Aliyekuwa msimamizi wa mradi wa maendeleo wa Sweden Carl Ake Gerden (kulia) na Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi Tanzania akimkabidhi aliyekuwa mwenyekiti wa PAC Mhe. John Momose Cheyo (Kushoto) kitabu cha mabadiliko ya Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi Tanzania kwa miaka 10 ya Ushirikiano wa Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi Tanzania na Sweden.
Mhe. John Momose Cheyo (aliyekuwa Mwenyekiti wa PAC) akizungumza jambo baada ya kupokea zawadi ya kitabu cha mabadiliko ya Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi Tanzania kwa miaka 10 ya Ushirikiano wa Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi Tanzania na Sweden.
Makamu Mwenyekiti wa Shirika la CCAF Canada wa Ukaguzi wa Ufanisi na Usimamizi John Reed akiwasilisha mada ya Ukaguzi wa Ufanisi kwenye warsha ya Kamati za Bunge za Hesabu PAC na LAAC.
Washiriki wa warsha ya Kamati za Bunge za Hesabu PAC na LAAC wakisikiliza mada mbalimbali.
Washiriki wa warsha ya Kamati za Bunge za Hesabu PAC na LAAC wakiwa kwenye picha ya pamoja mara baada ya ufunguzi wa warsha hiyo.
Washiriki wa warsha ya Kamati za Bunge za Hesabu LAAC wakiwa kwenye picha ya pamoja mara baada ya ufunguzi wa warsha hiyo.
Washiriki wa warsha ya Kamati za Bunge za Hesabu PAC wakiwa kwenye picha ya pamoja mara baada ya ufunguzi wa warsha hiyo.
Mwenyekiti
wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) Mhe. Martin Msuha
(MB) akizungumza maneno ya shukrani
wakati wa ufunguzi wa warsha ya Kamati za Bunge za Hesabu mjini Morogoro.
Na Sarah Reuben (NAOT)
MDHIBITI na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ameshirikiana na
wadau wa maendeleo kutoka Ujerumani (GIZ) na Canada CCAF kuandaa mafunzo kwa
wajumbe wa kamati mpya za Bunge za Hesabu za Serikali ambazo ni Public Accounts Committee (PAC) na Local Authorities Accounts Committee (LAAC).
Akizungumza wakati wa mafunzo hayo,
Makamu Mwenyekiti wa Ukaguzi wa Ufanisi na Bunge wa Canada (CCAF) John Reed,
amesema Kamati za Usimamizi za Bunge za Hesabu za Serikali, zinatakiwa kupewa mafunzo
ya kutosha na muda mwingi wa kufanya kazi zake kwani zina wajumbe wapya ambao
lazima wapate changamoto na ndiyo sababu wameshirikiana na Ofisi ya Taifa ya
Ukaguzi wa Hesabu za Serikali kuendesha warsha hii hapa nchini ili
kuwasaidia viongozi hao kufanya kazi zao kwa ufanisi zaidi.
Naye Makamu Mwenyekiti wa PAC Mhe.
Aeshi Khalfan Hilaly (MB) alisema mafunzo haya ya siku tatu ni muhimu sana
kwa kamati hizi ambazo ndio zinaanza rasmi kutekeleza jukumu lao la usimamizi
kwa kutumia ripoti za CAG. Alieleza kuwa hivi karibuni wameshuhudia kupitia
kwenye vyombo vya habari CAG amekabidhi ripoti yake ya Ukaguzi wa Mwaka 2014/15
ambapo itakabidhiwa bungeni na kuanza kutumiwa na kamati hizi kwa uchambuzi na
usimamizi hivyo kuwepo mafunzo haya ni kipindi muafaka ili kuzipa ujuzi stahiki
kamati hizi.
Akizungumza katika ufunguzi wa mafunzo
hayo Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali Prof. Mussa Assad (CAG)
alisema ofisi yake imekuwa ikifanya mahusiano mazuri na CCAF ya Canada kwa
ajili kuzijengea uwezo kamati hizo mbili nchini. “Tunatoa mafunzo kwa kamati
hizi ili wawe na mbinu za kuhoji matumizi ya fedha za wananchi na kuwasilisha
taarifa husika mahala husika,” alisema Prof. Assad.
Aidha CAG Prof. Assad aliongeza
kuwa ni muhimu kwa Spika wa Bunge kuona ombwe ya usimamizi wa Mashirika ya Umma
na hiyo kurejesha au kuunda kamati ya usimamizi nyingine ili kuwezesha shughuli
zilizokuwa zikifanywa na kamati ya POAC zikaweza kuendelezwa. “Tunafahamu umuhimu
wa kamati hiyo, leo tunaona umuhimu wa kazi zilizokuwa zikifanywa na kamati
iliyovunjwa, hivyo Bunge linapaswa kuzingatia uamuzi unaofanywa,” alisema. Prof.
Assad.
Pia, Prof. Assad aliwataka wabunge
kuangalia upya Sheria ya Bajeti na kuunga mkono mapendekezo ya Ofisi yake ya
kurekebisha kifungu cha 68 cha sheria hiyo kinachoinyima Ofisi ya CAG uhuru wa
kifedha ambao pia unaathiri uhuru wa kiutendaji wa Ofisi yake. “Kifungu cha 68
cha Sheria Mpya ya Bajeti kinabadili uhuru wa CAG wa kifedha uliokuwa umetajwa
kwenye Sheria ya Ukaguzi wa Umma Na. 11 ya Mwaka 2008 hiyo kuathiri utendaji wa
Ofisi ya CAG”, alifafanua Prof. Assad.
Naye Mwenyekiti wa LAAC, Mhe. Martin
Msuha (MB) alisema kuwa ni matarajio yao mwisho wa warsha hii wataweza
kuchambua ripoti za CAG kwa ufanisi zaidi pamoja na kuhoji Maafisa Masuuli
ipasavyo. “Ili nidhamu irudi katika halmashauri zetu tuna haja ya kujengewa
uwezo na kupewa muongozo wa masuala muhimu yaliyojitokeza kwenye kaguzi zenu
ili tunapokutana na Maafisa Masuuli tuweze kuwawajibisha,” alisema.
Mafunzo hayo ni muhimu kwa ajili ya
kuzijengea uwezo kamati hizo katika ukaguzi wa fedha za umma.

No comments:
Post a Comment