Kaimu Mtendaji wa Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) Mhandisi Manase Ole Kujan (katikati) akiangalia moja ya kifaa cha kupimia umeme kinachotumika katika mafunzo kwa wahandisi na mafundi wa Temesa yaliyofunguliwa leo.
Mhandisi Amani Mwanga akitoa maelekezo ya namna ya kufunga moja ya mitambo ya umeme wa nishati ya jua (Solar) Katika mafunzo ya wahandisi na mafundi wa Temesa yaliyofunguliwa leo.
Fundi Sanifu kutoka Temesa Mganza Juma (Katikati), akiwa makini kufunga moja ya mtambo wa umeme wa nishati ya jua (Solar) katika mafunzo ya wahandisi na mafundi wa Temesa yaliyofunguliwa leo.
Baadhi ya wahandisi kutoka Temesa wakiwa katika harakati za kuchuna na kuunga nyaja katika moja ya mitambo ya umeme wa nishati ya jua (Solar) Katika mafunzo ya wahandisi na mafundi wa Temesa yaliyofunguliwa leo.
Na Raymond Mushumbusi MAELEZO
WAKALA wa Ufundi na Umeme (TEMESA) ikishirikiana na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam wanaendesha mafunzo ya wiki mbili kwa Wahandisi na mafundi wa Temesa ili kuwajengea uwezo katika kutumia teknolojia ya umeme wa nishati ya jua.
Akifungua mafunzo hayo leo Jijini Dar es Salaam Kaimu Mtendaji Mkuu TEMESA Mhandisi Manase Ole Kujan amesema lengo la mafunzo hayo ni kuwaongezea uwezo wahandisi na mafundi ili kuweza kutumia teknolojia ya umeme wa nishati ya jua ambao umekuwa na tija kubwa hasa kwa sehemu ambazo umeme wa kawaida haujafika.
“Nishati ya umeme wa jua imeshika kasi kwa sasa na inatumiwa sana katika maeneo ambayo umeme wa kawaida haujafika hivyo basi kwa mafunzo haya wahandisi na mafundi wetu wataweza kushirikiana na wadau mbalimbali katika kuandaa na kutekeleza miradi itakayosaidia kuondokana na tatizo la umeme nchini.” Alisema Mhandisi Manase.
Akizungumza mara baada ya ufunguzi wa mafunzo,Mratibu wa mafunzo hayo kutoka Chuo Kikuu Dar es Salaam Prof Cathbert Kimambo amesema kwa kushirikiana na Temesa wameamua kutoa mafunzo kwa wataalamu hao juu ya teknolojia ya nishati ya umeme wa jua ili kuwasaidia kuendana na mabadiliko ya teknolojia kwa kuwa na utalaamu na uwezo wa kufanya kazi kulingana na mabadiliko yaliyopo.
Mmoja wa wahandisi Kutoka Temesa Bi Sara Moses ametoa wito kwa Wahandisi wengine kuwa na utaratibu wa kujifunza na kuongeza utaalamu ili kuwezesha kuendana na mabadiliko Sayansi na Teknolojia katika kuleta ufanisi katika kazi zao.

No comments:
Post a Comment