Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na
Utawala Bora, Mhe. Angellah J. Kairuki (Mb) akitoa taarifa kwa
Vyombo vya Habari kuhusu zoezi la kuondoa watumishi hewa katika orodha ya
malipo ya mishahara serikalini ofisini kwake mapema leo.( Picha zote na Hussein Makame-Maelezo)
Baadhi ya waandishi wa habari wakimsikiliza Waziri wa Nchi, Ofisi
ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Angellah
J. Kairuki (Mb) alipozungumza leo ofisini kwake jijini Dar es Salaam.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na
Utawala Bora, Mhe. Angellah J. Kairuki (Mb) akifafanua jambo kwa
waandishi wa habari (hawako pichani) kuhusu utekelezaji wa agizo la kuondoa
watumishi hewa katika orodha ya malipo ya mishahara Serikalini ofisini kwake
mapema leo.
Na Hussein Makame-MAELEZO
WAAJIRI 264
kati ya waajiri wote 409 Serikalini wamewasilisha taarifa zao kuhusu kuwepo kwa
watumishi hewa ambapo kati ya waajiri hao waajiri 63 wamethibitisha kwamba
hawana watumishi hewa katika Taasisi zao.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya
Utumishi Wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Angellah Kairuki (MB), amebainisha hayo
wakati alipozungumzia na waandishi wa habari ofisini kwake jijini Dar es Salaam
na kuongeza kuwa waajiri 201 wana watumishi hewa kuanzia mmoja na kuendelea.
“Waajiri
264 kati ya waajiri wote 409 wamewasilisha taarifa zao kuhusu uwepo wa
watumishi hewa. Kati ya waajiri 264 waliowasilisha taarifa zao, waajiri 63
wamethibitisha kwamba hawana watumishi hewa katika Taasisi zao na waajiri 201
wana watumishi hewa mmoja (1) na kuendelea.” Alisema Waziri Kairuki.
Hata hivyo,
alisema zipo taasisi 145 ambazo hazijawasilisha taarifa iwapo zina watumishi
hewa au la ikiwemo Mabaraza 11, Bodi 10, Vyuo Vikuu 25, Hospitali 3 na Ofisi za
Makatibu Tawala wa Mikoa 12.
Alizitaja taasisi
nyingine kuwa ni Mamlaka 6, Tume 10, Mamlaka za Serikali za Mitaa 38, Taasisi za Umma na Wakala 30 ambapo
aliziagiza Taasisi zote ambazo hazijawasilisha taarifa za watumishi hewa
kufanya hivyo kabla au ifikapo tarehe 26 Agosti mwaka huu.
Waziri
Kairuki alieleza kuwa kuanzia Agosti 15 mwaka huu, ofisi yake ilianza zoezi la uhakiki
wa kushtukiza katika taasisi sabini za Serikali zikiwepo Wizara, Idara za
Serikali Zinazojitegemea na kwamba zoezi hilo linaendelea.
Aliongeza
kuwa uhakiki wa kustukiza utafanyika pia kwenye Sekretarieti za Mikoa, Mamlaka
za Serikali za Mitaa na Taasisi za Umma kwa madhumuni ya kujiridhisha kwamba
taarifa za watumishi hewa zilizowasilishwa na waajiri ni sahihi.
Alibainisha
kuwa katika kufanikisha uhakiki huo, Ofisi yake imechukua hatua kadhaa ikiwemo
kuendelea kutoa mafunzo ya mara kwa mara kwa Maafisa Utumishi wenye dhamana ya
kutumia mfumo wa malipo ya mshahara kukuza uwajibikaji kwa maafisa wanaosimamia
malipo ya mishahara kwa kuwachukulia hatua za kinidhamu au kisheria
wanaobainika kusababisha watumishi hewa.
“Aidha
ofisi yangu pia inafanya uhakiki wa kushtukiza na kuanza safari ya kuunganisha
Mfumo wa Malipo ya Mishahara na mifumo mingine mikubwa kama ya NIDA, RITA na
Baraza la Mitihani la Taifa, na kuwezesha mfumo kuwaondoa moja kwa moja
(automatically) watumishi waliofikisha umri wa kustaafu kwa lazima.” alisema.
Waziri Kairuki atatoa taarifa
kamili ya watumishi hewa baada ya kupata taarifa hizo kutoka kwa waajiri ambao
hawajawasilisha taarifa hizo na kukamilika kwa zoezi la uhakiki wa Taasisi
sabini (70) linaloendelea sasa.
“Hivyo naagiza Taasisi
zote ambazo hazijawasilisha Taarifa za Watumishi Hewa kufanya hivyo kabla au
ifikapo tarehe 26 Agosti, 2016.” Alisema Waziri Kairuki.
Alisema kuwa ofisi yake
itawasilisha taarifa rasmi ya watumishi hewa kwa Mheshimiwa Rais ikiwa na orodha
na majina ya Taasisi ambazo zimewasilisha taarifa ya watumishi hewa na na zile
ambazo hazijawasilisha taarifa hizo.
Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli mnamo Machi 15 mwaka
huu aliwaagiza Wakuu wa Mikoa na Waajiri wote kwa ujumla kuchukua hatua ya
kuhakikisha katika Mikoa au Taasisi zao hakuna watumishi hewa ifikapo tarehe 30
Machi, 2016.
Katika
kutekeleza agizo hilo Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala
Bora imekuwa ikifuatilia utekelezaji wa agizo hilo na mnamo Mei 26 mwaka huu waajiri wote waliagizwa
kuwasilisha taarifa za mwisho za zoezi la kuwabaini na kuwaondoa watumishi hewa
katika orodha za malipo ya mshahara (payroll) ifikapo mwisho wa Mwezi Juni,
2016.
Waajiri
walitakiwa kutuma jina la Taasisi, Fungu la Taasisi (Vote), namba ya
Utambulisho ya Mtumishi wa Umma (Cheki Namba), jina kamili la mtumishi; cheo
cha mtumishi, jina la tawi la Benki ambalo mshahara wa mtumishi umekuwa
ukipitishwa au ukilipwa.
Taarifa
nyingine zinazotakiwa kutumwa ni hatua zilizochukuliwa na mwajiri dhidi ya
watumishi hewa waliobainika kama kurejesha fedha, na Maafisa wengine wa Taasisi
husika waliosababisha uwepo wa Watumishi hao kuwachukulia wahusika hatua za
kinidhamu au kisheria.
Nyingine ni
namba ya akaunti ya Benki ya mtumishi, tarehe ambayo mtumishi aliondolewa
kwenye mfumo wa taarifa ya Kiutumishi na Mshahara, kiasi cha fedha zilizolipwa
kwa mtumishi husika tangu alipotakiwa kuondolewa hadi tarehe aliyoondolewa kwenye
mfumo na sababu ya kuondolewa kama utoro, kufariki dunia, kuacha kazi, kustaafu
na sababu nyingine.

No comments:
Post a Comment