kuimarisha
mfumo wa Takwimu Huria ambayo utarahisha wadau mbalimbali kupata takwimu zinazohusu
masuala mbalimbali hususan Afya, na Elimu.
Ofisi ya Rais - Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora
(OR-MUUUB) ina majukumu ya kuandaa na kusimamia utekelezaji wa Sera za
Usimamizi wa Rasilimaliwatu katika Utumishi wa Umma; Taratibu, Miundo na Mifumo
ya Utoaji Huduma; Uendelezaji Rasilimaliwatu; Utunzaji wa Kumbukumbu na Nyaraka
katika Utumishi wa Umma. Aidha, Ofisi hii inasimamia maadili ya watumishi na
viongozi wa umma; mapambano dhidi ya
rushwa; Mfuko wa Maendeleo ya Jamii; Mpango wa Kurasimisha Rasilimali na
Biashara za Wanyonge; Mfuko wa Rais wa Kujitegemea; na Taasisi ya Uongozi.
Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Ofisi
ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma.

No comments:
Post a Comment