Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Mchezo wa Vishale Tanzania( TADA) Bi. Redempta Mwebesa (katikati) akiongea na waandishi wa habari hawapo pichani leo jijini Dar es salaam kuhusu kuanza kwa mashindano ya Afrika mashariki , wa kwanza kulia ni Katibu mkuu wa chama hicho Bi. Subira Waziri na wa kwanza kushoto ni Afisa Habari wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT) Bi Najaha Bakari.
Waandishi wa Habari wakifuatilia kwa makini mkutano ulioandaliwa na viongozi wa Chama cha Mchezo wa Vishale Tanzania( TADA) hawapo pichani kuzungumzia kuhusu kuanza kwa mashindano ya Afrika mashariki yanayotarajiwa kuanza April 29 mwaka huu. (Picha zote na BMT)
Na Mwandishi wetu- BMT
MASHINDANO ya wazi ya Kitaifa na Kimataifa ya
Shirikisho la Mchezo wa Vishale Afrika Mashariki yanatarajiwa kufanyika April
29 mpaka Mei Mosi jijini Dar es salaam, Tanzania ikiwa kama mwenyeji wa
mashindano hayo.
Mashindano hayo yanatarajiwa kujumuisha nchi za
ukanda wa Afrika mashariki zikiwemo Tanzania kama mwenyeji, Kenya, Uganda,
Burundi na Ruanda huku Kenya ikiwa
bingwa mtetezi wa michuano hiyo.
Akizungumza hayo leo jijini Dar es salaam Katibu
Mkuu wa Chama cha Mchezo wa Vishale Tanzania (TADA) Bi. Subira Waziri amesema
kuwa Tanzania ni miongoni mwa nchi
zitakazoshiriki michuano hiyo ikiwa na mategemeo makubwa ya ushindi.
“Tuna matarajio ya kuibuka washindi katika michuano
hiyo kutokana na kujiandaa vya kutosha kwa upande wa mazoezi ukizingatia kuwa tuna
utayari na uzoefu wa mchezo huo” alisema Bi. Waziri.
Kwa upande wa Makamu Mwenyekiti wa TADA Bi. Redempta
Mwebesi amesema kuwa licha ya mashindano hayo kuanza mwezi huu pia wana ukosefu
wa Vifaa vya Michezo pamoja na gharama za kuweka kambi ili kujifua zaidi.
Aidha Bi. Mwebesi ameongeza kuwa wana ukosefu wa
pesa taslimu na vikombe vya kuwapa washindi kwa kuwa wanategemea viingilio
kutoka kwa washiriki wa mashindano hayo.
“Tunaomba wadhamini na wadau wa michezo wajitokeze
kutusaidia kudhamini michuano hii kwa
kutupa vifaa na gharama za kukaa kambini ili tuweze kujifua zaidi na kurudisha
heshima tuliyoipata mwaka 2014 kwa kuibuka washindi wa michuano hii” aliongeza
Bi. Mwebesa.
Pia Bi. Mwebesa ameongeza kuwa wana mikakati ya
kuanzisha na kukuza mchezo huo kuanzia mashuleni , vijijini na Tanzania kwa
ujumla ili kuweza kupanua na kuongeza ushindani wa mchezo huo nchini.

No comments:
Post a Comment