· Mwenyekiti wa Bodi ya Ofisi ya Taifa ya Takwimu,
·
Viongozi kutoka Serikalini,
·
Mwakilishi kutoka USAID,
·
Wawakilishi kutoka Mashirika ya Umoja
wa Mataifa,
·
Wadau Wengine wa Maendeleo,
·
Wawakilishi kutoka Sekta Binafsi,
·
Wadau kutoka Vyuo vya Elimu ya Juu,
·
Waandishi
wa Habari,
·
Wageni Waalikwa,
·
Mabibi
na Mabwana.
Ndugu Mwenyekiti, awali ya yote napenda kumshuru Mungu kutumia
fursa hii kuwashukuru wote kwa kuitikia mwaliko na kuungana na Wizara yangu kwa
lengo la kuzindua Matokeo Muhimu ya Utafiti wa Afya ya Uzazi na Mtoto na
Viashiria vya Malaria wa Mwaka 2015, yaani "2015-16
Tanzania Demographic and Health Survey and Malaria Indicator Survey".
Aidha, napenda niwashukuru
waandaaji wa hafla hii kwa kunialika kufanya uzinduzi wa tukio hili muhimu. Kama
mnavyofahamu, Sekta ya Afya ni miongoni mwa Sekta muhimu sana katika jamii yetu
katika kuchangia uboreshaji wa uchumi wa Nchi na kupunguza Umaskini. Ni dhahiri kuwa, ukiwa na taarifa sahihi za
afya za Wananchi, ni fursa ya pekee ya kuboresha na kuimarisha ustawi wa uchumi
wa Taifa letu.
Ndugu Mwenyekiti, kutokana na matokeo ya utafiti huu tunapata takwimu za kutathmini
utekelezaji wa mipango mbalimbali ya Serikali katika kufikia malengo
iliyojiwekea ikiwemo yale ya Kitaifa na Kimataifa.
Taarifa hizi zitaisadia Wizara yangu,
watunga sera, waratibu wa miradi na wadau wengine katika kufuatilia na kufanya
tathmini ya miradi iliyopo, na kujua miradi ipi inatekelezeka na ipi ambayo bado
ina changamoto ili pale inapobidi tujiandae upya na kuainisha mikakati mipya
kuhusiana na taarifa za Sekta ya afya hapa Nchini.
Ndugu Mwenyekiti, binafsi nimepata wasaa wa kuipitia Ripoti ya Matokeo Muhimu ya Utafiti
huu na kutokana na nilichosoma, naweza kusema kuwa, kuna mambo mengi katika
matokeo haya ambayo tunaweza kupongezana kwayo. Lakini pia kuna maeneo ambayo
bado kuna changamoto na hivyo tunahitaji kujitathmini.
Kwa mfano, maeneo tuliyofanya vizuri
ni:
·
Kuendelea
kupungua kwa vifo vya watoto wachanga, yaani chini ya mwaka mmoja kutoka vifo 51
kati ya watoto 1,000 waliozaliwa hai katika Utafiti wa mwaka 2010 kufikia vifo 43
mwaka 2015/16.
·
Kuendelea
kupungua kwa vifo vya watoto chini ya miaka mitano kutoka vifo 81 mwaka 2010 na
kufikia vifo 67 mwaka 2015.
Kupungua kwa vifo hivi kumewezesha serikali
kutimiza lengo la Nne (4) katika yaliyokuwa Malengo ya Millenia ya 2015:
·
utafiti
huu umetuonyesha kuongezeka kwa matumizi ya njia za uzazi wa mpango ambapo
kiwango cha utumiaji wa njia za uzazi kwa wanawake walio kwenye ndoa au
wanaoishi na wenza wao kimefikia asilimia 38 kutoka asilimia 29 Mwaka 2010.
Asilimia 32 ya wanawake hawa katika
utafiti huu wa 2015/16 wanatumia njia za kisasa za uzazi wa mpango na asilimia
6 wanatumia njia za asili mwaka 2010. Ongezeko
la matumizi ya njia za uzazi wa mpango ni dalili nzuri inayoashiria uwezekano
wa kushuka kwa kiwango cha uzazi pamoja na kuongezeka nafasi ya uzazi kati ya
watoto.
Taarifa nyingine ambazo zimetokana na
juhudi za makusudi za Serikali ni kiwango kikubwa cha akina mama wajawazito
wanaohudhuria kliniki na kuhudumiwa na mtaalamu aliyesomea (asilimia 98):
·
Kuongezeka
kwa kiwango cha akina mama wanaojifungulia katika vituo vya kutolea huduma ya afya,
kutoka asilimia 51 mwaka 2010 kufikia asilimia 60 mwaka 2015 na kuongezeka kwa
kiwango cha akina mama wanaosaidiwa na wataalam waliosomea wakati wa kujifungua
kutoka asilimia 50 kufikia asilimia 60 mwaka 20015/16.
·
Matokeo
mengine muhimu ni kupungua kwa kiwango cha watoto waliodumaa kutoka asilimia 42
ya watoto walio chini ya miaka mitano katika Utafiti wa mwaka 2010 na kufikia
asilimia 34 kwa mwaka 2015/16.
Ndugu Mwenyekiti, ni dhahiri kuwa matokeo niliyoyataja yanatokana na juhudi mbalimbali
zinazoendelea kufanywa na Serikali katika kuwaletea Wananchi huduma bora za
afya na zilizo karibu na maeneo wanayoishi na ikichangiwa na mpango wa Serikali
katika kuhakikisha kuwa kunakuwa na Zahanati kila Kijiji na Kituo cha Afya kila
Kata.
Kama mtakumbuka vyema, matokeo ya Utafiti
wa Kutathmini Utoaji wa Huduma za Afya Nchini (Tanzania Srvice Provision Assessment Survey TSPA) uliofanyika
mwaka 2014/15 yalionesha kuongezeka kwa upatikanaji na utoaji wa huduma mbali
mbali za afya ikiwemo huduma kwa matibabu ya watoto na kuongezeka kwa vituo
vinavyotoa huduma za uzazi wa mpango.
Kwa huduma za kisasa za uzazi wa mpango
ilionekana kuwa asilimia 80 ya vituo vyote vinavyotoa huduma za afya vinatoa
huduma hii ya Uzazi wa Mpango. Kwa upande wa huduma zinazohusiana na Afya ya
Uzazi wa Mama na Mtoto, matokeo yalionesha kuwa asilimia 85 ya vituo vyote
vinatoa huduma zinazohusiana na Afya ya Uzazi wa Mama na Mtoto
Ndugu Mwenyekiti, pamoja
na matokeo haya mazuri, Utafiti umeonesha kuwa kuna baadhi ya maeneo yanapaswa kuangaliwa
upya na kutiliwa mkazo zaidi. Kwa mfano:- kupitia Utafiti huu tunaona kuwa kwa sasa wanawake Nchini Tanzania wanazaa wastani wa watoto
watano (5) katika vipindi vyao vya uzazi. Kwa kweli kiwango hiki bado ni
kikubwa.
-
Wastani wanawake wa vijijini huzaa
watoto wawili zaidi ya wanawake wanaoishi mijini. Yaani watoto Sita kwa
wanawake wa vijijini na watoto Wanne kwa Wanawake wa Vijijini.
Bado juhudi
zaidi za Serikali na wadau wengine zinahitajika hasa maeneo ya vijijini ili
kuweza kuondoa tishio la ongezeko kubwa la watu hapo baadae. Katika matokeo
haya pia tunaona ongezeko la mimba kwa wasichana wadogo. Utafiti wa 2015/16 umeonyesha
kuwa asilimia 27 ya wasichana wa miaka 15-19 wameshaanza kuzaa, hii ikiwa
imeongezeka kutoka asilimia 23 katika Utafiti wa mwaka 2010. Hii sio taarifa
nzuri kwani inatishia kuongezeka kwa idadi ya wasichana wanaokatisha masomo na
hivyo kuongezeka kwa umaskini. Aidha watoto ambao huzaliwa na wasichana hawa wadogo
wana uwezekano mkubwa kupoteza maisha ukilinganisha na wengine.
Hivyo, bado
tunahitajika kutoa elimu zaidi ili kupunguza kiwango hiki na kuwezesha watoto
wetu wa kike waweze kupata muda wa kusoma na kujiendeleza katika kujiandaa na
maisha.
Hivyo Serikali
itaendelea kutoa elimu juu ya madhara yanayoweza kutokea kwa wasichana kuzaa
wakiwa bado wadogo. Aidha, serikali in ania ya makusudi ya kuhakikisha Sheria
na Ndoa inafanyiwa marejeo ili kuhakikisha baadhi ya changamoto hizo
zinashughilikiwa.
Ndugu Mwenyekiti, utafiti
huu pia uliangalia kiwango cha maambukizi ya Malaria kwa watoto chini ya mwaka
mmoja, na wote tunatambua kuwa Malaria bado ni mojawapo ya magonjwa yanayoongoza
kwa kusababisha vifo Tanzania na inachangia pia asilimia kubwa ya vifo vya
watoto na akina mama wajawazito.
Utafiti huu
unaonyesha kuwa asilimia 14 ya watoto wa chini ya miaka 5 ambao walipimwa Malaria
kwa kutumia kipimo cha kutoa matokeo kwa haraka yaani Rapid Diagnostic Tests (RDT) walikuwa na Malaria. Kiwango hiki ni
kikubwa ikilinganishwa na kiwango kilichopatikana wakati wa Utafiti wa UKIMWI
na Malaria wa Mwaka 2011-12.
Japokuwa
yawezekana ongezeko hili linatokana na vipindi tofauti vya kufanya utafiti
katika tafiti hizi mbili, bado hatuwezi kukwepa ukweli kuwa Malaria bado ni
tishio kwa watoto wetu na Wananchi kwa ujumla.
Hivyo nitoe rai
kwa wenzangu katika Serikali na wadau wetu wa Maendeleo kuwa bado tunapaswa
kuendelea na juhudi zilizopo za kuhakikisha Malaria inamalizwa hapa Tanzania.
Natambua Mpango
wa Kudhibiti Malaria Tanzania (NMCP) upo katika utekelezaji wa awamu ingine ya
kusambaza vyandarua katika Kaya za Tanzania, na ni mategemeo yangu kuwa
vitatumiwa kama ilivyokubaliwa tunategemea juhudi hizi na nyingine zinazofanywa
na wadau wengine zitachangia kupunguza kiwango cha Malaria.
Hata hivyo
mapambano dhidi ya malaria ni ya kila mmoja wetu, kila mtu kwa nafasi yake
anapaswa kutekeleza ushauri wa wataalam ili kujiepusha na kupata Malaria mfano
matumizi ya vyandarua vyenye dawa, kukata majani na kuzuia madimbwi ya maji
kwenye makazi yetu.
Ndugu Mwenyekiti, nimegusia tu baadhi ya viashiria lakini natambua kuwa hali halisi ya
viashiria muhimu vya afya kutoka katika ripoti hii itawasilishwa na watoa mada
walioandaliwa hapo baadae kidogo na pia mtaweza kusoma katika ripoti ambayo nimetaarifiwa
mtapewa hivi punde. Hivyo, niwaombe msikilize vizuri mada hizo na pale ambapo
mtaona kunahitajika uchambuzi wa namna ya kipekee basi msisite kutoa taarifa
kwa wahusika na hii itachangia katika kuboresha taarifa ya kina ya hapo baadae
mwezi Oktoba 2016.
Ndugu
Mwenyekiti, Utafiti huu,
kama zilivyo tafiti nyingine nyingi unatupatia matokeo muhimu ambayo yanaakisi hali
halisi ilivyo katika mfumo wetu mzima wa afya. Ni jukumu letu sote kama wadau
kuweka mikakati ya namna ya kukabiliana na changamoto mbalimbali katika maeneo yetu
ya kazi. Kwa mantiki hiyo, napenda nitoe wito kwa Wadau wote wa Sekta ya Afya
Nchini na Wadau wote kwa ujumla kuyachukulia matokeo haya kama chachu ya kitaifa katika kuboresha utoaji wa huduma za
afya Nchini.
Wananchi pia watimize wajibu wao kwa mfano akina mama kunyonyesha watoto
kama inavyoshauriwa, kwenda kliniki kabla na baada ya kujifungua, n.k.
Kwa kuelewa hayo tunatakiwa sote kufanya kazi kwa pamoja na kwenda sambamba
na kauli mbiu ya awamu ya Tano ya HAPA
KAZI TU ili kufikia malengo yaliyokusudiwa katika kuboresha huduma za afya
na maisha kwa ujumla. Niombe kuwa sote kwa pamoja kutumia takwimu hizi ambazo
ni rasmi kwa ajili ya kupanga sera na mipango bora.
Ndugu
Mwenyekiti, kabla ya kufikia
tamati, napenda kutambua michango mbalimbali iliyowezesha kukamilika kwa utafiti
huu. Nianze kwa kuishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa
kuona umuhimu wa kufanya Utafiti huu.
Pili, kuwashukuru wataalam kutoka Wizara zote zilizoshiriki, waratibu,
wasimamizi, wadadisi na Wananchi kwa ujumla kwa kuwezesha kufanyika kwa kazi
hii.
Tatu, napenda
kutambua juhudi zilizofanyika chini ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii,
Jinsia, Wazee na Watoto, Wizara ya Afya - Zanzibar:
·
Wataalam kutoka Shirika la Macro la
Marekani, na pia niwashukuru Shirika la
·
Misaada
la Marekani (USAID),
·
Idara
ya Mambo ya Nje,
·
Biashara
na Maendeleo (Glabal Affairs Canada),
·
Ubalozi
wa Ireland,
·
Shirika
la Umoja wa Mataifa linahusika na idadi ya watu (UNFPA),
·
Shirika
la Umoja wa Mataifa linaloshughulika na Watoto (UNICEF) kwa kutoa msaada wa
fedha zilizotumika kutekeleza utafiti huu
·
wadau
wengine wa afya kwa kutoa raslimali fedha na wataalam na ufuatiliaji mzima wa utafiti
huu.
Niwashukuru pia Wananchi waliofikiwa
na wataalam na kutoa taarifa za Utafiti huu na tunaomba muendelee na moyo huu
kwani takwimu hizi zinasaidia Serikali katika kuwaletea wananchi huduma za afya
na ustawi wa maisha ujumla.
Ndugu Mwenyekiti, napenda kutumia nafasi hii kwa mara
nyingine kutoa wito kwa wadau wote kuwa dhana hasi iliyojengeka kwenye jamii
kuhusu matumizi ya takwimu kwamba Serikali ndio inayotumia takwimu tuifute na
naomba kwamba wadau wote wa Afya tutumie takwimu hizi ili tuboreshe huduma
zaidi na kuongeza uchumi wa Nchi.
Vitabu hivi vitumike ipasavyo, visiviweke
kwenye makabati ya vitabu. Visomwe kwa makini na kuchambua kwa kina ili kupata
majibu ya kukabiliana na changamoto zilizopo za upatikanaji wa taarifa za afya.
Wizara kwa kushirikiana na Ofisi ya
Taifa ya Takwimu na wadau wengine tutafanya kila linalowezekana ili kumaliza
uchambuzi wa kina wa taarifa za Utafiti huu ikiwemo taarifa kuhusiana na Vifo
vinavyotokana na uzazi, na kuzitoa hapo mwezi Oktoba 2016 kama ilivyoelezwa
awali.
Baada ya maelezo hayo, napenda
kutamka rasmi kuwa, TAARIFA YA MATOKEO MUHIMU YA UTAFITI WA WA AFYA YA UZAZI NA
MTOTO NA VIASHIRIA VYA MALARIA MWAKA 2015/16 IMEZINDULIWA RASMI.
Niwatakieni majadiliano mema
yatakayoboresha Sekta ya Afya Nchini.
Asanteni kwa Kunisikiliza.

No comments:
Post a Comment