Waziri wa Afya, Maendeleo ya jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu akitoa tamko kuhusu Siku ya Kifua Kikuu Duniani. |
Meneja Mpango wa Taifa wa Kudhibiti Kifua kikuu na Ukoma, Dkt. Beatrice Mutayoba, akitoa ufafanuzi kwa waandishi wakati wa mkutano huo. |
Dar es Salaam
24/3/2016
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu ametoa Rai kwa wamiliki wa
vituo binafsi vya kutoa huduma za afya kupanua wigo wa huduma na kutoa
matibabu ya Kifua Kikuu katika taasisi zao.
Rai hiyo imetolewa leo jijini Dar es Salaam na Waziri huyo
wakati akitoa tamko katika kuadhimisha siku ya Kifua Kikuu duniani ambapo ufanyika
tarehe 24 Machi kila mwaka.
“Pamoja na ushiriki
mzuri katika kutoa huduma mbalimbali za afya, napenda kutoa rai kwa wamiliki wa
vituo binafsi vya afya vya kutoa huduma ya afya kupanua zaidi wigo wa huduma na
kuanza kutoa matibabu ya Kifua Kikuu katika taasisi yenu” Alisema Waziri Ummy.
Waziri Ummy amesema kuwa Serikali kupitia Wizara hiyo itatoa
ushirikiano kwa kuwapatia vifaa na dawa za matibabu ya ugonjwa wa Kifua Kikuu
ili kuhakikisha vituo binafsi vinatoa
huduma iliyo bora.
Aidha Ummy ameongeza kuwa Mikoa inayoongoza kwakuwa na idadi
kubwa ya wagonjwa wa kifua kikuu ni pamoja na Arusha, Dar es Salaam, Mara,
Mbeya, Morogoro, Mwanza, Shinyanga na Tanga.
“Takwimu za mwaka 2015 zinaonyesha kuwa mikoa hii inachangia
zaidi ya asilimia 60% ya wagonjwa wa Kifua Kikuu waliogundulika Tanzania Bara
na Visiwani” aliongeza Waziri Ummy.
Waziri Ummy ametoa wito kwa wananchi kuwa na kawaida ya
kufanya uchunguzi wa afya ili kuweza kugundua tatizo mapema na kuzuia kuenea
kwa ugonjwa wa Kifua Kikuu nchini kwani kufanya hivyo kutasaidia kupunguza
uwezekano wa kupata maambukizo mapya ya Kifua Kikuu katika jamii.
Kauli mbiu ya maadhimisho ya mwaka huu inasema “Tuungane
kutokomeza Kifua Kikuu” ambapo inaweka msukumo wa kipekee kwa nchi kuongeza
kasi ya mapambano dhidi ya Kifua Kikuu.
No comments:
Post a Comment