TANGAZO


Monday, June 27, 2016

WAGANGA WA TIBA ASILI WATAKIWA KUJISAJILI

Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Hamis Kigwangalla.

Na Lilian Lundo – MAELEZO – Dodoma
27/06/2016
WAGANGA wa tiba asili ambao wamekuwa wakitoa huduma ya tiba pasipo kujisajili wametakiwa kujisajili Baraza la Tiba Asili na Tiba Mbadala ili waweze kutambulika kisheria.

Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Hamis Kigwangalla ameyasema hayo leo, Bungeni Mjini Dodoma alipokuwa akijibu swali la nyongeza la Mbunge Viti Maalum Mhe. Zainabu Mussa Bakar juu ya udanganyifu unaofanywa na waganga wa tiba asili wa kutoa dawa feki kwa wagonjwa.

“Waganga wa tiba asili wapo kisheria, ni kweli wapo wanaotoa dawa feki, na wengi wao ni wale ambao hawajasajiliwa, hivyo tumewaagiza kujisajili ili tuweze kuwatumbua na dawa zao ziweze kuhakikiwa na kusajiliwa kwa ajili ya matumizi ya binadamu,” alifanunua Mhe. Kigwangalla.

Mhe. Kigwangalla amesema kuwa, mganga yoyote atakaye kiuka agizo hilo la kujisajili basi hatua kali zitachukuliwa dhidi yake. Aidha, amesema Wizara iko makini na ufuatiliaji wa dawa feki nchini kwani wanapopata fununu ya uwepo wa dawa feki hutuma kikosi kuchunguza na ikibainika kuwa dawa ni feki basi hatua kali huchukuliwa kwa muhusika.

Aliendelea kwa kusema kuwa, ili kudhibiti uingizwaji wa dawa feki nchini Wizara hiyo hufanya uhakiki wa muda mrefu kuchunguza iwapo dawa inayopendekeza kuingia nchini siyo feki na inafaa kwa matumizi ya binadamu, ikiwa dawa haina madhara yoyote basi inasajiliwa kwa ajili ya kuingia sokoni.

Vilevile Mhe. Kigwangalla amesema kuwa, Wizara imewaagiza waganga wa tiba asili kufunga dawa zao kwa kutumia vifungashio maalum vya madawa ambavyo vitasaidia dawa hizo kuendelea kuwa salama kwa mtumiaji kwa kipindi kilichopangwa kutumika.

BUNGE LIMEPITISHA MUSWADA WA MAREKEBISHO YA SHERIA YA ELIMU

Mwanasheria Mkuu wa Serikali Mhe. George Masaju

Na Lilian Lundo – MAELEZO – Dodoma
27/06/2016.
BUNGE la Jamhuri wa Muungano wa Tanzania leo, Mjini Dodoma limepitisha muswada wa marekebisho ya sheria ya Elimu kifungu kinachoeleza kuwa mtu anayempatia ujauzito mwanafunzi wa shule ya msingi au sekondari kuwa adhabu yake ni faini isiyozidi shilingi laki tano au kifungo kisichozidi  miaka mitatu.

“Muswada unapendekeza kuwa kifungu hicho kifutwe na badala yake kitungwe kifungu kipya cha 60A ili kuweka masharti yanayojitosheleza kuhusu zuio la kuoa au kumpatia ujauzito mwanafunzi wa shule ya msingi au Sekondari, kinapendekeza adhabu yake iwe kifungo cha miaka 30 gerezani,” alifafanua Mwanasheria Mkuu wa Serikali Mhe. George Masaju.

Vile vile mtu atakayebainika kusaidia, kushawishi au kuacha mwanafunzi wa shule ya msingi au sekondari kuolewa au kuoa anatenda kosa la jinai ambalo adhabu yake ni faini isiyopungua shilingi milioni tano au kifungo cha miaka mitano gerezani au vyote kwa pamoja.

Mhe. Masaju aliendelea kwa kufafanua kuwa, sheria hiyo imependekeza kuwa pale ambapo kosa hilo litafanywa na mtoto basi adhabu yake itakuwa kwa mujibu wa masharti ya sheria ya mtoto. Hii ni kwa sababu sheria ya mtoto inakataza mtoto anayetiwa hatiani kufungwa gerezani.

Aidha marekebisho hayo katika sheria ya Elimu yanalenga kumjengea mwanafunzi wa shule ya msingi au sekondari mazingira mazuri ya kumaliza ipasavyo elimu yake kwa ngazi hiyo.Hivyo basi kila Mkuu wa shule au Mwalimu Mkuu atawasilisha kwa Kamishna wa Elimu taarifa ya robo mwaka kuhusu matukio ya ndoa na mimba kwa wanafunzi katika shule yake na hatua zilizochukuliwa.

Sheria ya Elimu inamruhusu mwanafunzi aliyepewa ujauzito kuendelea na masomo mara tu anapojifungua. Sheria hiyo inasubiri kuwekwa saini na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt John Pombe Magufuli ili ianze kutumika.

No comments:

Post a Comment