Kaimu Mtendaji Mkuu TEMESA Mhandisi Manase Lekujan akiongea na waalimu pamoja na wahitimu wa mafunzo ya teknolojia ya Umeme wa Jua (Solar Photovoltaic Technology).
Mhandisi Amani Mwanga akipokea cheti kutoka kwa Kaimu Mtendaji Mkuu TEMESA baada ya kuhitimu mafunzo ya teknolojia ya umeme wa jua (Solar Photovoltaic Technology).
Mhandisi Sara Moses akipokea cheti kutoka kwa Kaimu Mtendaji Mkuu TEMESA baada ya kuhitimu Mafunzo ya teknolojia ya umeme wa jua (Solar Photovoltaic Technology).
Wahitimu wa Mafunzo ya teknolojia ya umeme wa jua (Solar Photovoltaic Technology) kutoka TEMESA wakiwa kwenye picha ya pamoja.
Na Theresia Mwami
KAIMU Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi na Umeme(TEMESA) Mhandisi Manase Le-Kujan, leo Ijumaa Tarehe 22/04/2016 amefunga mafunzo ya umeme wa jua (Solar Photovoltaic Technology) kwa watumishi wa TEMESA.
Mafunzo hayo yaliyofanyika kwa wiki mbili, yametolewa na chuo kikuu cha Dar es Salaam kitengo cha Fizikia, kwa watumishi 20 wa TEMESA.
Katika hotuba yake Mhandisi Manase aliushukuru uongozi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kwa kuendesha mafunzo hayo kwa wataalamu wa TEMESA, aliongeza kuwa.
“Nishati ya umeme wa jua imeshika kasi kwa sasa na inatumiwa sana katika maeneo ambayo umeme wa kawaida haujafika hivyo basi kwa mafunzo haya wahandisi na mafundi wetu wataweza kushirikiana na wadau mbalimbali katika kuandaa na kutekeleza miradi itakayosaidia kuondokana na tatizo la umeme nchini.” Alisema Mhandisi Manase.
Aidha, TEMESA inasimamia miradi mbali mbali ya teknolojia ya umeme wa jua nchini ikiwemo; mfumo wa teknolojia ya umeme wa jua kwa shirika la utangazaji Tanzania (TBC) Songea, mfumo wa teknolojia ya umeme wa jua katika ofisi ya Rais Utumishi, kusimamia na kuhakiki mifumo ya teknolojia ya umeme wa jua inayofungwa vijijini katika mikoa ya Geita, Kigoma Ruvuma na Tabora iliyo chini ya REA, kusimamia matengenezo ya mifumo ya teknolojia ya umeme wa jua katika ofisi zote za TRA pamoja na miradi mbali mbali ya taa za kuongozea magari barabarani zinazotumia teknolojia ya umeme wa jua.

No comments:
Post a Comment