TANGAZO


Saturday, April 16, 2016

Rais Magufuli afungua rasmi mradi wa ujenzi wa Barabara ya juu eneo la Tazara

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Magufuli, akizungumza na Watanzania kabla ya kufungua na kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa mradi wa Barabara ya juu kwenye makutano, eneo la Tazara jijini Dar es Salaam leo. (Picha zote na Raymond Mushumbusi Maelezo)
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Magufuli, akifunua pazi ili kuweka jiwe la msingi kwa ajili ya ujenzi wa mradi wa Barabara ya juu makutano ya Tazara jijini Dar es Salaam leo. 
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Magufuli, akifungua ramani ya mradi wa Barabara ya juu makutano ya Tazara kuashiria ufunguzi rasmi na kuanza kwa ujenzi  wa mradi huo Tazara jijini Dar es Salaam leo. 
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Magufuli, akipokea maelekezo kuhusu mradi wa ujenzi wa Barabara za juu eneo la makutano la Tazara kutoka kwa Mkurugenzi Mkuu wakala wa barabara (TANROADS) Mhandisi Patrick Mfugale katika ufunguzi rasmi wa mradi huo jijini Dar es Salaam leo.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Magufuli, akikata utepe kuashiria ufunguzi rasmi na kuanza kwa ujenzi  wa mradi wa Barabara ya juu makutano ya barabara za Nyerere na Mandela, eneo la Tazara jijini Dar es Salaam leo.  
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Magufuli, akiwa katika picha ya pamoja na viongozi mbalimbaliwa wa Kitaifa na Kimataifa wakati wa ufunguzi rasmi na kuanza kwa ujenzi  wa mradi wa barabara ya juu katika makutano ya Tazara jijini Dar es Salaam leo. 

Na Lorietha Laurence-Maelezo
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Dk. John Pombe Magufuli ameweka jiwe la msingi ikiwa ni ufunguzi rasmi wa  ujenzi wa mradi wa barabara za juu (fly over) katika eneo la tazara utakaosaidia kupunguza  msongamano wa foleni  katika jiji la Dar es Salaam kwa asilimia 80.

Akizungumza wakati wa  hafla hizo   Mhe.Dk.magufuli ameeleza kuwa mradi unakadiriwa kugharimu kiasi cha shilingi, Bilioni 100, na unatarajiwa kukamilika mwaka 2018  huku akiwataka wananchi kutunza miundombinu kwa kuhakikisha jiji linakuwa safi na lenye kuvutia.

"Mradi huu ni kwa ajili ya maendeleo ya watanzania hivyo ni jukumu letu sotu kuutunza ili udumu ukizingatia fedha hizi za mradi zimetokana na  walipakodi wa Japani wameamua kuleta kwetu hii ishara ya ushirikiano mzuri kwetu,"alisema.

Aidha aliongeza kuwa   mradi  huu umeshirikisha  serikali ya Tanzania na ile ya Japani amabayo  imechangia kiasi cha  Bilion 93.44 huku Tanzania ikichangia shilingi Bilion 8.36.

Anaongeza na kueleza kuwa  lengo la mradi huu ni kuhakikisha kero ya  foleni inapungua kama si kwisha kabisa ikiwa ni pamoja na kuokoa muda wa usafirishaji kutoka kutumia dakika 45 mpaka dakika 10 pale mradi utakapokamilika.

 Mradi huu wa barabara za juu  utatengeneza ajira kwa vijana wa kitanzania  kwa  kuwataka kuitumia fursa hiyo vyema kwa kuwa waaminifu katika  ajira hizo  ili kusaidia kumaliza mradi huo kwa wakati.

"Tuna imani kuwa kazi itafanyika kwa haraka maana hakuna sababu kwa kampuni kubwa kutoka japani ambayo inatengeneza barabara kubwa kuchukua muda mrefu kumaliza ujenzi hivyo bora umalizike haraka na watanzania waone matunda yake,"alisema Mhe. Dk.Magufuli.

Dk. Magufuli aliongeza kuwa serikali ina mpango mzuri katika kuleta maendeleo ambapo kuna miradi mingine mingi inafanyika ikiwemo kujenga barabara nyingine za kawaida za njia sita zenye kilomita 128 zitakazoanzia  daraja la Kigamboni hadi Chalinze na za juu tano tayari   wakandarasi 13 wameshajitokeza  kushindania zabuni .

Vilevile ameeleza  kuwa katika  bajeti ijayo ya mwaka wa fedha wa 2016/2017  kiasi cha Trilioni 1 kitatengwa  kwa ajili ya mradi wa kujenga reli ya kati  kutoka Dar es Salaam kwenda nchi  za jirani ili kurahisisha usafirishaji wa bidhaa mbalimbali zinazopitia  Bandarini .

Kwa upande wake, Waziri wa Ujenzi Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa amesema kuwa  kwa kiasi kikubwa kumalizika kwa ujenzi wa mradi wa barabara hizo za juu 'Fly Overs' kutasaidia kuokoa kiasi kikubwa cha fedha kilichokuwa kikipotea kutokana na kutumia muda mwingi katika  msongamano wa foleni.

Katika hatua nyingine Rais alisema fedha za miradi ya maendeleo zimeongezeka kutoka asilimia 27 hadi kufikia 40 na kuwaomba makatibu wakuu na watumishi wa umma kuwa wavumilivu kwa kuwa fedha za safari, posho na chai zitapelekwa kwenye miradi hiyo kwa ajili ya maendeleo ya taifa.

"Nawaomba makatibu wakuu na watumishi kujifunga mkanda katika kipindi hiki  ili tuweze kufikia malengo kwa kuelekeza fedha za chai,safari na posho katika miradi ya maendeleo ikiwemo kufufua shirika la dnege la Tanzania kwa  kununua ndege mpya tatu “alisema Mhe. Magufuli.

Watanzania wamechoka kuona uchungu hivyo tuwafanye waone furaha, tubadilike ili fedha ziweze kurudi kwa wananchi   wa chini, naamini wote tunalilia maendeleo hivyo tushirikiane na vyama vyote katika kuleta maendeleo,"aliongeza.

Mtendaji Mkuu wa Tanroads, Mhandisi Patriki Mfugale alisema lengo la mradi huo ni kupunguza msongamano wa magari katika barabara ya Mandela na Nyerere  kwa kufungua njia nne ili magari yasisimame kwenye foleni katika makutano hayo.

Naye Balozi wa Japani Nchini Tanzania, Balozi Masaharu Yoshida amesema Ushirikiano wa Tanzania na Japani umeanza tangu mwaka 1960 na utaendelea kuwepo  ambapo mradi huu ni kiashiria mojawapo cha kudhibitisha hilo.

No comments:

Post a Comment